Ndoto za nyota wa KCPE zafifia kwa kukosa karo

Ndoto za nyota wa KCPE zafifia kwa kukosa karo

NA WAANDISHI WETU

MAMIA ya wanafunzi waliotia fora katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE), wamo hatarini kukosa kujiunga na shule za upili kwa sababu ya umaskini.

Licha ya mashirika mbalimbali, serikali ya kitaifa, za kaunti na wahisani wengine kutangaza misaada ya kielimu, imebainika bado kuna watoto wengi ambao hawajapata fedha za kutosha kujiunga na sekondari kuanzia kesho Jumatano.

Isitoshe, duru ziliambia Taifa Leo kwamba baadhi ya wahisani wanaojitokeza hushindwa kuendeleza ufadhili hata baada ya kuwapa matumaini wanafunzi wenye mahitaji.

Japhet Katana na Ike Israel, ni kati ya wale ambao wanahangaika.

Marafiki hao wawili kutoka kijiji cha Kibusu, Kaunti Ndogo ya Tana Delta, iliyo Tana River, walifanya KCPE katika Shule ya Msingi ya Arap Moi.

Japhet alipata alama 385 na ameitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Kagumo huku Ike akipata alama 340 na kuitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Pumwani, lakini kila siku matumaini yao yanapungua kwa kukosa karo.

Wawili hao, ambao ni mayatima, sasa wanashirikiana kufanya vibarua katika shamba lolote wanalobahatika kupata kila alfajiri ili kujitafutia karo zao za shule, mbali na kufanya mahubiri mitaani.

Wanapohubiri majira ya mchana nyumba hadi nyumba na hata mitaani, wao hutoa ushuhuda kuhusu maisha yao ya tangu utotoni huku wakiomba msaada wa kuendelea na shule ya upili.

Waliambia Taifa Leo kuwa, wamejaribu kuomba ufadhili wa masomo bila mafanikio.

Mjini Mombasa, Stephen Musyoka, ambaye alipata alama 359 katika Shule ya Msingi ya Mikindani, bado anakumbwa na ukosefu wa karo.

“Ameitwa Shule ya Upili ya St Lukes iliyo Yatta. Nilikuwa nafanya kazi kwa baa lakini imefungwa sasa siwezi kumgharamia karo na mahitaji mengine ya shule. Nimejaribu kutafuta msaada lakini sijanufaika bado,” akasema mamake, Bi Josephine Mailu.

Katika Kaunti ya Lamu, Ramla Isack Haji, ambaye aliibuka nafasi ya kwanza kaunti hiyo kwa alama 409, ameeleza wasiwasi ya kukosa fedha za kutosha kuendeleza masomo yake.

Ramla alifanya KCPE katika shule ya umma ya wasichana ya Mkomani Mahmoud Bin Fadhil iliyo katika kisiwa cha Lamu.

Alichaguliwa kujiunga na Shule ya Upili ya wasichana ya Pangani iliyo jijini Nairobi.

“Niko na wanangu wawili chuo kikuu na wengine wawili wako sekondari. Mzigo wa karo umenilemea. Wahisani wakijitokeza kufadhili masomo ya binti yangu Ramla nitashukuru,” akasema babake, Bw Maalim Isack Haji.

Katika kaunti iyo hiyo, Pascal Mongare hajui hatima yake ya masomo ya sekondari baada ya kupata alama 397 katika shule ya umma ya msingi ya Lake Kenyatta iliyo mjini Mpeketoni.

Pascal Mongare hajui hatima yake ya masomo ya sekondari baada ya kupata alama 397 katika shule ya umma ya msingi ya Lake Kenyatta iliyo mjini Mpeketoni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ameitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Maseno iliyo katika Kaunti ya Kisumu.

“Mimi ni yatima. Tegemeo langu ni iwapo serikali ya kaunti itanifadhili kwa karo. Mbali na hilo, hata fedha za kugharimikia sare, mahitaji mengine na usafiri kuelekea shuleni sina,” akasema Mongare.

Abdulrashid Yunis Abdi, ambaye pia alisomea katika shule hiyo akapata alama 367 na kuitwa Shule ya Upili ya Narok, pia anakumbwa na hali sawa na hiyo.

“Ningeomba kijana wangu asaidiwe. Sina mbele wala nyuma na tayari niko na mzigo wa karo ya ndugu zake wakubwa ambao wako chuo kikuu na sekondari,” akasema mamake, Bi Nasra Hussein ambaye ndiye mlezi wao pekee.

Maeneo ya Kilifi, Alphan Musa kutoka eneo la Kiwandani alisomea Shule ya Msingi ya St Thomas na kupata alama 357, akaitwa kujiunga na Shule ya Upili ya Dr Krapf iliyo Kaunti ya Kilifi.

Wazazi wake hawana uwezo wa kumpleka shule baada ya biashara ya mamake ya kuuza chakula kuzoroteka, huku babake ambaye ni dereva wa tuktuk pia akipata mapato duni.

Moses Kombe, kutoka kijiji cha Zimbabwe mjini Kilifi, alisoma katika Shule ya Msingi ya Kibaoni akapata alama 378 na kuitwa Shule ya Upili ya Wavulana ya Ikuu, iliyo Kaunti ya Machakos.

Mamake, Bi Saumu Mwashileta alisema juhudi zake kutafuta usaidizi katika mashirika ya kibinafsi na ya serikali zimegonga mwamba.

Ramadhan Sinema aliyefanya KCPE katika Shule ya Msingi ya St Thomas na kupata alama 372 aliitwa Shule ya Upili ya Ribe iliyo Kilifi.

Mamake, Bi Esther Nyevu, alisema anafanya kazi ya uyaya pamoja na kuzunguka vijijini kuwafulia wakazi nguo na kusafisha nyumba zao. Mumewe hutegemea vibarua vya mijengo ili kupata kipato cha familia yake.

Samson Mwandoro kutoka kijiji cha Kakanjuni alisomea Shule ya Msingi ya Mabirikani, akapata alama 371 katika KCPE.

“Imekuwa vigumu kupata vibarua na waeza zunguka siku nzima bila kupata kazi na iwe vigumu hata kununua chakula,” akasema mamake, Bi Joyce Kahindi.

Katika kaunti hiyo ya Kilifi, wengine waliobainika kuwa na mahitaji ni Jedida Mkoka aliyepata alama 370, Rington Dida (379), Shauri Bahati (394), Alfred Kahindi (364), Mutua Mzinga (357), na Sidi Latifah (380).

Ripoti za Stephen Oduor, Kalume Kazungu, Winnie Atieno na Maureen Ongala

  • Tags

You can share this post!

Wafanyikazi wahimiza vita Ukraine vimalizwe

Nassir na Omar walenga wawaniaji wenza wa kike

T L