Kigame kuzindua muungano

Kigame kuzindua muungano

Na VICTOR RABALLA

MGOMBEAJI wa urais Reuben Kigame amesema kwamba ataungana na vyama vingine anapojiandaa kuzindua chama atakachotumia katika uchaguzi mkuu ujao ndani ya wiki tatu zijazo.

Akiwataka wapinzani wake kujiandaa kwa ushindani mkali, mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili alipuuza maoni kuwa uchaguzi wa urais ni kati ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto wa UDA.

“Siko peke yangu. Unaweza kuwa na hakika sitakuwa mgombeaji wa kujitegemea,” alisema Jumatatu alipozuru Kisumu.

Bw Kigame alisema atazindua muungano wa Eagles National Alliance katika wiki tatu zijazo ambapo atatangaza pia chama atakachotumia kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

“Iwapo baadhi ya watu walidhani kuna farasi wawili pekee, basi hawajui kuhesabu,” alisema.

Alisema atapatia Wakenya fursa ya kuchagua kati ya viongozi wa sasa na uongozi unaowapa ahadi ya kumaliza dhuluma nyingi ambazo zimedumu tangu uhuru.

“Viongozi wetu akiwemo aliye ofisini, Rais Kenyatta, wamekuwa wakitufungia nje. Wanatupuuza. Hii ndiyo sababu baadhi ya watu hufikiri kuna farasi wawili pekee,” alisema.

“Wakati umefika tujitokeze na kuwaonyesha kuwa tuko na tunaishi, tunajua kuhusu serikali na uongozi,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kutumia Sh7 bilioni kuhamisha makaburi na...

Mudavadi alivyosaliti wenzake OKA

T L