Makala

KIKOLEZO: 'Father Abraham' wa Showbiz hapa!

August 14th, 2020 3 min read

Na THOMAS MATIKO

WATOTO ni baraka kutoka kwa Mungu, vitabu vya dini vitakuambia hivyo.

Hata hivyo tunaishi katika nyakati ambazo suala la kupanga uzazi linashauriwa sana, kutokana gharama ya maisha ya sasa kuwa magumu hivyo wana wachache inakuwa rahisi kuwajukumikia.

Lakini licha ya ushauri huu, wapo watu wameamua kwenda na yale mafundisho ya dini kuwa wanapaswa kuzaa na kuijaza dunia.

Miongoni mwa watu hao pia wapo maceleb ambao wameamua kwenda na kasi ya marehemu Akuku Danger aliyezaa watoto zaidi ya mia na wake zake.

Tatizo la mastaa hawa ni kwamba wameamua kuzaa watoto wengi tu ila na wapenzi tofauti tofauti.

DIAMOND PLATINUMZ

Watoto: 5

Hahitaji utambulisho. Jamaa kwa mademu, anawabadili zaidi ya anavyobadili nguo zake za ndani. Lakini pia kwenye kuzaa ndio hachelewi.

Diamond aliyepatiwa jina la utani ‘Father Abraham’ ana watoto watano aliozaa na wanawake wanne. Mtoto wake wa kwanza yupo Japan, alimpata kabla hata hajawa maarufu. Kisha akajaliwa wawili na soshiolaiti raia wa Uganda Zari Hassan walipodeti kwa miaka minne. Halafu akapata mtoto wa kiume na Hamisa Mobetto aliyechepuka naye akiwa bado na Zari. Kisha mtoto wa tano ndiye aliyemzalisha Tanasha Donna kwenye uhusiano wao uliodumu kwa mwaka mmoja na nusu. Sasa kuna tetesi anapanga kuoa binti Mrwanda, hapo tutarajie watoto zaidi.

J BLESSING

Watoto: 5

Ni mmoja kati ya welekezaji video matata humu nchini. Kazi yake imempa umaarufu mkubwa lakini pia jamaa ni sukari ya warembo.

Blessing licha ya umri wake mdogo akiwa kwenye maisha yake ya thelathini, kajaliwa watoto kadhaa na wanawake tofauti. Tetesi zinadai kuwa ana watoto watano. Mtangazaji wa redioni Mwende Macharia ana mtoto wake. Mwanamuziki staa Avril vile vile kazaa naye huku wale wengine kawafanya kuwa siri.

ELEPHANT MAN

Watoto: 15

Staa huyu wa Dancehall kutoka Jamaica akiwa na miaka 44, ana watoto zaidi ya 15 huku taarifa zingine zikidai kuwa wanaweza kufikia 30. Hawa ni kutokana na wanawake tofauti.

Wakati mmoja alipokabiliwa na tuhuma za kubaka, Elephant Man alijitetea kwa kusema kuwa hawezi kumbaka mwanamke wakati akiwa ana ‘baby mama’ 20. Tatizo hata hivyo ni kwamba kakabiliwa pia na kesi za kuwa ‘deadbeat’ kwa maana hatoi matunzo kwa watoto wake.

DMX

Watoto: 15

Rapa huyu wa Marekani kapitia mengi sana. Kalala jela kwa mwaka mzima kwa sababu ya kukwepa kulipa ushuru.

Kuna kipindi alikuwa maarufu sana na ni wakati huu aliamua kuijaza dunia. Akiwa na miaka 49, ni baba wa watoto 15 na wanawake tofauti.

Kati ya watoto hao 15, wanne aliwapata na mke wake wa zamani Tashera Simmons. Walitalikiana 2012 na hapo jamaa akaona isiwe kesi, bora aendelee kuzalisha kila rinda alilokutana nalo. Kifunga mimba wake alizaliwa 2016 na mpenzi wake Desiree.

Naye pia amekabiliwa na kesi kadhaa za kutotoa matunzo kwa watoto wake wote. 2013 alitangaza kuwa kafilisika huku akisema sababu kubwa iliyomsotesha ni majukumu ya kugharimia watoto hao.

BOB MARLEY

Watoto: 11

Nguli huyu wa Reggae alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 36. Hadi kifo chake alikuwa amezaa watoto 11 na wanawake saba akiwemo aliyekuwa mke wake Rita Marley. Katika ndoa yake na Rita alijaliwa watoto watatu. Zipo tetesi zinadai kuwa huenda jamaa aliacha watoto zaidi.

EDDI MURPHY

Watoto: 10

Mcheshi huyu mkongwe ni mzee wa kazi. Akiwa na miaka 59, jamaa bado ana nguvu za kuleta wana duniani.

Ana watoto 10. Tano kati yao aliwapata na mke wake wa zamani Nicole Mitchell. Mtoto wake wa kwanza ana miaka 31 na alimpata na demu wake wa zamani Paulette McNeely kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Kwa sasa anatoka na kichuna Paige Butcher mwenye miaka 41 na wana watoto wawili. Butcher alimzalia mtoto wake wa tisa 2016 na wa 10, 2018.

THE DREAM

Watoto: 9

Rapa huyu Mmarekani naye pia halalishi. Anazalisha kweli kweli. Akiwa na umri wa miaka 42 tu, jamaa atakuwa pengine ana nia ya kuendelea kuijaza dunia.

Tayari ana watoto tisa, watano kawapata na mke wake wa zamani Nivea aliyemwoa 2004. Baada ya hapo akamwoa mwanamuziki Christina Millian na kumzalisha binti mmoja 2010. Miaka mitatu baadaye akakutana na msupa mwingine kwa jina Lydia Nam na kumzalisha mtoto wa kiume.

FUTURE

Watoto: 6

Rapa huyu alipata umaarufu mkubwa alipokuwa akitoka na staa mwanamuziki Ciara. Ana watoto sita kila mmoja na mamake, Ciara akiwa mmoja wa waliomzalia. Mzee wa kazi kama vile shughuli hii hajamalizana nayo.