Habari MsetoSiasa

‘Kijana fupi nono round’ akataa kazi ya Ruto

June 16th, 2019 1 min read

Na OSCAR KAKAI

MWANASIASA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Dennis Ruto Kapchok, almaarufu Mulmulwas, amekataa kazi aliyoahidiwa na Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Ijumaa, Dkt Ruto alimtaka Mulmulwas kukoma mara moja kukosoa miradi ya maendeleo ya serikali ya kaunti na kuahidi kumtafutia kazi.

Ruto alijitolea kumpa kazi kufuatia shutuma kali kutoka kwa Gavana wa Pokot Magharibi Profesa John Lonyangapuo aliyemtaja Kapchok kama “mtu mvivu asiye na kazi ya kufanya.”

Gavana huyo alinukuliwa kwenye video moja maarufu mitandaoni akilalamika kuhusu “kijana fupi nono round, asiye na kazi” anayemhangaisha.

“Nilimsikia gavana wenu akilalamika kuhusu jamaa mmoja Mulmulwas ambaye nasikia anatoka hapa kwenu. Gavana alisema Mulmulwas hana kazi. Nataka kusema hivi, nitampa kazi Mulmulwas. Lakini lazima aache kukosoa serikali (ya kaunti) katika juhudi zake za kuleta maendeleo hapa. Lazima akome,” Bw Ruto aliambia umati uliomshangilia.

Aliongeza: “Kazi yake sio kuingilia ujenzi wa mfumo wa kuondoa maji taka katika kaunti. Hiyo si kazi; huo ni upuzi. Iwapo anataka atafute ajira, na niko tayari kumsaidia kupata kazi hiyo. Kukosoa serikali isiwe kazi ya Mulmulwas. Anafaa kuwa chonjo.”

Hata hivyo, Naibu Rais hakusema ni kazi aina gani ama wadhifa upi aliotaka kumpa Mulmulwas.

Akizungumza na Taifa Jumapili, Kapchok alisema hataki kazi hiyo aliyoahidiwa na Ruto.

“Sikutuma barua ya kuomba nafasi ya kazi. Nashukuru kwa ofa hiyo, lakini sidhani nitaikubali. Vita vyangu dhidi ya masuala ya kimsingi kama ufisadi, uvunjaji sheria bila kuhofia adhabu, na matumizi mabaya ya rasilimali za kaunti haviwezi kudidimizwa.

Mradi wa kujenga mabomba ya kuondoa maji taka uko na wahusika wengi wanaolenga tu maslahi yao,” akasema na kusisitiza kuwa lengo lake ni kushinikiza kuwepo kwa mabadiliko uongozini yatakayonufaisha wakazi wa kaunti.