Habari Mseto

Kifo cha Moi na biashara jijini Nairobi

February 11th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa wiki moja jiji la Nairobi limekuwa lenye shughuli chungu nzima tangu kitokee kifo cha Rais wa Pili wa Jamhuri ya Kenya Mzee Daniel Toroitich Arap Moi.

Usalama umeimarishwa vilivyo hasa katika majengo ya bunge na maeneo ya karibu, ambako mwili wa Rais huyo Mstaafu ulikuwa kwa muda wa siku tatu mfululizo Wakenya kuutazama na kumpa heshima za mwisho.

Maafisa kutoka vitengo mbalimbali vya idara ya usalama wanaendelea kupiga doria, huku hafla ya wafu Jumanne ikifanyika katika uga wa Nyayo, Nairobi.

Shughuli za kuutazama mwili wa marehemu zilifanyika kati ya Ijumaa na Jumapili, foleni ndefu za watu zikishuhudiwa.

Wananchi walistahimili miale kali ya jua.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya raia wenye ubunifu hasa katika uchoraji walijituma kutuliza nyoyo za waliokuwa kwenye foleni kwa minajili ya kuutazama wa Mzee Moi. Waliandaa beji na kalenda zenye picha na machapisho ya jumbe za heri njema kwa Mzee na familia yake.

Lilian Mumbi, ni mmoja wa wasanii waliosambaza beji kwa ada ya Sh20 pekee, iliyochapishwa picha ya Moi na mkewe Lena, yenye upini na ambayo inatundikwa kwenye mfuko wa shati au blauzi.

“Nilifakari njia ya kumpa heshima za mwisho Rais Moi, nikaona nitumie talanta yangu kuandaa beji zenye jumbe za heri njema,” Mumbi akasema.

Beji hizo zilikuwa na ujumbe “Mungu ailaze roho yako mahali pema Rais Daniel Toroitich Arap Moi”, Mkenya huyo akieleza kwamba ni mmoja wa waliopata maziwa ya Nyayo, wakati akiwa chekechea. Beji hizo pia zina bendera ya Kenya.

Mumbi alisema kufikia Jumamosi jioni alikuwa ameuza zaidi ya beji 500. Pia, kuna waliochuuza kalenda za 2020 zenye picha ya Moi na mkewe, pamoja na watoto wao. Kalenda ziliuzwa kati ya Sh50 – 100, kulingana na saizi.

Mzee Moi aliaga dunia wiki iliyopita katika Nairobi Hospital wakati akipokea matibabu. Alichukua hatamu ya urais 1978 baada ya kifo cha Rais Mwanzilishi wa taifa hili Mzee Jomo Kenyatta.

Bw Moi alitawala Kenya kwa miaka 24. Hata ingawa umri wake haujulikani, alifariki akiwa na miaka 96, baadhi wakidai huenda akawa na zaidi ya miaka 100.