Michezo

Kidume cha mbegu: Neymar atarajia mtoto wa tatu!

January 5th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

FOWADI mzoefu wa Brazil, Neymar, anatazamiwa kuwa baba mzazi kwa mara ya tatu.

Tovuti ya LeoDias nchini Brazil, imefichua kwamba mama wa kimalaika hicho kinachotarajiwa na Neymar ni mwanamitindo ambaye sasa ana ujauzito wa miezi mitatu.

Yasemekana habari za ujauzito huo zilimshangaza pia Neymar, ambaye kwa sasa anapata nafuu kutokana na upasuaji wa goti unaotarajiwa kumweka nje ya michuano ya Copa America mwakani.

Tovuti nyingine ya burudani, Segue A Cami, ilichapisha maoni yaliyopakiwa mtandaoni na mwanamitindo Jamile Alima akiambatanisha picha ya mtoto wa pili wa Neymar, Mavie, aliye na umri wa wiki sita.

“Mavie utapata kaka mdogo kutoka kwa baba Ney hivi karibuni. Tofauti kati yenu kiumri itakuwa ni mwaka mmoja pekee,” akaandika Jamile.

Taarifa iliyochapishwa na LeoDias ilisema: “Neymar anatarajia mtoto wa tatu kutoka kwa mwanamitindo mmoja aliyemburudisha miezi mitatu iliyopita. Ilivyo, yaelekea Neymar alionjeshwa asali akiwa bado anauguza jeraha la goti.

Kuna wasiwasi kuhusu afya ya mama wa mtoto. Alilazwa hospitalini kwa siku mbili hivi karibuni na kuruhusiwa kuendelea na matibabu akiwa nyumbani. Naye hakutarajia kabisa ujauzito huo na angali katika mshangao.”

Ni miezi miwili pekee imepita tangu aliyekuwa mchumba wa Neymar, Bruna Biancardi, athibitishe kutengana rasmi na sogora huyo wa zamani wa Barcelona na Paris Saint-Germain (PSG). Bruna alikatiza uhusiano na Neymar baada ya kufichuka kuwa nyota huyo wa klabu ya Al Hilal nchini Saudi Arabia, aliagiza kahaba amtumie picha za uchi mtandaoni.

Aline Farias ambaye hunadi picha na video za uchi kwenye jukwaa la OnlyFans aliweka wazi jumbe anazodai kutumiwa na Neymar akimsihi amrushie “burudani ya macho” kabla ya kumpangia “mechi ya siri”.

Ingawa Neymar alikana madai hayo, Bruna alifanya uamuzi wa kujiendea zake wiki chache tu baada ya uhusiano wake na Neymar kujaliwa mtoto wa kike, Mavie.

Aliandika kwenye mitandao ya kijamii: “Hili ni suala la faragha. Lakini vyema niwaambie kuwa siko tena kwenye uhusiano.”

Hata hivyo, mimi na Neymar ni wazazi wa Mavie na hicho ndicho cha pekee kinachotuweka pamoja. Natumai mtaelewa.”

Dalili za Bruna kutemana na Neymar zilianza kuwa wazi mnamo Juni mwaka jana baada ya mwanasoka huyo kunaswa na kamera akisisimuana kimapenzi na wanawake wawili tofauti wakati mchumba wake akiwa bado mjamzito.

Aliwahi pia kupapurwa peupe na kisura mmoja aliyekataa mistari yake ya mapenzi walipokutana kwenye hafla moja ya usiku iliyohudhuriwa na wageni 35 katika mkahawa wa Mangaritiba jijini Rio de Janeiro, Brazil, mnamo Septemba 2023.

Neymar ana mtoto wa kiume anayeitwa Davi Lucca, 11, kutokana na uhusiano wake wa awali na kidosho Carolina Dantas aliyeanza kumfungulia mzinga wa asali akiwa na umri wa miaka 19.

Hapo awali, nyota huyo alichumbiana pia na mwigizaji maarufu wa Brazil, Bruna Marquezine, kwa miaka sita kabla ya kutemana rasmi 2018.