HabariSiasa

Kikao cha Raila na Jumwa chazua mihemko mitandaoni

October 1st, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

MBUNGE wa Malindi Aisha Jumwa Jumanne aliwaacha Wakenya na maswali mengi baada ya kukutana na kinara wa upinzani Raila Odinga huku taarifa zikisambaa mitandaoni kwamba amegura kambi ya Naibu wa Rais Dkt William Ruto na kurejea katika chama cha ODM.

Bi Jumwa alionekana kwenye picha ya pamoja na Bw Odinga na kundi la wabunge wakipiga gumzo na kucheka baada ya mkutano wa wabunge wa ODM katika County Hall, mkabala na majengo ya Bunge.

Ingawa alipuuzilia mbali habari zilizodai kwamba alikuwa amehudhuria mkutano huo na “kurudi nyumbani,” Wakenya kwenye mitandao ya kijamii walitoa maoni mseto kuhusu tukio hilo la bungeni.

Kulikuwa na majibizano makali kati ya wafuasi wa ODM na wale wa Dkt Ruto. Kwa upande mmoja, wale wa ODM walisema marejeo ya Bi Jumwa yaliashiria jinsi Naibu Rais anazidi kutengwa na wandani wake.

Lakini kwa upande mwingine, wafuasi wa Dkt Ruto walipuuzilia mbali ripoti za marejeo ya mbunge huyo na kusema ni ishara ya jinsi ODM inavyotamani arudi zizini.

Bi Jumwa ameibuka kuwa mpinzani mkuu wa ODM kwenye kinyang’anyiro cha udiwani katika uchaguzi mdogo uliopangiwa kufanyika Wadi ya Ganda, Kaunti ya Kilifi. Mbunge huyo ambaye pia ni mwanakamati wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) alisema Bw Odinga ndiye alikuwa amepitia afisini mwake kumsalimia akiwa na wabunge wengine wa ODM.

“Alinitembelea kwenye afisi zangu za PSC baada ya kuhudhuria mkutano wa wabunge wa ODM ambao sikuhudhuria kamwe,” akasema kwenye taarifa.

Mbunge wa Makadara George Aladwa alithibitisha kwamba Bw Odinga alimtembelea Bi Jumwa afisini mwake baada ya mkutano huo lakini hapakuwa na majadiliano yoyote kuhusu kurejea kwake chamani.