Michezo

Kijasho Manangoi akivizia Cheruiyot katika mbio za Diamond League

May 29th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Diamond League mnamo 2018 katika mbio za mita 1,500, Timothy Cheruiyot amesema kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuhifadhi ufalme wa riadha hizo.

Duru ya tatu ya msururu wa mbio hizo za 2019 itaandaliwa hapo kesho jijini Stockholm, Uswidi.

Atakuwa akijibwaga ulingoni baada ya kuambulia nafasi ya pili katika kivumbi cha Diamond League kilichoandaliwa jijini Doha, Qatar mapema Mei.

Cheruiyot aliyetawala duru saba za IAAF Diamond League mwaka 2018, alizidiwa maarifa na Mkenya mwenzake, Elijah Manangoi katika makala ya kwanza yam waka huu jijini Doha.

Wawili hao wanatarajiwa kuendeleza ushindani mkali kwa mara nyingine hii leo jijini Stockholm.

Ingawa hivyo, wawili hao wanatazamiwa kukabiliana na upinzani mkali zaidi kutoka kwa ndugu watatu wa Norway – Henrik Ingebrigtsen, Filip Ingebrigtsen na Jakob Ingebrigtsen ambaye ni mshindi wa zamani wa mbio za mita 1,500 na mita 5,000.

Wengine wanaotarajiwa kutamba zaidi katika kinyang’anyiro hicho n bingwa dunia katika mbio za mita 1,500 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, George Manangoi na wanariadha wawili mahiri kutoka Ethiopia – Samuel Tefere na Aman Wote. Kulingana na Cheruiyot, ushindi hapo kesho utampa hamasa zaidi ya kujiandalia kwa Riadha za Dunia zitakazofanyika jijini Doha mnamo Oktoba 2019.

Kwa upande wa wanawake, malkia wa dunia katika mbio za mita 5,000, Hellen Obiri anatarajiwa kuendeleza ubabe wake katika Diamond League.

Kufikia sasa, Obiri hajazidiwa maarifa na yeyote mwaka huu. Aliibuka mshindi wa mbio za mita 3,000 katika duru ya kwanza jijini Doha mapema mwezi huu baada ya kusajili muda wa dakika 8:25.60. Isitoshe, alitamalaki pia mbio za kilomita 10 za Great Manchester, Uingereza.

Wapinzani wake wakuu watakuwa Wakenya Margaret Chelimo na Agnes Tirop ambaye anajivunia kushinda medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani. Wengine ni Caroline Chepkoech na Lilian Kasait. Mbio hizo zitawashirikisha pia Yasemin Can wa Uturuki na Fantu Worku kutoka Ethiopia.

Kukosekana kwa Caster Semenya wa Afrika Kusini, Francine Niyonsaba kutoka Burundi na Mkenya Margaret Nyairera katika mbio za mita 800, kutasaza vita vikali mikononi mwa Ajee Wilson wa Amerika na Nelly Jepkosgei.

Nyairera ambaye anashikilia medali ya shaba katika Olimpiki, alipigwa marufuku pamoja na wenzake kushiriki mbio hizo za mita 800 kutokana na kanuni mpya za IAAF zinazolenga kudhibiti viwango vya homoni za testosterone miongoni mwa wanariadha wa kike.