Kimataifa

Kidosho aangukia nyaya za stima akijipiga 'selfie'

July 19th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

ULYANOVSK, URUSI

MSICHANA mwenye umri wa miaka 13 alinusurika kifo alipoangukia waya ya stima kutoka kwa daraja la reli alipokuwa akijipiga selfie.

Picha zilizochapishwa na mashirika ya habari zilionyesha msichana huyo akining’inia kwenye waya ya stima.

Ilisemekana alining’inia hapo kwa karibu saa moja kabla kuonekana na mwendeshaji treni ambaye alipigia wasimamizi wa usambazaji umeme katika shirika hilo la treni wakatize umeme uliokuwa ukipitishwa kwa nyaya hizo.

Kulingana na ripoti za habari, mpitanjia alitumia kamba kumvuruta kumrudisha darajani huku wanakijiji wengine wakishikilia zulia kubwa chini yake endapo angeanguka.

Maafisa wa serikali walinukuliwa kusema alikuwa akirudi nyumbani na marafiki wake alipoamua kwenda pembeni mwa daraja kujipiga selfie wakati treni ya kusafirisha mizigo ilipokuwa ikikaribia, lakini kwa bahati mbaya akaanguka.

Wasamaria wema walimkimbiza hospitalini kwani alikuwa amechomeka katika sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mkononi, mabegani na mguu wa kushoto, kwa mujibu wa mashirika ya habari.

Madaktari walinukuliwa kusema alipata pia jeraha kichwani na alipopata fahamu baadaye hakuweza kukumbuka kilichomfanyikia.

-Imekusanywa na Valentine Obara