Makala

TEKNOLOJIA: Kijana ajizatiti kutengeneza mtambo wa kuwasha na kuzima taa, ving'ora

August 27th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

IKIWA ndoto ya James Nyakera, 26, ya kuwekeza na kufaulu katika uvumbuzi katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) itatimia, basi ni kwa muda tu atangoja kabla ya kufahamika kama bwanyenye.

Mwenyewe anasema anahitaji muda wa mwezi mmoja.

“Huu ndio muda nitahitaji kuunda na kuzindua rasmi mradi wa kutengeneza mashine ya kuuza bidhaa za majimaji bila kuajiri mtu wa mauzo,” anasema.

Aidha, anasema huu ndio muda atahitaji kuunda mtambo ulio salama wa kuwasha na kuzima taa na ving’ora hata ukiwa kwa umbali gani na nyumba au biashara yako.

Isitoshe, ikiwa ni katika shule na makanisa; hata katika vyumba vya uchapishaji habari za magazetini au kokote kule ambako hutumika kengele kama kikumbusho cha muda kuyoyoma, anasema kuwa anaweza akamwondolea binadamu kazi hiyo ya kupiga kengele.

“Kile nitafanya ni kuunda mtambo maalum wa kiteknolojia, niweke ratiba ya kengele kulia na ninakili sauti ya ukumbusho wa jukumu linalohitajika na iwe sasa ni rasmi kengele itakuwa ikilia kwa muda unaohitajika,” anasema Nyakera.

Anasema kuwa mtambo huu wa kengele umethibitika katika utafiti wake kuwa na uwezo wa kutofuata mfumo wa saa katika kiwango cha ongeza (+) sekunde moja kwa miaka 100. Ina maana kuwa, ukiwekeza katika teknolojia hii yake ya kupiga kengele kisayansi, basi kabla ya ipate hitilafu ya kukukanganya kwa kulia sekunde moja baada ya muda unaofaa, utakuwa umeishi na mtambo wenyewe kwa hadi miaka 100 ukijaliwa maisha marefu.

Lakini cha kuduwaza ni ile teknolojia ya taa na king’ora kutoka bongo la mtafiti huyu na mvumbuzi na mfumbuzi ambaye alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya (MKU) kilichoko mjini Thika mwaka wa 2017.

“Nitakuundia laini spesheli katika simu yako ya mkononi na kisha niunganishe na namba za siri katika milango, madirisha au lango kuu katika nyumba au jengo la biashara yako. Kukitokea uvamizi, hata uwe kwa umbali gani, laini hiyo katika simu yako itakupasha habari katika skrini ya simu yako. Kisha laini hiyo itagutusha zile nambari spesheli zizindue awamu ya kupiga king’ora na pia kuwasha na kuzima kwa awamu taa za usalama na hivyo basi kuwatimua wavamizi hao,” anasema.

Anaongeza kwamba teknolojia hii pia itaachilia miale ya stima kutoka kwa king’ora kujiunganisha na maeneo ambayo yameunganishwa na king’ora na ni ya vyuma, ili kusababisha shoki ya stima hivyo basi kuweka maisha ya wavamizi hao katika hatari kuu.

“Na la mwisho, niko na uwezo wa kuzindua msisismko mkuu sokoni kupitia mitambo ya uuzaji na ambapo utaondolewa gharama ya kulipia nyumba ya kazi au ya kuajiri watu wa kuhudumu katika duka lako,” anasema kijana huyu.

Hii ni kupitia mitambo hiyo ya mauzo na ambayo ikipakiwa na bidhaa ambazo ungetaka kuuza, iwe ni maziwa, mafuta taa, petroli, dizeli na bidhaa zinginezo za majimaji na zisizo na povu, mtambo huu utakupa kipimo cha pesa ambazo utauweka.

“Teknolojia hii inatumia sayansi ya kuunda programu za hela na vipimo ndani ya mtambo huo na ambapo ukishauzindua, wewe kazi yako inakuwa tu kuweka bidhaa katika hifadhi ya mtambo huo na wateja wakiingia na kuweka senti, bila kusita mtambo huu unafanya hesabu na kugawa kipimo cha kutosheleza senti ulizoweka,” anafafanua.

James Nyakera aonyesha jinsi mtambo wake wa kuuza bidhaa kiteknolojia hufanya kazi. Picha/ Mwangi Muiruri

Na sio eti mambo haya yote anayafanyia katika karakana kubwa ya uvumbuzi. La hasha!

“Utashangaa kujua kwamba natumia chumba changu cha malazi ambacho kina upana wa futi 12 kwa 10 katika kijiji cha Kiamagoko, kaunti ndogo ya Mathioya kama maabara na karakana ya uvumbuzi na ufumbuzi huu. Kwa sasa, mfadhili wangu mkuu ni mamangu mzazi na ndugu zangu na ambapo wamenisaidia kuwa nikiagiza vijisehemu vya teknolojia hizi kutoka China,” anasema.

Anasema kuwa pia hupata kazi za kibarua katika taasisi kadhaa kuwawekea na kuwatunzia idara zao za kiteknolojia lakini anakolenga ni kuwa na kiwanda chake ambacho kitakuwa kikiunda mitambo hiyo na kuuza kwa wateja.

Anasema kuwa amechukua mkondo huu wa kimawazo baada ya kusaka kazi kwa kampuni 108 na ambapo ni kampuni 21 pekee zilizojibu barua zake za kuomba kazi zikimwambia hazikuwa na nafasi ya kujazwa.

Anasema kuwa shida kuu ya taifa hili ni kwamba, kuna wafumbuzi na wavumbuzi ambao wanaweza wakaufaa uchumi wa taifa na pia wajijenge bila kusumbua serikali “lakini hakuna mikakati ya kuwapata na kuwalea hadi wafanikishe ndoto yao.”

Anasema serikali ikitaka kuinua kozi za kiufundi, sera zake ziziangazie tu kozi za ushonaji nguo, useremala na usonara.

Angependa kuona serikali ikiinua sekta za utafiti na uvumbuzi wa kisayansi.

Anahisi uvumbuzi ni sekta moja na ambayo haifai kujumuishwa pamoja na wanaosaka kozi kwa kuwa hakuna uwiano kamwe kati ya sekta hizo mbili.

Aidha, anasema serikali kuu na pia zile za Kaunti hazina ufahamu kamili wa sekta ya Kisayansi na ndiyo sababu hata vile vipawa tele ambavyo huonekana katika maonyesho ya uvumbuzi kwa wanafunzi wa shule za sekondari, vyuo vikuu na taasisi zinginezo, huishia kuoza mitaani na vijijini kwa kuwa hakuna sera maalum ya kuvilea hadi viwafaidi walio navyo.

“Imekuwa ni kama kaulimbiu hapa nchini ni kwamba hata uwe na werevu wa kiwango kipi hapa nchini, uwe na wazo gani la kibiashara au uwezo mwingine wowote wa kufaa nchi na watu wake, ole ukikosa pesa na huna wa kukushika mkono kama nilivyo kwa sasa, huenda ujipate katika jaa la taka miongoni mwa waliokosa kufanikiwa maishani. Ingawa hivyo, sichoki kumwomba Mungu wangu aninusuru kutoka hali hiyo,” anasema.