Kijana mwenye vipaji vingi, anayevitumia kuwafaa wenzake

Kijana mwenye vipaji vingi, anayevitumia kuwafaa wenzake

Na PETER CHANGTOEK

ABUBAKAR Ali, ni kijana mwenye vipaji vingi, na huwafaa wenzake; wanawake kwa wanaume.

Yeye hurekodi video za michezo ya kuigiza, huhariri video hizo na kuhudumu katika duka lake ambalo hulitumia kutoa huduma za mitandao. “Mimi hutoa huduma za mitandao na kuuza juisi na kuoka keki pia,” asema kijana huyo, mwenye umri wa miaka 23.

Kijana huyo, ambaye husakini na kuhudumu katika eneo la Pumwani, Nairobi, alijitosa katika shughuli za kutoa huduma za intaneti mwaka 2017. Anafichua kuwa, aliutumia mtaji wa takriban Sh50,000 kuanzisha biashara hiyo. Aliinunua kompyuta kwa Sh15,000 na vifaa vinginevyo vya kazi.

Kwa wakati huu, ana tarakilishi mbili, ambapo huitumia moja kuzihariri video za michezo ya kuigiza. “Nilianzisha kazi hii miaka miwili baada ya kuhitimisha masomo yangu ya Kidato cha Nne,” aongeza Abubakar, ambaye ni kifunguamimba katika aila ya watoto watatu.

Yeye pia hutoa filamu na ni mchoraji hodari wa kuchora michoro mbalimbali. Anasema kuwa amekuwa akijaribu mno kutoa video lakini hakuwa amefanikiwa hadi mwezi Aprili mwaka huu. “Nilianza 2015, lakini sikufanikiwa.

Abubakar akihariri mojawapo ya video zake…Picha/PETER CHANGTOEK

Nilikuwa nikijaribu nikifeli, lakini sikupoteza matumaini, kwa sababu nilikuwa na uraibu. Kwa hivyo, kila wakati nilipofeli, nilikuwa nikizinduka na kujaribu tena, hadi Aprili 16, 2021, ambapo ndiyo siku yangu ya kwanza kutoa video yangu kwanza,” aeleza Abubakar, ambaye kwa wakati huu, amerekodi michezo ya kuigiza zaidi ya 12.

Anasema kuwa, amekuwa akijaribu sana kupunguza gharama ya kurekodi video, na amekuwa akisaidiwa pakubwa na marafiki. “Sipati chochote kwa video. Ndoto yangu ni ya kurekodi video na kuandika michezo ya kuigiza. Nitakapopata pesa, nitafungua studio ya filamu, na si filamu fupi, bali ni filamu ndefu,” asema.

Anaongeza kuwa, waigizaji wanaoigiza kwenye filamu zake ni wa kujitolea, na wamekuwa wakishirikiana pamoja, ili kuyafikia malengo yao. Anadokeza kuwa, ana waigizaji takriban kumi na watano. “Hutumia kamera ya rafiki yangu, natumai nitainunua yangu siku moja,” asema Abubakar.

Anaeleza kwamba, huchukua muda wa siku mbili kurekodi na kuhariri video zake, endapo waigizaji hawana shughuli nyingi za binafsi, na wakati ambapo wana shughuli nyinginezo, yeye huchukua siku tatu au nne kufanya hivyo.

Abubakar anafichua kuwa, waigizaji hao hutoka katika eneo moja, na hivyo basi kuwapata kwa ajili ya shughuli hiyo ni rahisi. Huwachagua wale wenye vipaji vya kuigiza. Michezo yake ya kuigiza na video hupatikana kwa YouTube, Tiktok, Facebook, Instagram na Uhive, na hujulikana kama Tynka Stories.

Anawashauri vijana kutokufa moyo kwa yale wafanyayo. “Kama umejaribu na umefeli, usikate tamaa kwa ndoto zako, ni lazima ufeli ili ufanikiwe. Kufeli ni funzo ambalo hatuwezi kuepuka, utafeli ili ujifunze kutokana na makosa, ili wakati utakapojaribu tena, utaepuka makossa na kujua njia bora ya kutimiza ndoto zako,” ashauri kijana huyo.

Anasema kuwa, anapania kuimarisha shughuli zake na kuwa na kampuni ya filamu, ili awape nafasi walio na vipawa wavitumie vizuri

You can share this post!

Ufisadi, ulafi vinasababisha majumba kuporomoka

Ufugaji wa nguruwe unavyompa mkulima kipato Mwatate

F M