Habari Mseto

Kijana ashtua wanakijiji kujinyofoa sehemu nyeti

August 4th, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

WAKAZI wa kijiji cha Shikustse, Wadi ya Kabras Magharibi, Kaunti ya Kakamega bado wapo kwenye hali ya mshangao baada ya kijana kunyofoa nyeti yake katika hali isiyoeleweka.

Wazazi wa William Muchesia, 20, Jumamosi mchana walimpata akitokwa na damu kwenye sehemu nyeti na baada ya kuchunguza kwa makini waligundua sehemu nyeti ilikuwa imekatwa.

Cha kusikitisha ni kwamba sehemu ambayo ilikuwa imekatwa haikuweza kupatikana na kuifanya iwe vigumu kwa madaktari kumfanyia upasuaji wa kumrekebisha katika hospitali ya Kaunti ndogo ya Malava.

Hata hivyo, haijabainika Bw Muchesia alitumia kifaa kipi kukata uume wake kwani pia hapakupatikana kisu wala wembe mahali pa mkasa.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kakamega Kaskazini, Bw Peter Mwanzo uchunguzi umeanzishwa ili kubainisha kilichotokea.

“Familia haikuripoti tukio hili kwenye kituo cha polisi lakini tumewatuma maafisa wetu kwenye kijiji hicho kubaini kilichotokea,” akasema Bw Mwanzo.

Naibu Chifu wa Lokesheni ya Shikutse, Bw Alfred Malaha alisema kwamba amezungumza na wazazi wa kijana huyo na wamemweleza kwamba hayupo kwenye hali ya hatari hospitalini ingawa anakumbwa na maumivu makali.

“Bado hatujui ni nini kingemfanya kujisababishia madhara aina hiyo,” akasema.