Habari Mseto

Kifaru mweupe wa mwisho duniani aaga kwa kuzeeka

March 21st, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

KENYA na ulimwengu kwa jumla Jumanne waliamkia majonzi, baada ya kifaru wa kiume aina ya Nothern White Rhino wa mwisho duniani kufariki akiwa na miaka 45 katika mbuga Laikipia.

Hadi kifo chake, faru huyo aliyepewa jina Sudan hakufanikiwa kuzaa, na kuibua hofu ya vifaru hao kuangamia.

Mnyama huyo alikuwa kwenye hifadhi ya Ol-Pejeta iliyoko Kaunti ya Laikipia, baada ya kuhamishiwa huko kutoka taifa la Czech.

Walikuwa wamesalia vifaru wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike hadi 2014 pale mmoja wa kiume alipoaga na kumwacha Sudan kama kifaru wa pekee wa kiume aina ya Nothern White Rhino duniani.

Katika hifadhi hiyo waliishi pamoja na wawili wa kike, Najin (29) na Fatu (18). Kifaru huyo alishindwa kuendeleza kizazi kutokana na uzee.

Asubuhi ya Jumanne, hifadhi ya Ol-Pejeta pamoja na ile ya Dvur Kralove kutoka taifa la CZech ziliztoa taarifa zikisema kifaru huyo aliaga Machi 19.

“Sudan alikuwa akitibiwa hitilafu zinazohusiana na uzee ambazo zilipelekea mabadiliko ya kumdhoofisha misuli na mifupa pamoja na vidonda vikubwa ngozini,” ikasema taarifa yao.

“Hali yake ilidhoofika zaidi kwa saa 24 zilizopita ambapo alishindwa kusimama na alikuwa akiumia kiwango kikubwa. Kundi la madaktari wa wanyama kutoka hifadhi ya Dvur Kralove, Ol Pejeta na shirika la uhifadhi wa wanyamapori (KWS) ziliamua kumpa dawa ya kumpumzisha.”

Kulingana na taarifa yao, kizazi cha kifaru huyo kiliepuka kuangamia miaka ya sabini wakati Sudan alipohamishiwa hifadhi ya Dvr Králové. Katika uhai wa kifaru huyo, alifanikiwa kuzaa wana wawili wote wa kike.

Kulingana na chembechembe za kibayolojia zilizochukuliwa na wanasayansi jana, kuna imani kwa kizazi cha vifaru hao kuendelea kupitia mbinu za uzalishaji wa kisayansi na teknolojia.

“Sisi kutoka Ol Pejeta tumetamaushwa na kifo cha Sudan. Alikuwa balozi mkubwa na kizazi chake na atakumbukwa kwa kazi ya kuchangia juhudi za kulinda vizazi vya wanyama wengine wa porini kuokolewa,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Ol Pejeta Richard Vigne.

Sasa, ulimwengu umeachiwa vifaru wawili pekee wa kike wa aina hiyo, wote wakiwa katika hifadhi hiyo.