KIKOLEZO: Edi Gathegi yule msee!

KIKOLEZO: Edi Gathegi yule msee!

NA SINDA MATIKO

ITAKUWA sio sura geni kwako haswa ikiwa wewe mpenzi wa filamu. Amehusika kwenye filamu kibao kubwa kubwa kwenye kiwanda cha Hollywood.

Kama hukumwona kwenye Twilight Saga, basi utakuwa ulimcheki kwenye The Harder They Fall, au Series ya Blacklist ama pengine Into The Bad Lands.

Kivyovyote vile mwanakwetu Edi Mue Gathegi hakwepeki. Licha ya kuwa ni raia wa Marekani, Edi ni Mkenya kwanza.

Alizaliwa na kulelewa huku kabla ya familia yake kuhamia Marekani ambako ameishia kujitengenezea jina kwenye kiwanda cha Hollywood kutokana na ushupavu wa kazi zake.

“Haikuwa rahisi kuwa na mwingiliano na wenzangu hasa nilipokuwa tineja. Hasa shuleni ilikuwa changamoto kubwa ukizingatia kuwa wanafunzi wengine wote walikuwa tofauti na mimi,” aliwahi kunukuliwa.

Uigizaji ulikumta kwa bahati mbaya. Edi aliyesomea Chuo Kikuu cha California alikuwa mchezaji mzuri tu wa mpira wa vikapu hadi siku moja alipopata jeraha baya la goti lililozima ndoto yake ya kuwa Kevin Durant au Lebron James ukipenda.

Ni hapo alipoamua kupata mafunzo ya kuigiza katika Chuo Kikuu cha New York kitengo cha uigizaji, alikosomea pia Lupita Nyong’o.

“Kusema kweli niliupenda sana mchezo wa vikapu na ndio maana nilipoumia goti vibaya nikiwa shuleni, ishu hiyo ilinisumbua sana. Nilipatwa na sonona. Kujitosa kwenye uigizaji ilikuwa tu mbinu ya kujaribu kuyapunguza mawazo ndipo nikajiunga na chuo na baada ya hapo nikaanza kuitiwa usaili mbalimbali kuonyesha kipaji changu,” kafunguka.

Baada ya kufuzu 2005, Edi mwenye umri wa miaka 43 alianza rasmi uigizaji wake kwenye kumbi za sinema kabla ya kuishia kwenye filamu baada ya kiwango chake kuonekana na wadau wa Hollywood.

Filamu yake ya kwanza ilikuwa Crank iliyotoka 2006 na miaka 15 baadaye, amehusishwa kwenye zaidi ya filamu 50 huku nyingi zikiishia kufanya vizuri. Kutokana na mapato ya filamu, utajiri wake kwa sasa unakadiriwa kuwa zaidi ya dola 3 bilioni (Sh300 milioni).

DAIMA MKENYA

Kagongana mabega na mastaa wa nguvu pale Hollywood toka mwanzo jambo analosema lilichangia taaluma yake kukua. Hili anaamini pia linawezekana Kenya ilimradi kuna miundo misingi bora.

“Kenya kuna vipaji vya kutosha vya uigizaji vinavyohitaji malezi bora tu kuwa mastaa. Mwangalie Lupita Nyong’o kwa mfano na mambo anayoyafanya, hii inatuchochea sisi Wakenya tuliopo Hollywood kujituma zaidi. Natamani kuja kufanya kazi naye siku moja,” kasema.

Ingawaje bado Lupita na Edi hawajafanikiwa kukaa kwenye seti moja, jambo moja wanalojivunia wote ni Ukenya wao.

“Ndio tumeishi Marekani toka utotoni na maisha yetu yapo huku ila Ukenya ni utamaduni ambao huwezi kuupoteza hata itokee nini. Bado upo ndani yangu. Najielewa kabisa, naijua vyema historia yangu, chimbuko langu, uasisi wangu, hilo hawezi kunipokonya mtu,” kasisitiza Edi aliyelelewa Eastlands kabla ya familia yake kuhamia majuu ili wazazi wake waendeleze masomo yao.

Ni ishu hii ndio imemfanya mara kwa mara yeye kuzuru Kenya kwa ajili ya likizo na kwa safari chache alizokuwa huku, amekuwa akijitahidi kufanya mahojiano.

Mara ya mwisho yeye kuzuru nyumbani ilikuwa 2018.

“Niligundua Wakenya kumbe wananifuatilia sana pia, wanakubali ninachokifanya na ndio sababu kila nikija nyumbani kwa ajili ya likizo huwa napenda kufanya mahojiano ili niwape uelewa kuhusu mishemishe zangu kule,” asema.

Pamoja na nyota yake kung’aa, anakiri kuwa kule Hollywood maisha sio rahisi hata kwa mastaa.

“Haijalishi wewe ni nani, unatokea wapi au vitu kama hivyo, kubwa pale kiwanda kinachotambua ni bidii pekee. Sasa kama ukiamua kuwa na sifa hiyo, basi utafika sehemu. Na kwenye mafanikio, itategemea bahati yako, fursa na Mungu wako,” katupia.

HAJASHINDA OSCARS

Na licha ya wasifu mzito pengine hata kuliko wake Lupita, hajawahi kushinda tuzo za staa kama vile Oscars au Emmys’. Lakini pamoja na yote hilo halijawahi kumsumbua hata kidogo.“Unajua tuzo sio kama pipi za kutolewa kiholela. Ninachojua mimi ni kwamba kupata tuzo tu hata uteuzi, sio jambo rahisi kwa sababu huwa kuna siasa nyingi. Kwangu mimi huwa ninazingatia zaidi kazi yangu na kuwaridhisha watu sababu ukiwaridhisha, hiyo ni sawa na kushinda Emmy. Huwa nasemaje, kama hujatosha mboga kwa kutoshinda Emmy, utatoshaje kwa kushinda Emmy?” kasisitiza.Wakati hayupo bize, utamkuta akizunguka dunia na mke wake dansa Mromania Adriana Marinescu. Staa huyo twiga mwenye futi 6’1 alifunga ndoa na Adriana 2018. Lakini pia Edi anapenda kusoma na kucheki filamu.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Bibiye atapatapa kujipandisha dau!

WANDERI KAMAU: Tujifunze kutoka kwa Sri-Lanka na Tunisia...

T L