Kigogo Ibrahimovic sasa kuchezea AC Milan hadi atakapotimu umri wa miaka 40 baada ya kutia saini mkataba mpya

Kigogo Ibrahimovic sasa kuchezea AC Milan hadi atakapotimu umri wa miaka 40 baada ya kutia saini mkataba mpya

Na MASHIRIKA

FOWADI Zlatan Ibrahimovic,39, ametia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja na kikosi cha AC Milan kinachoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Kwa mujibu wa maelewano hayo, sogora huyo raia wa Uswidi sasa ataendelea kuwajibikia AC Milan hadi atakapotimu umri wa zaidi ya miaka 40.

Ibrahimovic aliingia katika sajili rasmi ya AC Milan kwa mara ya pili mnamo Disemba 2019.

Alirefusha kandarasi yake ya awali ya miezi sita kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi mnamo Agosti 2020 na sasa ameingia makubaliano mapya ya kuendelea kuvalia jezi za AC Milan wanaotiwa makali na kocha Stefano Pioli.

Kufikia sasa, Ibrahimovic amefungia waajiri wake jumla ya mabao 17 kutokana na mechi 25 za mapambano yote msimu huu na alipitisha jumla ya mabao 500 kitaaluma mnamo Februari 2021.

“Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba kuchezea AC Milan ni sawa na kuwa nyumbani kabisa. Nafurahia sana jinsi klabu hii inavyonifanya nihisi. Ningeteua kuchezea kikosi hiki kwa kipindi kizima kilichosalia cha maisha yangu iwapo ningeweza,” akasema nyota huyo.

Ibrahimovic alianza kusakata soka ya kitaaluma akivalia jezi za kikosi cha Malmo mnamo 1999 na tangu wakati huo, amewahi pia kuwa mchezaji wa Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, Paris St-Germain (PSG), Manchester United na Los Angeles Galaxy.

Uthabiti na utajiri wa kipaji chake katika ulingo wa soka umemfanya kuwa sogora wa pekee kuwahi kufunga mabao katika mechi zake za kwanza kwenye soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Italia (Serie A), Uhispania (La Liga), Ufaransa (Ligue 1) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Ibrahimovic ndiye mwanasoka wa pekee kuwahi kufunga mabao 50 ya Serie A akivalia jezi za klabu za AC Milan na Inter Milan.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Everton wakung’uta Arsenal 1-0 ugani Emirates na...

CHOCHEO: Usimpe mpenzi wako sababu ya kukushuku