Kimataifa

Kidosho apaka mboni ya macho rangi na kupasua ulimi kama wa nyoka

June 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

SYDNEY, AUSTRALIA

MWANAMKE ameamua kupaka mboni ya macho yake rangi ya samawati na kufanyia ulimi upasuaji uwe kama wa nyoka kwa sababu hakupenda maumbile yake ya kawaida.

Ripoti zinasema mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Amber Luke, 23, alitumia zaidi ya dola 8,000 (Sh800,000) kufanyia mwili wake mabadiliko mengi ikiwemo kujichora tatuu mwili mzima.

Alipohojiwa na wanahabari, alisema shughuli nzima ya kubadilisha rangi ya macho yake ilikuwa ya maumivu mengi na hangeweza kuona vyema kwa wiki tatu lakini hajutii uamuzi wake.

“Sijuti hata kidogo. Napenda sana maumbile yangu mapya. Kuna watu wengi ambao hujaribu kunifanya nijutie maamuzi ya kubadilisha maumbile ya mwili wangu lakini hawataweza. Mwili ni wangu,” alinukuliwa kusema.

Hata hivyo, aliongeza kuwa watu wengi zaidi huwa wanavutiwa na maumbile yake na hutaka kujua mengi zaidi kumhuzu, ikiliganishwa na idadi ambayo humkejeli au kumdharau.

Ilisemekana sasa anataka kufanya meno yake yawe kama ya mnyonya damu.

Imekusanywa na Valentine Obara