Habari

Kijana maskini aliyekataliwa na mchumba aandaliwa harusi ya mwaka

August 27th, 2018 2 min read

Na COLLINS OMULO

MWANAMUME aliyekuwa amekataliwa na mchumba wake wa awali kwa sababu ya umasikini, hatimaye wikendi alifanya harusi ya kukata na shoka.

William Mwangi alipata bahati hiyo baada ya kutoa ushuhuda kanisani kuhusu jinsi alivyokataliwa na mwanamke ambaye moyo wake ulikuwa umemchagua awe wake wa maisha. Alisimulia masaibu yake kanisani, na ikawa bahati kwamba Seneta wa Nairobi Bw Johnson Sakaja alikuwepo.

Baada ya Mwangi kumaliza kusimulia masaibu yake, na kwamba sasa alikuwa amepata mchumba mwengine, Bw Sakaja alimpa Sh50,000 alizomtaka azitumie kupangia harusi yake. Seneta huyo alimtaka Bw Mwangi atumie fedha hizo na kutojali kuhusu masuala ya usafiri.

Na kweli siku ya Jumamosi, Bw Sakaja akatimiza ahadi yake kwa kutoa gari lake la kifahari kumbeba Bw Mwangi na mchumba wake mpya, Bi Marion Kinya.

Si kwamba aliwapatia gari liwabebe tu, bali Bw Dakaja aliwaendesha mwenyewe hadi katika kanisa la Jesus Winner Ministry, Roysambu, Kaunti ya Nairobi ambako wawili hao walifunga pingu za maisha.

“Nina furaha kubwa kuwa sehemu ya wanaosherehekea harusi kati ya William na Kinya. Hadithi kuhusu mapenzi yao ilitugusa sana, kwani William alikuwa ameachwa na mchumbaye wa awali kwa kuwa maskini. Kinya aliamua kutozingatia hayo na kuapa kumpenda. Wamebarikiwa,” akasema Bw Sakaja.

Seneta huyo kijana alisema aliguswa sana na jinsi ambavyo umasikini na kukosa uwezo wa kifedha umekuwa ukichangia vijana wengi kukosa wachumba.

“Mungu ndiye hutupa utajiri. Hatupaswi kumbagua yeyote kwa msingi wa kile alicho nacho ama ambacho hana. Kisa hiki cha Bw Mwangi kimenifanya kutafakari kuhusu mustakbali wa jamii yesu, hasa katika mahusiano ya kweli,” akasema.

Bw Sakaja aliahidi kuwa atakuwa akimpa Bw Mwangi Sh15,000 kila mwezi mbali na mshahara wa Sh15,000 ayakaokuwa akipokea iwapo kanisa litatekeleza ahadi yake kuwa litamwajiri na kumlipa kiasi hicho.

Akizungumza baada ya kufunga pingu za maisha, Bw Mwangi alitoa wito kwa wasichana kutoangalia utajiri wa mwanamume katika masuala ya ndoa, ila kuzingatia uadilifu wake.

Bi Kinya naye aliahidi kumpenda mumewe, kwa msingi kuwa nguzo kuu ya ndoa si utajiri mbali upendo.