Makala

Kifaa cha kisasa cha kufugia nyuni

September 15th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Teknolojia ya kisasa imekuja na mbinu nyingi za kuboresha ufugaji, hasa kwa wakulima wadogo na wakubwa waliojikita katika kilimo biashara.

Mfano mzuri wa kupigiwa darubini ukiwa ni ule wa kufuga kuku, ambapo njia mbadala imezinduliwa baada ya wakulima kushirikiana na kundi la akina mama la Kenya Women kubuni kifaa cha kulinda ndege wako.

Ufugaji wa kuku ni chanzo cha kumwongezea mkulima mapato hasa wale wanaokaa mashambani.

Aidha bidhaa zinazotokana na kuku zinaweza kumpatia mkulima faida kubwa ,endapo atazingatia taratibu zote na kukabiliana na changamoto.

Kuku wa nyama na mayai ni fursa nzuri ya kutoa ajira kwa vijana wengi waliosoma na kuhitimu lakini hawajapata kazi kwa sababu ya ongezeko la soko kubwa la mahitaji ya bidhaa hizi.

Akilimali ilitembelea maonyesho ya kilimo ya Nakuru mapema mwezi huu na kutangamana na shirika la Kenya Women ambalo limevumbua kifaa cha kisasa kinachoweza kutimiza mahitaji yote ya ufugaji.

Kulingana na mkurugenzi wao Micah Makori mkulima anaweza kufanya shughuli zake bila kutumia wakati wake mwingi kuwaangalia kuku wake.

Micah Makori akielezea jinsi kifaa cha kufugia kuku hutumika ili kukidhi mahitaji ya ufugaji. Picha/ Richard Maosi

Kifaa hiki kina sehemu ya kuwalisha kuku,kuhifadhi mayai na mzunguko wa maji unaohakikisha kuwa ndege wako hawapungukiwi na maji wala kiwango sahihi cha lishe.

Micah anasema kuwa wakulima wengi wanafaa kuhimizwa wawe wakitembelea maonyesho ya kilimo,kila wakatii ili wajiongezee ujuzi katika sekta ya ufugaji.

Alieleza kuwa mfugaji hawezi kutumia wakati mwingi kuwakagua ndege wake na badala yake atumie wakati wake kufanya kazi nyinginezo za kujiongezea kipato..

Micah alifichulia Akilimali kuwa kuku wa gredi ndio wanalengwa sana, kwa sababu hawana hulka ya kutembea kila sehemu kama wale wa kienyeji wasioweza kutulia sehemu moja.

Kifaa hiki kimegawanywa katika sehemu ya vyumba vidogo vilivyozungukwa kwa waya na kila sehemu inaweza kubeba kuku wanne bila kusababisha msongamano.

Anasema sio lazima mkulima awe na sehemu ya ardhi kufugia ndege wake,ila jambo la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa sehemu ya kufuga inapata usalama wa kutosha.

Micah Makori akimhudumia mmoja wa kuku. Picha/ Richard Maosi

Kifaa hiki kimegawanyika katika sehemu ya kuweka lishe,sefu za kuhifadhi mayai na paipu za kuzungusha maji hadi kwenye makasha yaliyotengwa kimakusudi kubeba maji.

Vilevile kuku hawawezi kula mayai yao pindi yanapotagwa kwa sababu huingia katika sehemu tofauti ambayo haiwezi kufikika hata wakijaribu kudona namna gani.

“Kwa kuwa kifaa hiki kimeinuliwa sio rahisi kuku kupata maradhi,mara nyingi maana, hawapati fursa ya kukanyaga ardhi iliyojaa vimelea na uchafu wa aina mbalimbali,”akasema Micah.

Micah anasema ufugaji wa kuku unaweza kumpatia mkulima faida nyingi kwa sababu hutoa ajira,mbolea na wakati mwingine kuzalisha nishati ya kawi.

Micah anaamini kuwa kwa kigezo hicho wakenya wengi hawawezi kukwepa jukumu la kutekeleza kilimo kwa sababu bado ni uti wa mgongo kwa uchumi wa taifa hili.