Habari

Kihara awajibu wandani wa Ruto

March 13th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MKUU wa Sheria Paul Kihara Kariuki amekana madai ya baadhi ya wanasiasa kuwa vita dhidi ya ufisadi vinaendelezwa kwa malengo ya kisiasa akisema haja kuu ni kulinda mali ya umma.

Bw Kariuki, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Shirikishi inayoendesha juhudi hizo (MAT), pia alifafanua kuwa zoezi hilo halilengi watu kutoka jamii au eneo fulani la nchini bali watu wanaoshukiwa kuiba pesa za umme.

Mkuu wa Sheria Paul Kihara Kariuki (akiashiria) azungumza Machi 13, 2019. Picha/ Charles Wasonga

Wandani wa Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakidai kuwa vita hivyo vinalenga watu kutoka ngome yake ya Rift Valley kwa nia ya kuzima ndoto yake ya kuingia Ikulu ifikapo mwaka 2022.

“Hatuendeshi vita hivi kwa nia ya kutimiza malengo fulani ya kisiasa. Tunaendesha kazi hii kitaalamu bila kuendeleza masilahi ya kibinafsi. Lengo letu ni kuzuia wizi wa pesa za umma kwa kuhakikisha kuwa haki imetendeka bila mapendeleo,” Kihara akawaambia maseneta ambao ni wanachama wa Kamati kuhusu Sheria na Haki za Kibinadamu Jumatano katika majengo ya bunge, Nairobi.

Bw Kihara alikuwa ameandamana Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbaraki na Mkuu wa kitengo cha kutwaa mali zilizopatikana kwa njia ya ufisadi Muthoni Kimani.

Mkuu huyo wa sheria alisema kuwa kila asasi inayoshiriki katika juhudi za kupambana na ufisadi inaendesha majukumu yake kwa njia huru bila kuingiliwa kwa njia yoyote.

“Wahesimamiwa maseneta, kila mmoja yetu hapa anafanya kazi yake kwa njia huru, kwa utaalamu na kulingana na Katiba. Hamna anayeingiliwa wala kushawishiwa kwa njia yoyote kama ambavyo baadhi yenu wanasiasa mwasema huko nje,” Bw Kihara amesema.

DPP afichua

Akiunga mkono kauli hiyo Bw Haji alifichua kuwa uchunguzi unaoendelezwa kuhusu malipo ya Sh21 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer utaendelezwa katika miradi mingine aina hiyo inayotekelezwa katika maeneo mengine ya nchi.

“Baada ya kukamilisha uchunguzi wa sakata ya Arror na Kimwarer tunaendeleza uchunguzi wetu katika maeneo ya Kati, Mashariki na Pwani ambako mabwawa mengine yanajengwa,” akasema Bw Haji.

Alikuwa akijibu swali la mwenyekiti wa kamati hiyo Samson Cherargei aliyetaka kujua ikiwa wanachama wa MAT wanaingiliwa kisiasa “inavyodaiwa na baadhi ya Wakenya.”

Wabunge kutoka Rift Valley wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi wamemshambulia DCI Bw George Kinoti kuhusiana na uchunguzi wa  malipo tata ya Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Walisema uchunguzi huo unalenga kumhujumu Dkt Ruto kwa kulenga watu wanaotoka jamii yake.

“DCI ametekwa kisiasa. Haendeshi shughuli zake kwa njia huru kwani ni wazi kuwa anatumiwa kuzima ndoto ya Naibu Rais William Ruto kuwania uchaguzi urais 2022 kwa kuwaondoa afisini watu kutoka Rift Valley wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini,” Bw Sudi alisema wiki jana.

Bw Murkomen alitoa kauli sawa na hiyo akihusisha uchunguzi huo na njama ya kuhamisha miradi hiyo kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet hadi maeneo mengine.