Habari Mseto

Kidege Shakira hapumui ‘mafisi’ wakiwania tunda lake baada ya kutemana na Pique

February 24th, 2024 1 min read

NA CHRIS ADUNGO

MWANAMUZIKI Shakira Isabel anazidi kuviziwa kimapenzi na vidume vizito tangu atemane rasmi na mwanasoka mstaafu raia wa Uhispania, Gerard Pique.

Mnamo Julai mwaka jana, mrembo huyo raia wa Colombia alikiri kuwa “anakaribia kupata hifadhi mpya ya penzi lake” baada ya kuonekana akiponda raha na dereva mzoefu wa magari ya Langalanga, Lewis Hamilton.

Akihojiwa na Jarida la Marca wiki hii, Shakira alibainisha kuwa ungamo lake hilo la awali “lilifungulia kila mwanamume fursa ya kujaribu bahati ya kuliwania tunda lake.”

“Sasa naviziwa sana mitandaoni, usiku na mchana. Wapo wasiolala kwa ajili yangu. Kila mmoja anaomba asali,” akasema.

Mbali na Hamilton, wanaume wengine wanaohusishwa kimapenzi na Shakira ni mwanavikapu Jimmy Butler, mwanafilamu Tom Cruise na mwanasoka wa zamani wa Amerika, Julian Edelman. Wa hivi karibuni zaidi, kwa mujibu wa Shakira, ni mwanamuziki raia wa Argentina, Rafael Arcaute.

“Mapenzi yana ajabu zake. Hisia zipo ila moyo huchoka sana nikikumbuka mambo ambayo Pique alinifanyia,” akasema Shakira.

Kipusa huyo alitemana na Pique mnamo Juni mwaka jana baada ya kuwa pamoja katika ndoa kwa miaka 12 na kujaliwa watoto wawili – Milan na Sasha.

Akihojiwa na gazeti la The Mirror, Cruise, 60, alikiri kuvutiwa kimapenzi kwa Shakira tangu zamani japo akachelea kuanzisha uhusiano naye akiwa bado katika ndoa na Pique.

“Tumeponda raha mara kadhaa. Tumetaniana sana na Shakira ila hatujawahi kuonana kimwili. Nimekuwa na mipango mikubwa ya kuishi naye raha mustarehe. Nimeshtuliwa sana na habari kwamba ananyemelewa pia na Hamilton, Butler na Arcaute,” akasema Cruise.

Hamilton amewahi kutoka kimapenzi na vichuna wengi, wa hivi majuzi zaidi akiwa mwimbaji Nicole Scherzinger aliyetengana naye mnamo 2015.

Kwa upande wake, Cruise naye hana mke kwa sasa baada ya ndoa zote tatu alizofunga na warembo Mimi Rogers (1987-1990), Nicole Kidman (1990-2001) na Katie Holmes (2006-2012) kusambaratika.