Habari Mseto

Kicheko bungeni Rais akihutubia taifa

November 13th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta aliubua kicheko bungeni alipokamilisha hotuba yake kuhusu Hali ya Taifa bungeni Alhamisi kwa kutamka neno la dholuo “erokamano” alipowakabidhi maspika ripoti zake.

Neno ‘erokamano” linamaanisha ‘asante’ katika lugha hiyo ya asili ya wakazi wa eneo kubwa la uliokuwa mkoa wa Nyanza. Wabunge na maseneta waliokuwa ukumbini waliangua kicheko baada ya Rais kutoa tamko hilo.

Rais Kenyatta aliwasilisha ripoti kuhusu Hali ya Usalama Nchini, Mafanikio ya Serikali katika Ushirikiano wa Kigeni na Hali ya Uchumi wa Nchini kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka dakika chache baada ya kukamilisha hotuba yake.

Naye Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alikuwa kivutio bungeni kwa mara nyingine alipohudhuria kikao hicho maalum akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni ya Kimaasai.

Bw Olekina ambaye Jumanne aliwashangaza maseneta wenzake alipoingia ukumbi akiwa amevalia mavazi hayo alisema kuwa ataendelea kuyavalia akiwa bungeni, kwa sababu “Katiba inalinda tamaduni za Wakenya.”

Spika wa Bunge la Seneti Bw Lusaka alitetea hatua yake ya kuvalia mavazi hayo akisema hakukiuka kanuni za mavazi bungeni.

“Siwezi kumfurusha Seneta Ole Kina kama alivyopendekeza Seneta wa Wajir Abdullahi Ali kwa sababu kanuni za bunge hazijapiga marufuku mavazi ya kitamaduni. Kila kaunti ya nchini ina tamaduni zake; mavazi haya yanayovaliwa na wakazi wa kaunti za Kajiado na Narok ni maarufu hata katika rubaa za kimataifa,” akasema Bw Lusaka.

Jana, Rais Kenyatta aliipigia debe mchakato wa maridhiano (BBI) huku akijifananisha na Musa katika Bibilia

Rais alisema mabadiliko ya Katiba kupitia BBI yanalenga kulinda na kudumisha mustakabali wa taifa hili.

“Kama Musa kwenye Bibilia ambaye aliketi katika Mlima Nebo na akaona mustakabali wa watu wa Israeli kwamba walikuwa wakikaribia kufikia nchi ya ahadi, mimi pia nimeona muskabali hiyo,” akasema.