Kiini cha vyama vya Pwani kutovuma kitaifa

Kiini cha vyama vya Pwani kutovuma kitaifa

NA PHILIP MUYANGA

Licha ya ukanda wa Pwani kuwa na takriban vyama vitano, hakuna chama ambacho kinaweza kujivunia kuwa kimekita mizizi na kuwa na ushawishi mkubwa hadi nje ya Pwani.

Swala hili limeibua hisia tofauti tofauti huku watu wengi wakijiuliza ni kwa sababu gani vyama ambavyo chimbuko lake ni Pwani vinaonekana haviendelei na kuwa ‘vinafufuka’ tu wakati wa uchaguzi mkuu ukikaribia.

Kuanzishwa hivi majuzi kwa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) ambacho kinara wake ni Gavana wa Kilifi Amason Jeffa Kingi pia kumeongeza msisimko na tashwishi pia iwapo kitaendelea au kufifia baada ya msimu huu wa siasa.

Hata hivyo, katika mkutano mmoja hivi majuzi Bw Kingi alisema kuwa PAA ni chanzo cha safari ya eneo la Pwani kuelekea ikulu mwaka wa 2027.

“Chama cha PAA kitawasilisha wagombeaji viti kwa kila nyadhifa na mwaka wa 2027 ni ikulu, faida ya PAA haiji kwangu,inakuja kwa wananchi,”alisema Bw Kingi.

Kando na PAA vyama vingine ambavyo asili yake ni Pwani ni pamoja na Shirikisho Party of Kenya, Umoja Summit Party, Kadu Asili na Republican Congress Party.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa kutoimarika kwa vyama vya kisiasa vya eneo la Pwani kunasababishwa na ukosefu wa fedha na wafadhili ambao huhakikisha utenda kazi wa chama unatekelezwa.

Mshauri wa maswala ya kisiasa Bw Bozo Jenje anasema kuwa wengi ambao wanaanzisha vyama vya kisiasa eneo la Pwani hawana uwezo mkubwa wa kifedha ikilinganishwa na waanzilishi wa vyama vingine maeneo tofauti nchni.

“Pia swala lingine ni kuwa wale ambao wanadhamini vyama kifedha pia huona pia hawawezi kuhatarisha fedha zao kama chama hakionyeshi kuwa na thamani yoyote,” alisema Bw Jenje.

Eneo muhimu kisiasa

Bw Jenje pia alisema kuwa serikali pia imechangia pakubwa kwa kutoendelea kwa vyama vya Pwani kwa kuwa inajua ni eneo muhimu kisiasa ambapo inaweza kupata kura wakati wa siasa.

Aliongeza kusema kuwa serikali inauwezo wa kudhoofisha vyama hivyo asi – lia na kwamba vikiwa hafifu ni rahisi kuwaendesha viongozi wa vyama hivyo wapendavyo.

Bi Maimuna Mwidau ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa anaunga mkono hoja ya kuwa ukosefu wa fedha unaathiri kuendelea kwa vyama vya Pwani.

Alisema kuwa kuanzisha chama na kuweka miundo misingi kama vile kuanzisha maafisi kila eneo bunge na pia kuitisha mikutano ya wajumbe pia kunahitaji pesa nyingi.

“Hakuna chama ambacho hakina pesa,kila chama lazima kiwe na wajumbe ishirini katika kila eneo bunge,hapo awali chama cha KANU pekee ndicho kiliweza,huwa ni jambo ghali mno,”alisema Bi Mwidau.

Aliongeza kusema kuwa wengine ambao wamesajili vyama hawana uwezo wa kuvigharamikia ikitiliwa maanani kuwa kusajili vyama kunahitaji takriban Sh500,000 ili kupata cheti cha muda na pesa zingine kama hizo kupata cheti rasmi.

“Ukiona vyama vimeshindikana basi jua ni fedha hakuna mpaka wakati ule mwenye uwezo wa kifedha akiingia akifadhili, lakini pia akitoka huwa kinasambaratika,”alisema Bi Mwidau.

Katika mahojiano ya hapo awali na Taifa Leo, mchanganuzi wa siasa Bw Yusuf Aboubakar alisema kuwa wapiga kura eneo la Pwani wameshindwa kuvipigia debe vyama vya asili ya Pwani na kuwapigia kura watu wao.

“Nawalaumu wapiga kura,wanawasukuma viongozi wao kwa vyama vingine,”alisema Bw Aboubakar akiongeza kuwa katika kura za mwaka wa 2007,chama cha shirikisho kiliungana na kile cha PNU lakini wapiga kura hawakukipigia kura.

Hoja hiyo inaonekana kuungwa mkono na Bw Jenje anayesema kuwa wananchi wa Pwani pia hawatambui viongozi wao na wanapendelea wanasiasa kutoka nje ya ukanda wa Pwani.

“Swala hilo ni kama ule msemo wa kuwa shujaa hatambuliki kwao,” alisema Bw Jenje.

Miungano ya vyama vya Pwani kuwa kitu kimoja na kuwasilisha wagombeaji kura katika uchaguzi mkuu ni swala ambalo limekuwa likitangazwa kila kikicha lakini bado wananchi hawajajua bayana iwapo vyama hivyo vitaungana.

Kwa sasa waakaazi wengi wa Pwani wanasubiri kuona iwapo vyama vyenye asilia ya Pwani vitasikika hadi nje ya Pwani kwa kuwasiliasha wagombeaji viti katika maeneno yote nchini na uwepo wao katika siasa za nchini umetambulika.

 

  • Tags

You can share this post!

Upweke wajaa Ford Kenya Olago naye aking’oka

Kivumbi kikali kushuhudiwa robo fainali za Koth Biro

T L