Kimataifa

Kijana ashtua kuua watu watano wa familia

January 29th, 2019 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAUME wa miaka 21 kutoka Amerika anazuiliwa na polisi baada ya kumuua mpenzi wake, baba na kaka yake, kisha akaenda nyumbani kwao (mshukiwa) na kuwaua wazazi wake.

Picha za kuogofya zikionyesha damu iliyotapakaa chumbani, huku mashimo ya risasi yakipenyeza chumba hicho ambapo Bi Elizabeth na Keith Theriot, wote waliokuwa na miaka 50 waliuawa Jumamosi.

Kijana huyo, Dakota Theriot, sasa amefunguliwa mashtaka matano ya mauaji, matumizi mabaya ya bunduki, uvamizi na wizi wa gari.

Theriot anadaiwa kumuua mpenzi wake Summer Ernest, 20, babake Billy Erneest, 43 na kakake Tanner Ernest, 17, kabla ya kwenda kuwaua wazazi wake.

Alikamatwa alipokuwa nyumbani kwa nyanyake eneo la Warsaw, Virginia Jumapili asubuhi, na polisi waliofika kwa bunduki.

Polisi walisema kuwa alikuwa ametoroka zaidi ya kilomita 2,000.

Wakili mmoja alisema kuwa nyanyake mshukiwa alihama Jumamosi hiyo na kulala hotelini, kwani alihofia kuwa mjukuu wake angefika huko nyumbani kwake.

Ajuza huyo alirejea akiwa na maafisa wa polisi nyumbani kwake asubuhi ya Jumapili, wakati kijana huyo alichomoza akiwa na bunduki, akasema afisa wa polisi.

“Polisi walimwamrisha kuweka bunduki chini kisha akatii na akakamatwa na kupelekwa seli,” akasema.

Polisi walisema kuwa alionekana kuwa mchovu na ambaye hakuwa amepata usingizi na kuwa baadaye alirekodi habari.

Anatarajiwa kufikishwa kortini kufunguliwa mashtaka, japo kiini cha kutekeleza mauaji hayo hakijajulikana. Hata hivyo, polisi wanaamini kuwa ulikuwa mzozo wa kimapenzi baina yake na mpenzi wake.

Polisi walisema kuwa Theriot alikuwa akiishi pamoja na mpenzi wake na wazazi wa mpenzi wake kwa wiki kadha kabla ya kutekeleza kitendo hicho na kuwa hawakuwa na mapenzi ya muda mrefu.

Polisi waliendelea kusema kuwa alianza kwa kumuua mpenzi wake, baba, kisha kaka.

Hata hivyo, hakuwagusa watoto wa miaka saba na mmoja ambao walikuwa eneo hilo la tukio. Ni mtoto huyo wa miaka saba aliyembeba mwenzake wa mwaka mmoja hadi kwa jirani na kuomba msaada.

Baada ya kuwaua aliiba lori na kuelekea nyumbani kwao, takriban kilomita 50 ambapo nako aliwaua wazazi wake. Polisi walipofika nyumbani kwao, bado wazazi wake walikuwa hai.

“Ni Keith Theriot aliyetufahamisha kuwa ni mwanaye aliyefanya kitendo hicho,” akasema mkuu wa polisi.

Juhudi za kuokoa maisha ya wawili hao zilifeli kwani waliaga dunia hospitalini kutokana na majeraha.