Makala

KIELELEZO: Alipuuzwa akianza ila sasa ufanisi wake unavutia wengi

August 29th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na CORNELIUS MUTISYA

WAKATI Moses Musau aliamua kujitoma mzimamzima katika bahari ya kilimo mnamo mwaka wa 1995, watu wengi walimpuuza.

Walidai eti alikuwa anapanda tufani na kuvuna upepo wasijue hiyo yao ilikuwa fikra ya kukosa kujiamini.

Zaidi ya miongo miwili baadaye, Bw Musau ameondokea kuwa mkulima maarufu wa mboga za kila sampuli janibu za Ukambani.

Hakika, ameondokea kuwa fahari kuu kwa watu wa eneo hili kutokana na sababu kwamba amebobea katika kilimo katika maeneo kame; hasa upanzi wa mboga za kiasili aina ya marenge inayojulikana kwa kimombo kama cojets.

“Sikujali maneno ya watu. Niliamua kujikakamua na kutia bidii ya mchwa katika ukulima wangu na sasa nachuma faida kutokana na kazi ya mikono yangu,’’ Bw Musau anasema.

Anaongeza kuwa alianza kazi ya ukulima kwa mtaji wa Sh200 pekee alizopewa na wazazi wake. Alitumia hela hizo kununua mbegu za nyanya na miche ilipokomaa, akazipanda katika shamba dogo la nusu ekari.

“Kilimo cha nyanya kilifaulu mno. Nilipata faida ya Sh100,000 baada ya miaka miwili. Nilitumia sehemu ya pesa hizo kufungua biashara ya duka katika kituo cha kibiashara cha Mutini,” asema Bw Musau aliyezaliwa katika kijiji cha Ting’ang’a, kata ya Iveti, Machakos.

Mnamo mwaka wa 2000 mkulima huyu alianza kukodisha mashamba kutoka kwa majirani ili kuendeleza kilimo chake kikamilifu. Aliamua kuingilia kilimo mseto.

“Nilipanda mboga za sukuma wiki, nyanya, mishiri, mnavu na marenge,” aeleza mkulima huyu mkakamavu.

Musau anasema kwamba, kwa kuwa eneo hilo hukumbwa na kiangazi cha kipindi kirefu, alianza mpango wa kuhifadhi maji ya mvua na kuyatumia kunyunyizia mimea yake nyakati kama hizo.

“Hatua hii imeniwezesha kupata mazao mazuri kila msimu. Isitoshe, baadhi ya mashamba niliyokodisha yako karibu na mto ambapo mimi hutumia maji hayo pia kunyunyizia mimea,” anaeleza.

Baada ya miaka minne, Musau anaongeza, aliweza kupata pesa za kununua shamba kubwa la ekari tatu ambako amekuwa akiendeleza kilimo mseto hadi wakati huu.

“Namaanisha kuwa niweza pia kupanua mawanda yangu na kuweza kufuga ng’ombe wachache wa maziwa kuku, nguruwe na hata kondoo,” anatufichulia.

Na je, soko la mazao yake inapatikana wapi? “Huwa ninauza mazao yangu katika soko la Marikiti mjini Machakos. Saa zingine huwa nauzia shule, hospitali, mikahawa na vyuo vya mafunzo ya kiufundi,” Bw Musau anafichua.

Sh1 milioni

Mkulima huyu anakadiria kuwa mwaka mmoja mapato yake kutoka kwa fani zote za kilimo ni takriban Sh1 milioni, kabla ya kuondoa gharama zote.

“Baada ya kuondoa gharama mimi husalia na pesa nzuri ambayo zimeniwezesha kugharama masomo ya watoto wangu hadi viwango vya elimu ya juu,” Bw Musau anaeleza. Ili kuhakikisha amefaulu itakikanavyo katika shughuli zake mkulima huyu amewaajiri vijana sita kumsaidia Mkewe naye hujishughulisha na harakati za kusaka soko za mazao ya shambani na kutokana kwa mifugo.

Anasema amebaini kuwa kinachofelisha kilimo katika maeneo ya Ukambani ni ukosefu wa maji. Kwa mintaarafu hii anaiomba serikali ya kaunti ya Machakos iwachimbie wakazi mabwawa mengi ili waweze kupata maji ya kuendeleza kilimo, hasa nyakati za kiangazi.

“Kilimo ndicho tegemeo kuu kwa watu wa maeneo haya. Kwa sababu hii, tunafaa kuchimbiwa mabwawa mengi ili tujitume kwa kilimo na kujiimarisha kiuchumi,’’ aeleza Bw Musau.

Anawashauri vijana wakumbatie kilimo badala ya kulaza damu manyumba kisha kupoteza matumaini maishani na kujiunga na magenge ya wahalifu.

“Vijana ndio viongozi wa kesho. Hata kama kazi za ofisi zimeadimika haifai kwa vijana kuvunjika moyo na kupoteza dira ya kimaisha. Wanafaa kuingilia kilimo na bila shaka wataona faida na manufaa yake,” Bw Musau anashauri.