HabariSiasa

‘Kieleweke’ wadai Ruto anavuruga viongozi Mlima Kenya

May 14th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

VIONGOZI kadha wa Mlima Kenya wamemhusisha Naibu Rais, Dkt William Ruto na mgawanyiko unaokumba eneo hilo.

Wanadai mienendo yake ya kumkaidi Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu kampeni za mapema ni chanzo cha mgawanyiko huo wa viongozi katika ngome ya Rais.

Wengi wao, wanahisi Dkt Ruto amekuwa akimkaidi Rais Kenyatta kwa ‘kufadhili’ viongozi wa Mlima Kenya ilhali wao ndio wanapasa kuwa katika mstari wa mbele kutekeleza ajenda za Rais.

Wakiongozwa na Mbunge Maalum, Bw Maina Kamanda, Mbunge Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kiambu, Bi Gathoni wa Muchomba, na Mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Ngunjiri Wambugu, viongozi hao walidai Dkt Ruto amesababisha mtafaruku katika eneo hilo ambalo limekuwa na umoja kisiasa kwa miaka mingi.

Kulingana na Bi Wamuchomba, shida zilianza wakati Rais alipoalika viongozi wote wa kisiasa walioshinda uchaguzini katika Ikulu ya Nairobi na ya Nyeri mnamo Septemba 30, 2018, akawaagiza wakomeshe kampeni za mapema zinazohusu uchaguzi wa urais wa 2022.

Alikuwa ameahidi wakati ukifika, atasimamia kampeni za urais kumpigia debe Dkt Ruto na kusisitiza wakati haujafika kuendeleza siasa nchini.

“Alifafanua maono yake ya nchi hii akatushauri tusiwe tukitangatanga maeneo tofauti ya nchi bali tukae katika maeneobunge yetu kufanyia kazi wapigakura. Lakini Dkt Ruto hakufuata agizo la mkubwa wake bali ‘alinunua’ viongozi kumpigia debe kwa urais na hatua hiyo ilitufanya tuzinduke kuipinga,”?akasema Bi Wamuchomba.

Alitaja matukio matatu ambayo yalionyesha Dkt Ruto hamtii Rais Kenyatta kama vile kuhusu utathmini wa utajiri wa watumishi wa umma, vita dhidi ya ufisadi ambapo alidai maafisa wanaoendesha juhudi hizo ni wakora, na kusitasita kwake kujisajili kwa Huduma Namba.

Alizidi kusema wakati wa kampeni, Rais hakuwahi kuzuru eneo la Rift Valley bila kuandamana na Dkt Ruto ilhali yeye amekuwa akienda katika ngome ya kisiasa ya Rais bila kushauriana naye.

Kwa upande wake, Bw Kamanda anaamini Dkt Ruto ndiye atapata hasara kubwa zaidi kwenye mgawanyiko aliosababisha kwani asipopata uungwaji mkono kikamilifu Mlima Kenya ifikapo 2022, itakuwa vigumu kwake kushinda urais.

“Ataona matokeo yake ifikapo Uchaguzi Mkuu mwaka wa 2022,” akasema Bw Kamanda.

Lakini kuna viongozi walio wandani wa Naibu Rais wanaohisi kwamba kimya cha Rais Kenyatta kuhusu mizozo ya kisiasa nchini ndio kimesababisha hali kuwa mbaya zaidi na wanataka kuwe na mkutano wa dharura wa wabunge ili kurekebisha hali.

Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro alidai serikali inafadhili wapinzani wa Dkt Ruto kuendeleza kampeni dhidi yake, ingawa madai hayo hayangeweza kuthibitishwa.

“Huwa wanajigamba mbele zetu jinsi wanavyofadhiliwa kueneza chuki na kampeni dhidi ya Naibu Rais, lakini tunataka watangaze wanamuunga nani mkono kwa urais kwani sisi tayari tuna mgombeaji wetu,” akasema.

Mchanganuzi wa siasa katika Kaunti ya Murang’a, Bw George Nyoro pia alimlaumu Rais kwa misukosuko ya kisiasa Mlima Kenya na kusema Rais huonekana kana kwamba anachukia sana mrengo wa Tangatanga ilhali yuko kimya kuhusu Kieleweke ambayo pia inaendeleza siasa.