Makala

KIKOLEZO: EMB kama 'ndrama', kunani?

February 7th, 2020 3 min read

Na THOMAS MATIKO

KABLA ya kifo cha mzee Moi, maceleb wawili waliokuwa wakitrendi hapa nchini walikuwa ni Tanasha Donna na Kevin Bahati.

Tanasha alitrendi kutokana na uzinduzi wake wa kitoto wa EP yake alioufanya Jumamosi iliyopita.

Kabla yake, msanii wa injili Bahati alikuwa akitrendi baada ya kumtupa seli aliyekuwa msanii wa lebo yake ya EMB Records, Peter Blessings.

Kikweli toka Bahati alipoanzisha lebo hii ya EMB kwa kile mimi ninachokiona kuwa alifanya kukurupuka na kumwigiza Diamond Platnumz wakati huo, hakuna kizuri kilichotoka hapo.

Tangu Bahati alipoanzisha EMB Records, amekuwa akiandamwa na kashfa moja baada ya nyingine.

EMB aliianzisha miaka minne iliyopita, ikiwa ni takriban miaka miwili baada ya Diamond kuanzisha Wasafi iliyoishia kushika kasi na kuwa lebo kubwa.

Yale mafaniko ya Wasafi naamini yalimzengua Bahati kuamini kwamba na yeye angeishia kupata mafanikio hayo. Lakini ndio mpaka leo, imekuwa ni misukosuko tu. Drama moja baada ya nyingine.

Mr Seed, David Wonder, Rebecca Soki, Weezdom wajitoa

Weezdom ndiye aliyekuwa msanii wa kwanza kusainiwa EMB lakini mambo hayakumwendea vizuri na baada ya mwaka hivi, akajitoa. Kusajiliwa kwa Weezdom pale EMB kulichangiwa na urafiki wa muda mrefu kati yake na Bahati. Alipojitoa, Weezdom alidai kuwa chanzo kilikuwa ni Diana Marua, mkewe Bahati aliyemchochea mshikaji wake kumtimua.

Madai ya Weezdom aliyatoa ikiwa ni baada ya Mr Seed kutangaza kuondoka kwenye lebo hiyo baada ya miaka miwili. Ndipo pia ikabainika kuwa wasanii wote waliokuwa wamesainiwa kipindi hicho akiwemo Rebecca Soki na David Wonder wote walikuwa wamejitoa. Kwenye mahojiano, David Wonder alisema Bahati alimpa ridhaa ya kujitoa ikiwa ni ishara tosha kwamba hakuwa akihitajika tena pale.

Bahati alia hasara ya milioni sita

Mara tu baada ya Weezdom kufunguka kilichomtoa EMB, Mr Seed naye alipata nguvu na kufichua kwamba aliondoka baada ya Bahati kumkausha malipo yake kwenye shoo moja waliyopiga mjini Thika. Lakini hata zaidi alidai Bahati alimdhalilisha mke wake Nimo aliyekuwa mjamzito kipindi hicho.

Muda wote akichambwa, Bahati alisalia kimya na alipoamua kufungua kinywa, alikana madai yote aliyokuwa ametupiwa na wasanii hao huku akisema aliamua kusimamisha shughuli za EMB kwa muda baada ya kuwekeza zaidi ya milioni sita kwa wasanii hao, lakini hakuna hata mmoja ambaye kazi zake zilikuwa zimefanikiwa kuleta kakitu.

Azindua EMB upya, Weezdom arudi

Aprili mwaka jana nilipokea simu kutoka kwa Bahati akinialika kwa hafla ndogo ya chakula cha jioni aliyoifanyia pale KICC.

Nakumbuka akinielekeza kwamba nivalie nadhifu sababu itakuwa ni hafla spesheli ambapo atatoa tamko.

Siku ya siku nilifika na kukuta Bahati kakusanya kijiji cha maceleb wote wa mji kuanzia Akothee, Jaguar, Daddy Owen kati ya wengine.

Ni hapo ndipo alipotangaza kuwa ameamua kuzindua upya lebo hiyo kwa kumsajili msanii mpya Danny Gift.

Vile vile ni kwenye hafla hiyo alitueleza hasara aliyoingia na kusisitiza kuwa licha ya hesabu hiyo, alikuwa ameshakata tamaa ya biashara ya lebo lakini roho wa Mungu ukamshauri ajaribu tena.

Pia ni kwenye hafla hiyo ambapo Weezdom alimwomba msamaha na kusema kuwa karejea nyumbani baada yao kuzika tofauti zao. Mpaka leo wapo pamoja damu damu ila Weezdom ndio tayari kabatizwa jina la ‘Watermelon’, wengi wakimchukulia kuwa kibaraka.

Tetesi Danny Gift naye kajitoa

Miezi minne tu baada ya uzinduzi huo, nilipokea taarifa za utendeti kutoka kwa produsa mmoja mkubwa aliyenifahamisha kuwa Danny Gift naye alikuwa tayari ashagura baada ya kuzenguana na Bahati.

Nilipomuuliza alikozitoa taarifa hizo, produsa huyo aliniambia kuwa ni Danny mwenyewe ndiye aliyemwelezea alipofika kwenye studio yake na kuomba kurekodi ngoma pale. Produsa akashangaa ikizingatiwa kuwa EMB kama lebo ina vifaa vyote. Nilipompigia simu Bahati, aliruka stori. Nilipompigia Danny simu kutaka kusikia upande wake, naye vile vile akaruka. Hata hivyo ninaweza kuthibitisha kwamba wawili hawa hawafanyi kazi pamoja tena.

Bahati azenguana na Peter Blessings

Maisha yalisonga na ghafla tukaanza kuona picha za Bahati na Peter Blessings zikizagaa mitandaoni. Ikatoka taarifa kwamba ndiye msanii mpya pale EMB. Miezi michache tu takriban sita hivi, Bahati na Peter wakazenguana na msanii huyo akajitoa kwenye lebo.

Kilichofuatia ni msanii huyo kutupwa ndani. Alipoachiliwa huru, alimshtumu Bahati kwa kumsababishia yale. Bahati tulipomhoji, akasema kuwa aliamua kumshtaki Peter baada yake kuvunja mkataba pasi na kufuata sheria.

Alimshutumu kwa kutumia wakili kudai fidia ya Sh1 milioni kutoka kwake na hapo ndipo naye akaamua kumfunza adabu. Pia ngoma zote za Peter alizorekodiwa EMB zimechujwa YouTube.

Kesi hiyo ipo mahakamani na inatarajiwa kutajwa ndani ya wiki mbili. Mpaka hapo, ni dhahiri Bahati hawezani na masuala ya usimamizi wa lebo, bora aifunge tu. Na kama sivyo, basi tusubirini vitimbi zaidi.