Habari za Kitaifa

Kiini cha masaibu ya Wa Iria

April 23rd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, mke wake Bi Jane Waigwe na aliyekuwa Kamishna wa Murang’a Bw Patrick Mukuria, ni miongoni mwa watu saba ambao Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amependekeza washtakiwe kwa madai ya kufisadi Sh140 milioni.

Bw Mukuria alikuwa akihudumia serikali ya Wa Iria (2012-2022) akiwa Katibu wa Kaunti na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 akateuliwa kuwa kamishna.

Mwingine aliye katika lawama ya kashfa hiyo ni mwanasiasa wa Kaunti ya Embu Bi Jane Mbuthia ambaye aliwania wadhifa wa mbunge wa Mbeere Kusini katika uchaguzi wa 2022 lakini akaangukia pua.

Wengine ni wandani wa Bw Wa Iria ambao ni David Maina Kiama, David Maina Njeri, Solomon Mutura Kimani na Peter Muturi Karanja.

Kwa sasa, Bw Wa Iria, mkewe na Bw Mutura–ambaye ni nduguye mke wa Wa Iria–wamepata idhini ya mahakama ya kuzuia kushtakiwa kwao huku wengine wakiendelea kusakwa baada ya kukosa kufika mahakamani kama walivyoagizwa.

Katika taarifa ya DPP ya Aprili 13, 2024, wote hao katika miaka ya kifedha ya 2014/15 na 2015/16 walitapeli Kaunti ya Murang’a jumla ya Sh140 milioni kupitia kashfa ya matangazo ya kibiashara.

Pesa hizo zilipitishiwa kampuni moja ya utangazaji inayomilikiwa na mwanasiasa mashuhuri mstaafu wa eneo la Mlima Kenya. Inadaiwa kampuni nyingine za utangazaji zilizokuwa zikipewa kandarasi za utangazaji hazikulipwa kwa mujibu wa mikataba iliyotiwa saini bali pesa zao zililiwa na washukiwa hao.

Ofisi ya DPP ilisema kwamba uamuzi wa kuwashtaki ulitokana na uchunguzi wa kina ambao umekuwa ukiendeshwa na Tume Huru ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Washukiwa hao wamesemwa kwamba walitumia kampuni ya uhamasisho ya Top Image Media Consultants Limited na nyingine ya Value View Limited kufisadi hela hizo.

Katika hali hiyo, wanane hao watashtakiwa kwa makosa sita kwa kila mmoja, yakiwa ni kushirikiana kutekeleza ufisadi kinyume na ibara ya 47A(3) ikiambatanishwa na 48 ya sheria za kudhibiti ufisadi na makosa ya kiuchumi.

Aidha, wameorodheshwa kuwajibikia kosa la matumizi mabaya ya ofisi, kujinufaisha na mali ya umma kinyume na sheria, kutekeleza biashara kwa njia inayokinzana na nafasi zao za ofisi, kujihifadhia mali iliyo na shaka ya uadilifu na utakatishaji wa pesa zionekane kama ni halali huku wakijua ni mapato haramu.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba washukiwa wote wa ufisadi wanafaa kubebeshwa msalaba wao na wakipatikana kwa makosa mahakamani, kwanza warejeshe pesa walizopora.

“Ni baada ya kurejesha pesa hizo ambapo wanafaa kufungwa gerezani pasipo huruma,” akasema.

Mnamo Ijumaa wiki jana, wabunge Mary wa Maua (Maragua) na Betty Maina (Murang’a) walilalamika kwamba kuna baadhi ya washukiwa wa ufisadi ambao walikuwa wakitembea huru licha ya kupendekezewa mashtaka.

Walisema mafisadi walikuwa wanachomea serikali picha na kuifanya iishiwe na umaarufu huku harakati za kuitetea zikigeuka kuwa kibarua kigumu.

Walihofia kwamba ni hali ambayo inaweza ikageuka kuwa mtego wa wanasiasa wakisaka kura 2027 hivyo basi kuwa suala la dharura wote waliohusishwa na ufisadi wawajibishwe mkondo wa kisheria.

[email protected]