Kifo cha Mbunge chaongeza mkosi kwa Bunge la 12

Kifo cha Mbunge chaongeza mkosi kwa Bunge la 12

Na CHARLES WASONGA

KIFO cha Mbunge wa Juja, Francis Munyao Waititu mnamo Jumatatu, kinafikisha idadi ya wabunge na magavana waliofariki katika Bunge la 12 kuwa kumi.

Bw Waititu alifariki katika hospitali ya MP Shah, Nairobi Jumatatu usiku baada ya kuugua kansa ubongo.

Kufikia sasa, jumla ya wabunge sita na maseneta wawili wamefariki wakiwa afisini, idadi kubwa ya wajumbe ambayo haijawahi kushuhudiwa nchini.

Ifuatayo ni orodha ya wabunge na maseneta ambao wamefariki tangu mwanzo wa kipindi cha kuhudumu cha Bunge la 12.

KEN OKOTH (Mbunge wa Kibra, ODM)

Alifariki mnamo Julai 26, 2019 katika Nairobi Hospital ambako alikuwa amelazwa akiugua kansa ya utumbo. Marehemu Okoth aliyefariki akiwa na umri wa miaka 41, alikuwa akihudumu muhula wa pili kama mbunge wa Kibra, kaunti ya Nairobi.

SULEIMAN DORI (Mbunge wa Msambweni, ODM)

Alifariki mnamo Machi 9, 2020 katika Hospitali ya Aga Khan Mombasa ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu. Hata hivyo, familia yake haikufichua ni ugonjwa gani alikuwa akiugua.

JUSTUS MURUNGA (Mbunge wa Matungu, ANC)

Alifariki mnamo Novemba 14, 2020 akikimbizwa katika hospitali ya St Mary’s Mumias baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua nyumbani kwake katika kijiji cha Makunda, eneo bunge la Matungu.

Awali, Bw Murunga alikuwa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, Kisumu kwa muda wa majuma mawili, akitibiwa ugonjwa wa kisukari. Alikuwa akihudumu muhula wake wa kwanza bungeni.

JAMES LUSWETI MUKWE (Mbunge wa Kabuchai, Ford Kenya)

Hadi kifo chake mnamo Desemba 5, 2020 marehemu alikuwa akihudumu muhula wa pili kama mbunge wa Kabuchai.

Alifariki katika Nairobi Hospital ambako alikuwa akitibiwa ugonjwa wa yabisi, (arthritis), kulingana na familia yake.

BONIFACE MUTINDA KABAKA (Seneta wa Machakosa, CCU)

Kifo cha seneta Kabaka kilitokea mnamo Desemba 11, 2020 baada ya kuzirai akikimbikizwa hospitalini. Upasuaji uliofanyiwa maiti yake ulibainisha kuwa alifariki kutokana na kuganda kwa damu ubongoni mwake. Alikuwa akihudumu muhula wa kwanza katika seneti.

JOHN OROO OYIOKA (Mbunge wa Bonchari, PDP)

Bw Oyioka alifariki mnamo Februari 15, 2021 katika hospitali ya Aga Khan, Kisumu ambako alikuwa amelazwa baada ya kuugua kiharusi. Marehemu alikuwa akihudumu muhula wa pili bungeni.

YUSUF HAJI (Seneta wa Garissa, Jubilee)

Seneta Haji ambaye pia alihudumu kama Mwenyekiti wa Jopo ya Maridhiano (BBI) alifariki mnano Februari 14, 2021 katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Nairobi. Mzee Haji, aliugua kwa muda mrefu na aliwahi kutibiwa nchini Uturuki. Alifariki akiwa na umri wa miaka 80.

Watu wengine mashuhuri waliofariki baada ya uchaguzi wa 2017 ni magavana Wahome Gakuru (Nyeri), Joyce Laboso (Bomet) na John Nyagarama (Nyamira).

You can share this post!

Olunga hatimaye achezeshwa mechi nzima na Al Duhail ikizima...

Wito kwa vinara wa NASA waungane upya