Habari

Kikao cha seneti chaahirishwa malumbano yakiwa yamechacha

July 29th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine maseneta walikosa kukubaliana kuhusu mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti baada ya wao kulumbana kuhusu suala hili hadi usiku Jumanne.

Naibu Spika Profesa Margaret Kamar alilazimika kuahirisha kikao hicho hadi Jumanne Agosti 4, 2020, kwa kuzingatia sheria ya kafyu.

Kamar alisema ingekuwa makosa kwa maseneta kuendelea na mjadala kuhusu suala hilo ilhali Rais Uhuru Kenyatta aliamuru polisi kutowasaza wale wote watakaokiuka sheria za kafyu “hata kama wao ni waheshimiwa.”

Wakati huo, maseneta walikuwa wakijadili marekebisho kwa ripoti ya Kamati ya Fedha, kuhusu mfumo inayopendekeza kuwa kaunti zenye idadi kubwa ya watu zipate mgao mkubwa wa fedha, pendekezo ambalo lilipingwa vikali na maseneta kutoka kaunti ambazo zitapoteza.

Awali, maseneta kutoka kaunti ambazo zingepoteza walipinga pendekezo la kiranja wa wengi Irungu Kang’ata kwamba utekelezaji wa mfumo huo ucheleweshwe kwa miaka miwili, na uanze kutekelezwa katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Jumla ya maseneta 25 walipiga kura ya kupinga pendekezo hilo la Bw Kang’ata na maseneta 22 waliaunga mkono.

Waliopinga pendekezo hilo la Bw Kang’ata, ambalo lilionekana kupendelewa na Rais Uhuru Kenyatta, ni maseneta kutoka kaunti za Pwani, Kaskazini Mashariki, Kaskazini mwa Kenya, Ukambani na kaunti za Kisii na Nyamira katika eneo la Nyanza.

Kaunti za maeneo haya zitapoteza fedha ikiwa mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Fedha na ule wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) utatekelezwa kwa misingi Sh316.5 bilioni zilizotengewa kaunti zote 47 katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.

Katika mapendekezo yake Bw Sakaja anataka mfumo wa ugavi wa fedha uliotumiwa mwaka jana, udumishwa, ili kaunti zisipoteze fedha zozote.

Seneta huyo wa Nairobi anataka mfumo huo mpya uanze kutekelezwa wakati ambapo mgao wa fedha kwa serikali za kaunti utaongezwa kuzidi Sh316.5 bilioni, kauli ambayo inaonekana kuungwa mkono na maseneta kutoka kaunti ambazo zingepoteza fedha chini ya mfumo mpya.

Bw Sakaja alisema kuwa dhana kuwa baadhi ya kaunti zitapata pesa nyingi ikilinganishwa na mwaka uliopita inafaa kuondolewa kwani ndiyo chimbuko la mvutano kuhusu suala hilo.

“Ni heri kaunti yangu ya Nairobi ipoteze Sh100 milioni zaidi ambazo ingepata endapo mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Fedha inayoongozwa na mwenzangu Charles Kabiru, badala ya kaunti zingine kupoteza fedha,” akaeleza.

Maseneta walionekana kugawanyika pakubwa kuhusu suala hilo, kiasi kwamba wakati mmoja kiongozi wa wachache James Orengo na mwenzake wa Bungoma Moses Wetang’ula walipendekeza mjadala uahirishwe. Hata hivyo, maseneta wengi walipinga wazo hilo.

Wawili hao walitaka maseneta watenge muda zaidi ya kukubaliana kuhusu masuala kadhaa yanayohusu mfumo huo mpya kabla ya kurejea bungeni na kupitisha mfumo huo.

Bw Wetang’ula alisema hakuna hasara yoyote kuhusiana na suala hilo kwani Katiba inasema wazi kuwa ikiwa maelewano hayataafikiwa kuhusu mfumo mpya, mfumo uliopo ndio utaendelea kutumika katika ugavi wa fedha baina ya kaunti mwaka huu.

Lakini Bw Kang’ata, kiranja wa wachache Mutula Kilonzo Junior na maseneta wengine, walipinga pendekezo hilo la Orengo na Wetang’ula, kwamba kikao kiahirishwe.

Kang’ata alisema bunge hilo limeahirisha mjadala kuhusu suala hilo kwa mara tano, na “hatuwezi kufanya kosa hilo tena.”

“Kama viongozi tunafaa kutekeleza wajibu wetu wa kuamua kuhusu suala hilo leo (Jumanne) na wala sio wakati mwingine. Kiongozi asiyeweza kufanya maamuzi mazito wakati ufaao hafa kwa niaba ya wananchi hafai kuendelea kuitwa kiongozi,” akasema Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a.

Alishikilia kuwa marekebisho ambayo alipendekeza, kwamba utekelezaji wa mfumo mpya ucheleweshwe kwa miaka miwili, pamoja na yale ya Bw Sakaja, ni mazuri kwa sababu yakizingatiwa hamna kaunti itakayopoteza fedha.

“Nilisikia kilio kutoka ndugu zetu kutoka kaunti zilizo nyuma kimaendeleo. Ndiposa napendekeza mfumo uanze kutekelezwa mwaka wa kifedha wa 2022/2023. Kwa hivyo, mwaka huu na mwaka ujao hakuna kaunti zitakazopoteza,” akasisitiza Bw Kang’ata.

Bw Orengo pia aliunga mkono pendekezo la Bw Kang’ata, akisema kaunti hazifai kupoteza fedha zozote.

“Chini ya pendekezo hili la Bw Kang’ata hakuna anayepoteza. Hakuna atakayepoteza mwaka ujao, na mwaka utakaofuata,” Senata huyo wa Siaya akakariri.

Alipoanzisha mjadala kuhusu ripoti ya kamati ya fedha Bw Kibiru ambaye ni Seneta wa Kirinyaga, alisema kamati yake ilikusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau wote.

“Kwa hivyo, mjadala usiwe kuhusu kiasi cha fedha ambazo kaunti zitapokea bali ikiwa mfumo huu unakubalika miongoni mwa wadau,” akasema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta wa Migori Ochilo Ayacko, ambaye aliwataka maseneta kutizama mfumo huo sio kwa misingi ya kiasi cha fedha ambazo kila kaunti itapokea.