Makala

Kidosho anayetamba kwa kuigiza kwa lugha ya mama

March 18th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

VIJANA wengi wachanga wamekuwa wakikwepa uzungumzaji na utumiaji wa lugha zao asilia.

Kutokana na wimbi la usasa, wengi wamekuwa wakijivunia uzungumzaji wa lugha ya Kiingereza ama Kiswahili, ili kutoonekana “kuandamwa na uzamani”.

Naam, ili ‘kutoaibika’ mbele ya wenzao au kutoonekana kama wasioufahamu usasa, baadhi yao hata wamekuwa wakitumia majina ya Kiingereza pekee ili kuficha asili yao!

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa mwanadada Diana Nyaboke Nyabuto, maarufu kama ‘Bonareri Actress’, ambaye amejijengea jina katika tasnia ya uigizaji nchini kwa kuigiza kupitia lugha yake asilia—Ekegusii.

Mwanadada huyu, 25, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Zetech, Kaunti ya Kiambu, anasema alilelewa katika mazingira ya kijijini, hivyo ana ufahamu wa kutosha wa lugha yake ya mama.

“Bila shaka, nina ufahamu wa kutosha wa lugha za Kiingereza na Kiswahili, kwani nimesoma hadi katika  Chuo Kikuu. Hata hivyo, hilo halifai kuwa sababu ya kujifanya kwamba sifahamu lugha yangu ya mama—yaani Ekegusii. Hilo ndilo limeifanya safari yangu ya uigizaji kuwa ya  kipekee,” akasema mwigizaji huyo mchanga.

Kutokana na weledi wake katika tasnia ya uigizaji, amefanikiwa kuigiza katika vituo vya televisheni kadhaa, baadhi vikiwa NTV, Ndizi TV (kwenye mtandao wa YouTube) kati ya majukwaa mengine.

Mara nyingi, amekuwa akiigiza kwenye video tofauti mitandaoni kwa kushirikiana na waigizaji kama Osoro Okiondo na Antivirus Sabiri kutoka Ndizi TV.

“Huwa tunachanganya uigizaji wetu kwa ucheshi, hali ambayo imetuwezesha kuvutia mashabiki wengi, kwani kando na uigizaji, huwa tunawachangamsha kwa vicheko,” akasema.

Kando na waigizaji hao, ameshirikiana na mwigizaji Smart Joker kwenye video kadhaa.

“Bado niko kwenye safari ya uigizaji. Huu ni mwanzo tu. Hata hivyo, ninaamini kwamba ikizingatiwa tayari nimepata nafasi ya kushirikiana na watu wanaojulikana katika tasnia hii nikiwa bado mchanga, naamini ndoto yangu ya kuigiza katika majukwaa makubwa zaidi itatimia,” akasema mwanadada huyo, kwenye mahojiano na Taifa Dijitali.

Safari ya uigizaji ya mwanadada huyu imekuwa ndefu, kwani alionyesha mapenzi kwa tasnia hiyo akiwa bado mchanga.

Alisomea katika Shule ya Upili ya Nyakorere kati ya 2013 na 2016. Hata hivyo, alirudia Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Bishop Mugendi Mesabakwa katika Kaunti ya Kisii mnamo 2017.

Alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Kisii mnamo 2019, alikosomea Fasheni na Utengenezaji Nguo hadi 2021. Kwa sasa, anasomea uanahabari katika Chuo Kikuu cha Zetech.

Anasema ataendelea kutilia mkazo uigizaji kwa lugha yake asili ya Ekegusii, kwani “kuna soko kubwa kwa sanaa asilia nchini’.

“Nairai serikali na taasisi husika kuweka mikakati ifaayo kukuza tasnia ya uigizaji wa lugha asilia, kwani ni sehemu ya kukuza tamaduni na desturi zetu dhidi ya kusombwa na tamaduni za kigeni,” akasema.