Makala

Kiini cha Museveni, Owino kukabana koo

Na BENSON MATHEKA August 31st, 2024 1 min read

KATIKA kile kinachoweza kufananishwa na malumbano ya ndovu na sungura, Mbunge wa Embakasi Mashariki  hakuchelea kuzungumzia madai ya Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni aliyemlaumu kwa kuingilia siasa za nchi yake.

Akionekana kumshtaki kwa viongozi wa Kenya na hasa kinara wa chama Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, Bw Museveni alisema hapendezwi na shughuli za Bw Owino katika nchi yake alizoashiria zinalenga kuhujumu serikali yake ya chama cha National Resistance Movement (NRM).

Bw Babu Owino, rafiki wa karibu wa kiongozi wa upinzani wa Uganda, Robert Kyagulanyi Bobi Wine,  alimjibu Museveni baada ya rais huyo kumshutumu kwa kuingilia siasa za nchi hiyo jirani

Bw Owino alipuuza matamshi ya Rais Museveni akisisitiza kuwa kama kiongozi, ataunga  mkono demokrasia.

Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda

“Kuna baadhi ya watu katika kundi la Raila ambao sidhani wanajua wanachofanya. Mimi ni huwa ninapata huduma za kijasusi kwa hivyo huwa naona ripoti za idara ya ujasusi.

“Kuna mhusika anaitwa Babu. Huwa namuona Babu akishughulika na makundi yanayopinga NRM. Sijawahi kumshtaki lakini sasa namshtaki.”

Babu Owino, Mbunge Embakasi Mashariki

“Namshukuru Rais Museveni kwa kuunga mkono azma ya Baba( Raila Odinga) ya Uenyekiti wa AUC. Hata hivyo, kuwa kiongozi kijana nchini Kenya, baada ya kukulia katika umaskini, najua maana ya kukosa,” alisema Owino.

“Ukiniambia kuwa umelala njaa, najua maana ya kukosa chakula kwa sababu nimepitia hayo. Ukiniambia unakosa karo, nitakuelewa kwa maana najua kukosa karo ya shule ni nini. Kwa sababu ya changamoto tunazokabiliana nazo nchini Kenya na Afrika, sisi kama viongozi tunafaa kutafuta suluhu.”

“Kama Babu Owino, ninasimamia kidemokrasia ambapo mtoto nchini Kenya atapata dawa zinazofaa, na elimu na  kazi. Vile vile, mtoto nchini Uganda anafaa kupokea matibabu sawa na ya mtoto nchini Kenya.”