Makala

KIKOLEZO: Filamu iligeuka nuksi kwao

October 18th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

MAPENZI bwana achana nayo kabisa.

Huu ni ugonjwa wa aina yake. Hauna tiba. Huleta utemi kwa kila anayejikuta akikabiliana nao. Hata maceleb pamoja na ustaa wao, mapenzi huwahangaisha tu.

Wapo waliochora chale kisa, mapenzi. Lakini tena wakaishia kuzifuta kwa machungu pale penzi linapokwisha. Lakini si nao ni binadamu?

Penzi huchipuka popote pale hata kazini. Nao pia wapo maceleb wamejikuta wakiotesha penzi wakiwa kazini. Wapo waliofanikiwa kudumisha penzi lao lililootea kazini. Na pia wapo ambao mahusiano yao yalivunjwa kisa, kazi. Wafuatao ni mfano tu. Waigizaji hawa ndoa zao zilivurugwa na filamu.

BRAD PITT NA JENNIFER ANISTON (2000-2005)

FILAMU: Mr & Mrs Smith

Ndoa ya waigizaji staa Brad Pitt na mkewe wa zamani mwigizaji mcheshi Jennifer Aniston ilidumu kwa kipindi cha miaka mitano tu toka 2000.

Penzi la nyota hawa lilikuwa tamu ajabu, kila aliyewaona alitamani. Hata hivyo ndoa hiyo iliingia mdudu 2005 wakati filamu ya Mr & Mrs Smith ilipotoka.

Brad alikuwa ndiye staa wa filamu hii akiigiza pamoja naye nyota mwingine Angelina Jolie. Kwenye harakati za kikazi, mapenzi yakaota kati yao na akajikuta akimchepukia Jennifer.

Wakaamua kutalikiana miezi michache kabla ya uzinduzi rasmi wa filamu hiyo. Jennifer alisema sababu zao za kutalikiana hazingeepukika. Baadaye Brad alikuja kukiri kwamba alipagawishwa na penzi la Angelina kipindi wakiwa wanashuti filamu hiyo.

TOM CRUISE NA MIMI ROGERS (1987-1990)

FILAMU: Days of Thunder

Kipindi filamu hii ilipotoka mapema 1990, mwigizaji nyota pale Hollywood Tom Cruise, tayari alikuwa ameingia kwenye ugomvi na mke wake wa wakati huo Mimi Rogers.

Ugomvi huo ulitokana na michepuko ya mara kwa mara ya Tom. Filamu hii pia ilichangia kwani Tom aliigiza pamoja na nyota mwingine Nicole Kidman ambaye alianza kuchepuka naye wakati akiwa yupo kwenye ndoa na Mimi. Mimi aliposhindwa kuvumilia aliomba talaka. Talaka hiyo ikatoa fursa kwa Cruise kumwoa Nicole mwaka mmoja baadaye.

RYAN REYNOLDS NA SCARLETT JOHANSSON (2008-2011)

FILAMU: Green Lantern

Mwigizaji wa kike Blake Lively na Ryan Reynolds walianza kuchepuka wakati wakiwa wanashuti filamu ya Green Lantern walikoigiza kama wahusika wakuu.

Kipindi hiki Blake alikuwa kwenye mahusiano na staa wa Gossip Girl, Penn Badgley huku Ryan akiwa mume wake staa Scarlett Johnasson.

Blake na Ryan waliishi kuchepuka kimya kimya huku wakitumia shughuli yao ya kikazi kama kisingizio. Hata hivyo hawangetoboa kuiweka siri kutokana na mapaparazi waliokuwa makini sana nao. Punde tu filamu hiyo ilipotoka Scarlett akamtaliki Ryan huku Blake akitemwa na Penn. 2012 Blake na Ryan wakafunga ndoa.

JAMES CAMERON NA LINDA HAMILTON (1997-1999)

FILAMU: Titanic

Mwelekezi James Cameroon aliyeandaa filamu maarufu ya Titanic alijikuta akilemewa na mahaba ya mwigizaji Suzy Amis wakati wa uandaaji wa filamu hiyo.

Kipindi hiki 1997, Cameroalikuwa kwenye ndoa yake ya nne na Linda Hamilton ambayo hata haikuwa imemaliza miezi tisa alipoanza kumchepukia na Suzy.

Licha ya ugomvi wa kila siku nyumbani kutokana na mchepuko, Linda alijitahidi sana kuhakikisha ndoa yao haivunjiki na ndio sababu alisalia na mume wake huyo kwa miaka miwili zaidi akijaribu kuiokoa. Hata hivyo nguvu la penzi la suzy likawa lishamtoa Cameron uchizi na kwa kuona hana namna, Linda akaomba talaka. Cameron mara tu baada ya talaka akamwoa suzy kama mke wake wa tano. Mpaka leo ndoa yao imesimama.

BEN AFFLECK NA JENNIFER LOPEZ (2002-2004)

FILAMU: Daredevil

Wakati Ben Affleck na Jennifer Garner walipoanza kushuti filamu ya Daredevil, 2002, wote walikuwa kwenye mahusiano makubwa.

Ben alikuwa ndio kamchumbia Jennifer Lopez huku Garner akiwa ni mke wake Scott Foley. Mapenzi ya yaliwazidia sana japo walijitahidi sana kudumisha ndoa zao.

Hata hivyo filamu hiyo ilipotoka Februari 2003, Ben akaamua kuvunja uchumba wake kwa Lopez ikiwa ni wiki kabla ya ndoa yao. Apili 2003 naye Garner akamtaliki Foley. Oktoba 2004, Ben na Garner wakaanza kuonekana hadharani pamoja. Ben baadaye alikiri waziwazi kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na Garner kipindi wanashuti Daredevil.