Kieni: Kanini Kega akubali sauti ya wapigakura akae kando

Kieni: Kanini Kega akubali sauti ya wapigakura akae kando

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa sasa Kieni, Kanini Kega Jumatano ametangaza kukubali kushindwa kuhifadhi kiti chake baada ya matokeo ya kura kuashiria huenda mpinzani wake akamrithi.

Katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9, 2022, Bw Kega alimenyamana na Wainaina Antony Njoroge (UDA).

Kega ambaye alikuwa anagombea kuingia bungeni awamu ya tatu, aliwania kwa tiketi ya Jubilee.

“Kufungua chapta nyingine, mlango mmoja unapofungika mwingine unafunguka…” mbunge huyo amechapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Kwenye chapisho hilo la saa chache zilizopita, Kega amesema anaelekea Ukumbi wa Bomas of Kenya, Kituo Kikuu cha kuhesabu na kujumlisha kura za uchaguzi wa urais na kutangaza atakayeibuka mshindi.

Amechukua hatua hiyo kwa sababu katika eneobunge hilo la Kieni, matokeo kutoka vituo mbalimbali yanayoendelea kuwasilishwa na kusomwa, japo idadi jumla haijatangazwa rasmi, yanaashiria Bw Wainaina wa UDA anaongoza.

Mbunge wa Kieni anayeondoka Kanini Kega akipiga kura Agosti 9, 2022. PICHA | SAMMY WAWERU

Kwenye mahojiano na vyombo vya habari Jumanne baada ya kupiga kura yake katika Shule ya Msingi ya Kahuho, Naromoru mbunge huyo alisema endapo atabwagwa ataitikia matokeo.

“Nikishindwa, nitakubali matokeo,” Kega akaahidi.

Mwanasiasa huyo hata hivyo alilamikia idadi ya chini ya wapigakura eneo la Mlima Kenya.

“Sababu kuu ya idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza ni kwamba mwaka huu 2022 hatujakuwa na mgombea wa urais mwenye ushawishi mkubwa kutoka eneo hili,” akaambia wanahabari.

Shughuli ya kuhesabu kura za Kieni na kujumlisha inaendelea katika Shule ya Upili ya Mweiga.

  • Tags

You can share this post!

Man-United wajiondoa katika mbio za kumsajili fowadi Marko...

TUSIJE TUKASAHAU: Kenya yajikokota kusaka fidia kwa familia...

T L