Makala

KIKOLEZO: Bado kiza kinene!

October 4th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

MIAKA 10 iliyopita rapa mkali kutoka Bongo, Mwana FA, aliachia bonge la fataki ‘Unaoa Lini’.

Inawezekana alikuwa akikabiliwa na presha ya kuoa kutoka kwa ama jamii na jamaa au mashabiki.

azi hiyo ikawa gumzo sana hadi huku kwetu Kenya kiasi cha kuibua promosheni ya kampuni ya Nation Media Group, ‘Utahama Lini’.

Miezi michache baadaye, Mwana FA akaja tena na ‘Bado Nipo Nipo’ yakiwa ni majibu ya lini anaoa. Ulikuwa ni ubunifu tu wa kisanii ila kiuhalisia, ilimchukua miaka kadha kuja kuoa. Ndoa yake aliifunga Juni 2016 na mpenzi wake wa siku nyingi.

Katika nyakati tunazoishi sasa, vipo vitu vitatu ambavyo watu wanaonekana kuogopa sijui kulikoni?

Kifo, magonjwa yasiyo na tiba na sasa ndoa.

Woga huu upo kwa kila mja mpaka pia wasanii wamo. Wafuatao ni baadhi tu ya wasanii ambao wamedumu kwenye mahusiano ya muda mrefu ila wanapotupiwa swali wanaoa lini, wanatoa vijisababu kama vyote.

VIVIAN NA SAM WEST

Tayari wanaishi kama mume na mke ila bado haijashuhudiwa sherehe rasmi ya wawili hawa wakilishana yamini.

Msanii Vivian amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na meneja wake Sam kwa miaka mitatu sasa.

Sam alimchumbia rasmi Vivian Aprili 2017. Mwaka 2018 waliandaa sherehe ndogo ambapo Sam alitoa mahari kwa kina Vivian.

Mwaka huu 2019 wameahidi kufanya harusi yao ingawaje bado hawajatangaza tarehe. Siku nazo zinayoyoma mwaka ukiwa umesalia na miezi miwili tu ufikie tamati. Wamekaa kimya. Au ndio wamesogeza mbele?

TANASHA NA DIAMOND PLATNUMZ

Mwishoni mwa mwaka 2018 staa wa Bongo Flava, Diamond Platnumz alitangaza kuwa kwenye uhusiano na mrembo Mkenya, Tanasha Donna, mtangazaji wa redioni pale NRG.

Miezi miwili baada ya kuanzisha uhusiano wao, Diamond alitangaza kuwa atamwoa kufikia Februari 14, 2019.

Diamond Platnumz na Tanasha Donna. Picha/ Maktaba

Siku zilipokaribia, akaibuka na kuahirisha harusi hiyo pasi na kutoa tarehe mpya.

Sababu za Diamond ni kwamba anapania kufanya harusi kubwa na mastaa kibao washikaji zake kama Rick Ross, Omarion, wanapaswa kuhudhuria. Na kutokana na sababu hawataweza kufika Februari 14, ndipo akaamua kuisogeza mbele.

Tayari Tanasha kanasa ujauzito wake na kajifungua majuzi. Huo ndio uhakika uliopo kwa sasa, lakini suala la ndoa ni la kusubiri tu.

BEN POL NA ANERLISA MUIGAI

Penzi lao lilianza na mkutano wa kibiashara ila sasa ni wapenzi wakubwa. Wanaishi maisha ya kutamanisha na kila mmoja anaamini ni kutokana na uwezo wa kifedha wa Anerlisa.

Wanatumia muda wao mwingi angani zaidi ya ardhini, wakizunguka dunia. Mara wapo Dubai, mara wamekwenda visiwa vya ushelisheli, mara wapi kule. We acha tu!

Tayari Ben keshatambulishwa ukweni na hata sherehe ndogo kufanyika. Pia Anerlisa kafikishwa Tanzania kuwacheki wazazi wa mwana. Kilichobakia ni ndoa japo majuzi Ben kadai kwamba walishaoana zamani kwenye hafla ya kimya kimya. Ila hakuna anayewaamini. Kwa namna wanavyopenda kuposti picha zao wakifurahia maisha, haiwezekani wakazificha za shughuli kubwa kama harusi. Ila kama zipo acha tusuburi.

AIKA NA NAHREEL

Wapenzi hawa ndio wanaounda kundi la Navy Kenzo ambalo lilivuma na wimbo Kamatia Chini na sasa wanafanya vizuri na kibao Katika.

Wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa zaidi ya miaka minane toka walipokutana India walikokuwa wamekwenda kusoma.

Kwa sasa wamejaliwa mtoto na ingawaje wameishi kama mke na mume kwa miaka yote hiyo, hawajahi kuhalalisha uhusiano wao.

Hivi majuzi Nahreel alitangaza kuwa mipango ya ndoa ipo jikoni ikiwa ni baada yao kununua mjengo wa mamilioni ya pesa wanakoishi pamoja. Tayari Aika kanasa ujauzito wa pili. Sasa sijui ndoa itasubiri au itafanyika akiwa kwenye hali hiyo.

KING KAKA NA NANA OWITI

Rapa King Kaka na kichuna Nana wamekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa miaka minane sasa.

Wamedhihirisha waziwazi kwamba nia yao ni kuzeeka pamoja hadi milele. Uhusiano wao umewajalia watoto wawili, mabinti warembo. Hata hivyo mpaka sasa hawajafunga ndoa rasmi licha ya kuwa tayari wanaishi kama mtu na mke.

Novemba mwaka jana kwenye uzinduzi wa albamu yake mpya Eastlando Royality, ndipo King Kaka alimposa rasmi kwa kumvisha pete ya uchumba. Harusi kama ipo, itabidi watu wasubiri.

DK KWENYE BEAT NA SHANICE WANGECHI

Mwanamuziki huyu wa injili amekuwa kwenye uhusiano wa miaka saba na mpenzi wake Shanice.

Alimchumbia miaka kadhaa imepita hata tumeshasahau. Akifanyiwa mahojiano na gazeti moja 2017, DK alifichua kwamba walikuwa kwenye mipango ya kufunga ndoa Disemba mwaka huo.

Siku zimepita na mpaka leo hamna taarifa zozote za harusi yao.