Kiini cha Uhuru kuteleza nyumbani

Kiini cha Uhuru kuteleza nyumbani

Na BENSON MATHEKA

KUSHINDWA kwa chama cha Jubilee katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja, Kaunti ya Kiambu na Wadi ya Rurii iliyo Nyandarua, kumezua maswali kuhusu alikoteleza Rais Uhuru Kenyatta katika ngome yake ya Mlima Kenya, kiasi chao kumuabisha nyumbani.

Eneobunge la Juja linapakana na Gatundu Kusini ambako ni nyumbani kwa Rais Kenyatta, na kushindwa kwa Jubilee kumetoa picha ya uasi dhidi ya kiongozi wa nchi eneo hilo.

Ingawa chama hicho kilipoteza katika chaguzi ndogo tatu zilizofanyika Jumanne wiki hii, kushindwa katika eneo la Juja kumetajwa kuwa ishara ya jinsi umaarufu wa Rais Kenyatta ulivyoshuka hata katika kaunti anakotoka.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, matokeo ya chaguzi za Juja na Rurii ni ujumbe kwa rais kwamba umaarufu aliokuwa nao eneo la Mlima Kenya umeshuka kwa kiwango kikubwa.

Wataalamu wa siasa wanasema Rais Kenyatta amechangia kushuka kwa umaarufu wake kwa kutotimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017, hasa kufufua uchumi kwa kuweka mazingara bora ya biashara, kilimo na kuwapa vijana kazi.

Pia suala la kutegemea ushauri wa watu ambao hawakuchaguliwa kuliko wa walioshinda viti vya kisiasa limetajwa kuchangia kudidimia kwa umaarufu wa rais.

Mwanasiasa mmoja wa Jubilee asema mtindo wa utawala wa Rais Kenyatta ndio umesababisha pengo kati yake na wapigakura kupanuka zaidi.

“Serikali imeweka sera ambazo zimevuruga maisha ya Wakenya wa kawaida. Hii imefanya wafanyabiashara na wakulima wadogo kutumbukia katika mateso makubwa kiuchumi. Kuna kilio kikubwa kutoka kwa wakulima wa kahawa, chai na wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.

“Makosa ya Rais Kenyatta ilikuwa ni kuondoa msingi ambao mtangulizi wake Mwai Kibaki aliweka kuinua uchumi, na badala yake akaweka sera zilizopokonya raia haki zao za kupata riziki,” aeleza mbunge wa Jubilee aliyeomba tusitaje jina lake.

Alipokutana na wakazi wa Mlima Kenya katika Ikulu ya Sagana mapema mwaka huu, waakilishi wa wakazi walilalama kwamba sera za serikali yake zimefanya biashara katika masoko ya Nyamakima, Gikomba, Kamukunji na Kirinyaga jijini Nairobi kufungwa.

Pia walilalamikia kuhusu kufurushwa kwa wakazi katika mitaa ya Ruai na Kariobangi wakati wa janga la corona, na pia wakamlaumu kwa kutowatembelea mashinani kusikiliza shida zao.

Jambo lingine ambalo wataalamu wa siasa wanasema limechangia kudorora kwa umaarufu wa Rais Kenyatta ni kukosa kutimiza ahadi zake za kisiasa.

Wakati wa kampeni za 2017, Rais Kenyatta aliahidi kwamba atamuunga mkono naibu wake William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, ahadi ambayo amepuuza na badala yake akaelekeza juhudi zake katika handisheki yake na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Inaonekana Mlima Kenya walichukulia kauli ya Uhuru ya kumuunga mkono Ruto kwa uzito sana. Aliahidi miaka kumi ya Uhuru na miaka kumi ya Ruto. Wengi bado wanashikilia hapo,” asema mchanganuzi wa siasa Barrack Muluka.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo wanahisi wana deni la Dkt Ruto kwa jinsi alivyosimama na Rais Kenyatta mnamo 2013 na 2017.

“Uhuru alitwambia akiondoka atamuachia Ruto. Kisha akasema Raila ni mbaya. Hapa basi twajiuliza, ilikuwa vipi mzuri akawa mbaya na mbaya akawa mzuri?” akasema mkazi wa Juja, Irungu Karanu.

“Uhuru hatupendi tena. Alikuwa akituita ‘jeshi’ ili tumpige kura. Siku hizi akija eneo la Kati anatutusi tu kwa hasira. Polisi wake nao wanatuhangaisha tu. Tulimalizana naye kitambo!” Akaeleza Jimmy, ambaye ni manamba mjini Ruiru.

Alipoapishwa kwa muhula wa pili, Rais Kenyatta aliahidi kuimarisha maisha ya Wakenya kwa kuzingatia Ajenda Nne Kuu ambazo ni afya bora kwa wote, kuimarisha kilimo, viwanda na makazi. Hata hivyo, kufikia sasa ahadi hizo zingali ndoto.

Kulingana na aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini, Kabando wa Kabando, Rais Kenyatta aliteleza kwa kuwapuuza wakazi na kutotimiza ahadi zake kwao.

Lakini maafisa wa serikalini na viongozi wanaomuunga rais mkono wanasema angali na ushawishi mkubwa eneo la Mlima Kenya.

Wandani wake pia wanahoji kuwa Rais Kenyatta ameanzisha miradi mingi hasa ya barabara ambazo zimerahisisha uchukuzi wa bidhaa na usafirishaji wa watu. Wakazi wengi wa Mlima Kenya waliohojiwa walieleza kufurahishwa na miradi hii, lakini wakasisitiza kuwa hilo ni jukumu la serikali kwao kama walipaji ushuru.

You can share this post!

Spurs wavizia huduma za wakufunzi Hansi Flick na Ralf...

Wazee waingilia zogo la Matiang’i, Ongwae