Habari Mseto

Kidosho afungwa nje miaka 3 kwa kumuua mumewe akiwa mlevi

January 30th, 2019 1 min read

Na GERALD BWISA

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 19 alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu kwa kuua mumewe alipofika nyumbani na mwanamke mwingine wakiwa walevi.

Bi Sheillah Chemutai Ikobwa, mama ya mtoto mmoja, alimuua Hussein Juma Nyongesa katika eneo la Matisi, Kaunti ya Trans Nzoia miaka sita iliyopita alipofika nyumbani akiwa na mwanamke mwingine.

Mahakama Kuu ya Kitale iliambiwa kwamba, mshtakiwa na marehemu walitofautiana kuhusu mgeni huyo na wakaanza kugombana.Mshtakiwa aliingia jikoni na kuchukua kisu akitaka kumdunga mwanamke huyo lakini kwa bahati mbaya alimdunga mumewe aliyekuwa akimkinga mgeni wake.

Mshtakiwa alikiri shtaka mbele ya Jaji Karanja na katika kilio chake kwa mahakama, alisema alijuta kwa kosa hilo na kuomba ahurumiwe.

Alilia mahakama akisema angemuomba msamaha mama ya marehemu. Wazazi wa marehemu walikubali kifungo cha nje na kuambia maafisa wa probesheni kwamba walimsamehe.

Walisema kwamba hawakutaka kulipwa chochote wakisema hakuna kinachoweza kujaza pengo la mpendwa wao.

“Marehemu alikuwa mwenye fujo na mraibu wa changaa na bangi, tabia ambayo ilitokana na kazi yake,”alisema mzee wa kijiji Bw John Huru. Kwa miaka mitatu ambayo atakuwa chini ya uangalizi wa maafisa wa probesheni, mwanamke huyo hafai kufanya makosa au kukiuka maagizo ya korti. Akifanya hivyo, atafungwa jela miaka mitatu.