Habari

Kifo kingine feri mwanamume akidaiwa kutumbukiza gari lake

December 7th, 2019 2 min read

NA MOHAMED AHMED

MWANAMUME aliyekufa baada ya kutumbukiza gari lake baharini kwenye kivuko cha Likoni, Mombasa alikuwa na hasira na kuzongwa na mawazo, waliomuona kabla ya tukio hilo wamesema.

John Mutinda alikuwa amevalia suruali fupi pekee na kifua chake kilikuwa wazi.

Iliripotiwa kuwa alichukua gari lake kutoka nyumbani kwake mtaa wa Vanga eneo la Likoni na kuliendesha kwa kasi mwendo wa saa kumi alfajiri.

Kabla ya kutumbukia baharini, Mutinda aligonga pikipiki iliyokuwa karibu na gari lake wakati aliondoka kwa mwendo huo wa kasi na kuelekea hadi katika kivuko cha Likoni ambapo alijitosa baharini.

Mlinzi wa gari lake aina ya Toyota Allion nambari ya usajili KAX 474B, Bw Mbithi Matheka, alisema kuwa jamaa huyo alionekana kuwa na hasira na mawazo mengi wakati huo.

“Alikuja hapa bila kusema lolote lile. Alituangalia kwa muda akionekana kuwa kama amechanganyikiwa na kuingia kwenye gari lake ambalo aliliondoa kwa kasi sana,” alisema Bw Matheka.

Muda mfupi baada ya kuondoka, mkewe Bi Ruth Mueni ambaye amezaa naye pacha alikuja kumuulizia kwa walinzi hao.

Kulingana na taarifa za majirani, awali muda wa saa sita usiku, Bi Mueni aliripitiwa kuonekana kughadhibika na kusikika akilalama kuhusu shida kati yake na mumewe.

“Mke huyo alikuwa hapa akinung’unika lakini haikudhihirika wazi shida ilikuwa ni nini. Alirudi nyumbani na baadaye ndio tukio hilo tukasikia lilijiri,” alisema mmoja wa majirani.

Kulingana na jamaa ya Mutinda, mkewe alidai kuwa mumewe alitoka nyumbani akisema kuwa amepokea simu kutoka kwa babake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa.

“Alikuwa anatoa maneno ambayo hayaeleweki akimwambia mkewe wakati alikuwa anatoka. Mkewe alijaribu kumzuilia lakini alionekana mwenye hasira zaidi na akashindwa,” alisema Bw Benedict Kieti, ambaye aliongea kwa niaba ya familia iliyokuwa imeandamana na mkewe marehemu, ambaye ndiye aliyetambua mwili huo.

Bw Mutinda alitumbukia majini muda wa saa kuni na dakika 20 alfajiri baada ya kupita eneo la kuegeshwa magari kwa kasi na kujitosa baharini.

Wakati huu hakukuwa na feri upande huo wa Likoni. Feri moja ambayo ilikuwa inahudumu ilikuwa upande wa Mombasa kisiwani.

“Wafanyakazi waliokuwa hapa walijaribu kuzuia gari hilo lakini wakashindwa kwani jamaa huyo alikuwa anaendesha gari hilo kwa kasi sana,” akasema mkurugenzi wa KFS, Bw Bakari Gowa.

Baada ya tukio hilo maafisa wa KFS walipiga simu kwa jeshi la wanamaji pamoja na mashirika mengine ya usaidizi kwa ajili ya kusaidia kwenye mkasa huo.

Ilipofika saa mbili asubuhi wanajeshi wa majini waliupata mwili wa Bw Mutinda na kuuweka kwenye boti lao kabla ya kuusafirisha upande wa kisiwani na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Jocham.

Kufikia saa tatu wanajeshi hao walilipata gari hilo na kuliopoa mwendo wa saa sita mchana kutoka kwenye kivuko hicho ambacho mnamo Septemba 29 , mwanamke na mwanawe pia walizama na kufa maji baada ya gari lao kutumbukia baharini.

Mwanamke huyo, Bi Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu, walitumbukia baharini baada ya gari lao kuanguka kutoka kwenye feri ya MV Harambee.

Ilichukua siku 13 kwa miili yao na gari lao kutolewa baharini.

Wakati huo huo, Jumamosi Gavana wa Kaunti ya Mombasa alitoa salamu zake za pole kwa familia ya wale waliopoteza mpendwa wao.

Bw Joho alihimiza watumizi wa feri kuwa makini wakati wanapotumia kivuko hicho ili kuepuka maafa mengine.