Kimataifa

Kifaru mweusi mkongwe zaidi afariki nchini Tanzania

December 30th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

KIFARU anayesadikiwa kuwa mkongwe zaidi duniani alikufa nchini Tanzania akiwa na umri wa miaka 57.

Fausta ambaye ni kifaru mweusi wa kike, alionekana kwa mara ya kwanza katika eneo la Ngorongoro Crater mnamo 1965, akiwa mwenye umri wa miaka mitatu.

Aliishi hapo kwa muda wa miaka 54 lakini baada ya matatizo ya kiafya na ukongwe ulisababisha kuhamishwa kwake hadi katika hifadhi fulani ambako amekuwa akipokea utunzi maalumu.

Fausta, hakujaaliwa uwezo wa kupata watoto, hali ambayo ilichangia wataalamu wa utunzaji wanyamapori katika eneo la Ngorongoro kukisia ndiyo ilisababisha kuishi kwake kwa miaka mingi.

Mnamo mwaka wa 2016 kifaru huyo alianza kupoteza uwezo wa kuona kando na kuuguza majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa na fisi.

“Wanyamapori kama vile chui walianza kumshambulia na ndipo akapata vidonda vingi,” Kamishna Dkt Freddy Manongi, kutoka Mamlaka ya Hifadhi eneo la Ngorongoro (NCAA) aliambia wanahabari.

“Kufikia mwaka wa 2016, ilitubidi kumwondoa msituni na kumweka chini ya utunzaji maalum,” akaongeza.

Dkt Manongi aliongeza kuwa siku ambayo Fausta alifariki, kifaru mwingine alizaliwa, yaani mnamo Desemba 27, 2019.

Kwa kawaida, vifaru huishi katika mazingira ya msituni kwa kati ya miaka 37 na 43, au hadi miaka 50 wakiwa wakifungiwa.

Vifaru weusi wanasemekana kukabiliwa na hatari ya kuangamia. Idadi yao inapungua kwa sababu huuawa na wawindaji haramu wakitaka kuuza pembe zao.