Michezo

Kigali Peace Marathon yavutia watimkaji 8,000

May 17th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI 8,000 watashiriki makala ya 14 ya Mbio za Amani za Kigali Marathon mnamo Mei 20, 2018.

Gazeti la New Times nchini Rwanda limesema Alhamisi kwamba mwenyeji Felicien Muhitira ameapa kumaliza utawala wa Kenya katika kitengo cha wanaume cha mbio za kilomita 21.

“Wakati wangu wa kutwaa taji ni mwaka huu. Sijawahi kuhisi niko tayari kabisa kwa mashindano haya kama mwaka huu. Nataka kupanda kwenye jukwaa hilo, nitazame bendera ya taifa langu ikipepea kabisa na wimbo wa taifa langu ukiimbwa.

Najua ni kibarua kigumu, hasa kutoka kwa Wakenya, lakini nimekuwa nikishindana nao nchini Italia na ninaamini naweza kuwalemea,” Muhitira alinukuliwa na gazeti hilo akisema.

Mwaka 2017, Bartile Kiptoo aliongoza Mkenya mwenzake Ezekiel Kimeli kunyakua nafasi mbili za kwanza katika mbio za kilomita 21 za wanaume, huku Mrwanda John Hakizimana akifunga tatu-bora.

Naye Salome Nyirarukundo alishindia Rwanda taji lake la kwanza kabisa katika mbio za kilomita 21 cha Kigali Peace Marathon katika kitengo cha wanawake. Alifuatwa na Mkenya Sheilla Chesang na Mrwanda Claudette Mukasakindi.