Habari

Kifo cha diwani wa Kahawa Wendani chaacha wengi na mshangao

February 13th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa wadi ya Kahawa Wendani wanaendelea kuomboleza kifo cha MCA wao Bw Cyrus Omondi, aliyefariki akiwa ziarani India.

Kifo chake kilithibitishwa na Spika wa bunge la Kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu, aliyesema alifariki akiwa katika ziara ya kikazi kwenye hoteli aliyokodisha nchini India.

Habari hizo pia ziliwasilishwa nchini kupitia afisa mmoja katika idara ya nchi za kigeni, Bw Rono Kosigi.

Wakazi wa eneo lake la uwakilishi – Kahawa Wendani – na familia yake bado wameachwa na mshangao mkubwa wakitaka haki itendeke kupata ukweli kamili kilichomuua diwani huyo.

Bw Omondi aliandamana na viongozi wengine watatu kutoka Kaunti ya Kiambu katika ziara hiyo.

Baadhi ya viongozi hao walioandamana na marehemu ni Bw Joseph Kang’ethe, afisa mkuu katika kaunti ya Kiambu, Bw Isaac Mwaura, afisa katika idara ya elimu, na Bi Susan Wanjiku ambaye ni MCA maalumu.

Kifo cha diwani huyo kimewaacha wenzake – MCAs 92 – katika bunge la Kaunti ya Kiambu katika mshangao mkubwa huku kila mmoja asijue la kusema.

Imeelezwa kuwa katika bunge la kaunti ya Kiambu alikuwa mkakamavu katika mijadala huku akijieleza bila kuwa na wasi wasi wowote.

Bw Omondi alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama MCA katika wadi ya Kahawa Wendani kaunti ya Kiambu mnamo 2017 ambapo aliingia na tiketi ya chama cha Jubilee, jambo lililoshangaza wengi.

Yeye kama mtu aliyetoka sehemu za Nyanza ilikuwa ni vigumu sana kuchaguliwa lakini kwa sababu alikuwa na uhusiano mwema na vijana katika mashinani aliweza kupata kura nyingi ajabu uchaguzini.

Alikuwa akifanya kazi ya umekanika katika eneo la Kahawa huku akishirikiana vyema na wakazi wa mahali hapo.

Pia alizungumza lugha ya Gikuyu kwa ufasaha, na ameweza kuishi eneo hilo tangu utotoni mwake.

Kutokana na kifo chake Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wametuma salamu zao za pole kupitia kurasa zao za mitandao wa kijamii.

Kwa majina ya utani alijulikana kama Mtambo wa Reli ama Gear Box ambapo alifanya kazi yake kwa uwazi, unyenyekevu na ukakamavu.

Bi Gathoni Wa Muchomba mwakilishi wa wanawake Kiambu, na Bw Isaac Mwaura ambaye ni Seneta maalum wamepatwa na mshangao kufuatia kifo cha MCA huyo ambaye alishirikiana nao kwa karibu sana.

“Mimi kama rafiki wake wa karibu nimeshindwa la kusema kufuatia kifo hicho. Alikuwa kiongozi aliyesimamia haki kwa watu anaowawakilisha na hakuwa na ubaguzi wowote kwa wakazi wa Kahawa Wendani,” alisema Bw Mwaura.

Mwingine ni Mwakilishi wa Wanawake wa Kianbu katika Bunge la Kitaifa Bi Gathoni Wa Muchomba.

“Bw Omondi amekuwa mtumishi aliyependwa na wengi na alifanya kazi yake bila ukabila. Tumempoteza kiongozi shupavu,” alisema Bi Muchomba.

Mashabiki wake wengi na wakazi wa Kahawa Wendani bado wanataka kujua ukweli wa mambo kwa sababu bado hawajaamini chanzo cha kifo hicho.

Bi Millicent Odhiambo ambaye ni mamake mzazi ametaka uchunguzi kamili ufanywe ili kubainisha ukweli wa mambo.

“Tungetaka serikali ifanye hima kuona ya kwamba kitendawili cha kifo cha mwanangu mpendwa kimeteguliwa,” alisema mamake.

Bw Omondi anatoka katika kaunti ya Siaya na wengi wamekuwa wakishangazwa na jinsi alivyochaguliwa kama MCA katika eneo la Mlima Kenya.