Kijana mjasiriamali atangaza nia ya kufuata nyayo za Ruto

Kijana mjasiriamali atangaza nia ya kufuata nyayo za Ruto

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

JUMBA lililokuwa la sinema ya Moons iliyokuwa maarufu Mombasa lilikosa kutumika kwa miaka kadhaa baada ya wapenzi wa filamu aina mbalimbali kushuhudia filamu wazipendazo kwenye simu zao kupitia kwa mitandao ya kijamii kama vile YouTube.

Alikuwa kijana Nabil Khamis Salim aliyezaliwa Juni 18, 1991, aliyebuni wazo la kuanza kulikodisha jumba hilo kama mbinu ya kudumisha kumbukumbu za umuhimu wake.

Nabil alifikiria mpango maalum wa kulitumia jumba hilo baada ya kulikodisha kwa kipindi cha miaka mitano na akaanza kulifanyia ukarabati kuanzia mwaka wa 2019 na kulikamilisha mwaka wa 2020, ndipo likaanza kutumika kwa harusi na tamasha mbalimbali.

“Nilifanikiwa kulifanyia jumba hili la Moons ukarabati na kuwa ukumbi wa kisasa ambao umekuwa ukitumika kwa sherehe za harusi, mikutano na tamasha nyingine za kijamii,” akasema Nabil aliyetufahamisha kuwa alisitisha matumizi ya jumba hilo wakati wa mkurupuko wa Covid-19.

Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jumba hilo lililoko eneo la Tononoka ambako ni katikati ya mji wa Mombasa na mahali ambako kunasifika kuwa kuna usalama wa kutosha, Nabil alilipa jumba hilo jina la Noble Ballroom.

Kwa kipindi cha miaka michache, jumba hilo la Noble Ballroom linaendelea kuwa maarufu huku likitumika zaidi kwa sherehe za harusi.

“Niliona jumba hilo limekaa bila ya kutumiak kwa kipindi kirefu ndipo nikawafuata wamiliki wake na kukubaliana nao kulikodisha na kulitumia kama ukumbi wa kufanyiwa harusi pamoja na tafrija nyingine, kutegemea wale wanaotaka kulikodisha ili kulitumia kwa siku moja ama zaidi ya kipindi hicho,” akasema.

Mbali na kuwa na biashara hiyo, Nabil alisema alivutiwa mno na maono ya Rais William Ruto alipotangaza nia yake ya kuwania kiti cha urais kutokana na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha muhula wake wa pili wa wadhifa huo.

“Kutokana na kuvutiwa na sera za Ruto, niliamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha mwakilishi wa wadi ya Majengo-Mwembe Tayari nikiwa na nia kubwa ya kuleta mageuzi na nilifanikiwa kupata tikiti ya chama cha UDA kwenye uchaguzi wa mwaka 2022,” akasema.

Alisema alifanya kampeni za kukata na shoka hasa kwa madhumuni ya kumzolea Ruto kura nyingi katika sehemu hiyo aliyogombea ambayo iko eneo-bunge la Mvita, kura ambazo zilimkaribia zile alizopata mgombea wa chama cha ODM, Raila Odinga.

“Nilifurahi kuona Rais Ruto akishinda kwenye vituo sita kati ya vituo 11 vilvyokuwa kwenye wadi hiyo ya Majengo-Mwembe Tayari,” akasema Nabil huku akibainisha kuwa Bw Raila alipata kura 6,201 naye Ruto akamfuata kwa karibu kwa kuzoa kura 5,856, tofauti ikiwa ndogo sana.

Nabil alikirembesha kwa gharama yake binafsi kibanda cha chama cha UDA katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo ya Mombasa ambayo yalifunguliwa rasmi na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua majuzi.

Naibu Rais Rigathi Gachagua (kulia) akiongea na viongozi wa UDA kwenye kibanda cha chama hicho wakati wa Maonyesho ya Kilimo ya Mombasa. PICHA | HISANI

Mbali na kurembesha kibanda hicho, kwa niaba ya chama chake cha UDA, Nabil alitayarisha hafla ya Iftar wakati wa mwezi mtukufu wa Ramdhan ambapo viongozi kadhaa wa chama hicho walihudhuria katika ukumbi wa Aga Khan Sports Club (Jubilee).

Nabil anasema mnamo Julai 19, 2022 katika ukumbi wake wa Noble Ballroom, aliandaa shughuli ya uzinduzi wa kitabu cha Babior Newton cha ‘The rise of a Hustler’ ambapo viongozi kadhaa wa UDA wakiwemo Mbunge wa Afrika Mashariki aliyewahi kuwa seneta wa Mombasa, Hassan Omar Sarai, mwenyekiti wa KMA Hamisi Mwaguya na Fatma Barayan walihudhuria.

Nabil ni mtoto wa aliyekuwa diwani na mwanasiasa shupavu katika Baraza la Manispaa ya Mombasa, marehemu Khamis Salim almaarufu Nyundo na ana nia ya kuvaa viatu vya babake vya siasa alivyoviacha.

“Ninaamini Rais Ruto ataiongoza nchi yetu katika ufanisi mkubwa na ninawaomba wananchi wamuunge mkono kwani ndipo taifa letu litaweza kupiga hatua ya maendeleo,” akasema Nabil.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Agizo la Gachagua halitatatua athari za...

TALANTA: Pacha waimbaji

T L