Bambika

Kiki ya mcheshi KK Mwenyewe ya kula pilipili yaishia kukimbizwa hospitalini

April 7th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MCHEKESHAJI Zachariah Kariuki almaarufu KK Mwenyewe ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kutafuta tiba katika hospitali kutokana na kula pilipili kilo moja.

Mchekeshaji huyo aliambia Taifa Leo Dijitali alikula pilipili hizo ili kutimiza ahadi aliyokuwa ametoa kwa mashabiki wa mpira. Mnamo Alhamisi, aliapa kula kilo nzima ya pilipili ikiwa timu anayoshabikia, Manchester United ingeshindwa na Chelsea.

“Sijui nianzie wapi? Niliambia mashabiki nitakula pilipili. Mwanzo nilikuwa na uhakika kuwa timu yangu ingepta ushindi na hivyo sitakula,” alisimulia KK Mwenyewe.

KK Mwenyewe, 24, alipatwa na huzuni na kulazimika kutimiza ahadi yake kwa mashabiki wake. ‘Mashetani Wekundu’ walichapwa 4-3 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge Alhamisi usiku.

“Sijua kilichotokea. Nilianza kula pilipili hizo, muda ulivyosonga niliwashwa zaidi. Sikuweza kumaliza,” alikiri KK Mwenyewe.

Alisema kuwa alichukua jukumu la kujipeleka hospitali akiwa kwa kuhofia kwamba kibaya kingetokea labda azidiwe na maumivu usiku.

“Nilifika hospitali kumwona daktari baada ya kula pilipili zile. Daktari alinifahamisha nisiwe na shaka kila kitu kitakuwa sawa,” alisema KK Mwenyewe.

Kabla ya mahojiano na Taifa Leo, mcheshi huyo alikuwa amepakia video kwenye mitandao ya kijamii ili kuonyesha kiwango cha pilipili alichopania kula. Pia, alieleza wazi kuwa hakufahamu matokeo ya hatua yake hiyo.

Katika video hiyo, mchekeshaji huyo alionekana akihangaika kumeza pilipili na hakuweza hata kumaliza vijiko viwili vya tunda hilo kali.

Baada ya kushindwa kuendelea, alionekana akinywa soda pengine kuondoa ukali mdomoni mwake. Kisha, kupiga mswaki, na kula sukari nyingi ili kuondoa ladha kali.

Kufuatia matokeo hayo, aliyoyataja kuwa mabaya, KK, ameweka wazi kuwa hatawahi kutoa ahadi asiyoweza kutimiza. Pia, alitangaza kwamba hatashabikia tena mpira wa miguu.