Makala

KIKOLEZO: Jay Z kakafunga mbaya!

June 7th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

KWA miaka mingi kumekuwepo na ule utani kwamba kama rapa-mwigizaji Ludacris akiamua kuja Afrika na kudai hela za matangazo ya biashara kutokana na picha zake kutumiwa sana kwenye vinyozi na saluni, basi ataishia kuwa rapa wa kwanza kuwa bilionea.

Hii ni kwa sababu kila ukikatiza miji mbalimbali ya Afrika, kati ya saluni 10 takriban nane huwa zimetundika picha zake kama njia ya kuwavutia wateja.

Lakini kama Ludacris amekuwa na mawazo hayo, basi atakuwa alisleki sana sababu Jumatatu ya wiki hii, rapa Jay Z aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu akitajwa kuwa rapa wa kwanza kufanikiwa kuwa bilionea.

Kwa zaidi ya mwongo, Jay Z hajawahi kukosa kuwa kwenye listi ya 10 bora ya marapa matajiri zaidi duniani.

Lakini mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 49 pekee, kajitoa kwenye ligi hiyo na kujipaisha hadi levo nyingine kabisa ya kipekee.

Ndiye rapa bilionea pekee aliye hai kwa sasa na tena wa kwanza. Lakini hadi anafikia upeo huu, Jay Z kafanya nini?

Kujitambua

Kwenye tafsiri ya ubeti wa mwisho wa wimbo wake U Don’t Know, Jay Z anaangusha mistari mizito akijisifia namna alivyo mpambanaji asiyekubali kushindwa.

‘Nauzaga barafu msimu wa baridi, Nauzaga moto kuzimu, mimi ni mtafutaji, nauziaga maji kisima, nilizaliwa kusaka keki, kupanda levo na kufanya mapinduzi, nilizaliwa kutoa amri sio kuamrishwa, wapuzi hamniwezi, nyie masnichi huyu mnayemfanyia mzaha ni Big Jay, Kamwe hawezi kushindwa, haitawahi kutokea…’

Wimbo huu aliuachia miaka 18 iliyopita ukiwa mojawapo ya vibao kwenye albamu yake ya The Blueprint. Wakati huu alikuwa ni tajiri ila hakuna aliyewazia kwamba angetokea kuja kufunika kama sasa.

Ila Jay Z alijielewa, alijitambua na akajipanga kufanya mapinduzi jinsi tu alivyochana.

Wanasema utakula unachokiota.

Jay Z aliota kuwa sio tu rapa mkali lakini pia mjasiriamali wa kupigiwa mfano.

Leo hii, ndoto yake imetimia akiwa amewekeza katika kila biashara unayoweza kusema ina pesa.

Ujasiriamali

Jay Z ni kama vile mababu bilionea wa nyumbani Chris Kirubi au Manu Chandaria ambao haiwezi kupita siku hujatumia bidhaa kutoka kwa kampuni zao au kupata huduma kutoka kwa kampuni wanazomiliki.

Rapa huyu katanda mabawa yake kwenye biashara kibao, utaanza na muziki akiwa anamiliki lebo yake ya Roc Nation, pia yupo kwenye fasheni akiwa na lebo ya Rocawear, yupo kwenye usafiri akiwa mmoja wa wanahisa wakubwa kwenye kampuni ya Uber, yupo kwenye michezo hasa basketiboli anakoripotiwa kuwa kawekeza hisa kwenye klabu kadhaa ikiwemo Brooklyn Nets ambayo aliuza hisa zake 2013, kawekeza kwenye biashara za vileo kama vile D’Usse pia na Armand de Brignac. Pia yupo kwenye biashara za ujenzi na umiliki wa majengo (Real Estate), kawekeza kwenye vyombo vya habari na pia anamiliki kampuni ya usambazaji na uuzaji muziki Tidal. Kwa kifupi Jay Z yupo kila mahali.

Safari

Maisha yake ya utotoni yalikuwa magumu sana katika mitaa ya Brookyln.

Ndoto yake ya ujasiriamali ilianza akiwa mchanga kwa kujihusisha na biashara haramu ya uuzaji dawa za kulevya.

Baadaye akapata upenyo na kugeukia muziki akianzisha lebo yake Roc-A-Fella Records iliyoachia albamu yake ya kwanza Reasonable Doubt 1996. Toka wakati huo mpaka leo, kaingiza zaidi ya dola 500 milioni kupitia muziki pekee huku akishinda tuzo 22 za Grammy Awards.

Baada ya kupata umaarufu akaamua kuutumia kuikuza brandi yake hata zaidi.

Ndivyo lebo yake ya mavazi Rocawear ilianza 1999, kisha akafuatisha na ubia na kampuni ya Bacardi kutengeneza kileo cha D’Usse. Na zingine zikafuata baadaye.

Hesabu zilivyoingiana

Ili kuziweka hesabu zake sawa jarida la Forbes lilifanya uchanganuzi wa uhusika wake katika biashara mbalimbali anazomiliki binafsi au na wenzake na hii hapa orodha yao;

•Armand de Brignac

(dola 310 milioni)

Hisa zake kwenye kampuni hii ni asilimia 100. Kampuni hii alianzisha 2006 na akatumia muziki wake kuitangaza na mpaka sasa imemwingizia kiasi hicho cha fedha.

•Uber

(dola 70 milioni)

Hisa zake kwenye kampuni hii ni za thamani ya dola 70 milioni kwa sasa. Alinunua zake kwenye kampuni hiyo iliyoanzishwa na Travis Kalanick 2013. Wakati akinunua hisa hizo alitumia dola 2 milioni pekee na alipotaka kuongezea nguvu zake kwenye kampuni hiyo kwa kuzidisha hisa zake kwa kumwekea Kalanick dola 5 milioni zaidi mezani, ofa hiyo ilikataliwa.

•D’Usse

(Dola 100 milioni)

Kampuni itengenezayo kileo hiki aina ya cognac anaimiliki kwa ushirikiano na kampuni ya Bacardi ambayo kipato chake kimekuwa kikifikia asilimia 80 kila mwaka.

Wateja wengi wa kileo hicho wanatajwa kuwa watu ambao ni mashabiki wakubwa wa rapa huyu na wanaopenda kuhusishwa naye.

•Tidal

(Dola 100 milioni)

Jay Z alinunua kampuni hii 2015 kwa dola 60 milioni na kisha kuibrandi upya kwa kuwasainisha mastaa kama mkewe Beyonce, Kanye West, Calvin Harris miongoni mwa wengine. Mastaa hao wamechangia pakubwa kuimarisha mapato yake.

Lebo hii ni ya kusimamia wasanii na wanamichezo. Miongoni mwa wanamichezo waliosainiwa hapa ni Kevin Durant na Gurley, wanamuziki kama Rihanna, J. Cole miongoni mwa wengine ambao umaarufu wao umekuwa baraka kibiashara.

•Muziki

(Dola 500 milioni)

Ndio makadirio ya mkwanja alioweza kuingiza kupitia mauzo ya albamu na pia malipo ya shoo kwa zaidi ya mwongo. Hata hivyo mkwanja huu ni kabla ya makato ya kodi. Jay Z anamiliki majumba kadhaa ya nguvu yenye bei mbaya ambayo hukodisha, mengine akiishi.

•Sanaa

(Dola 70 milioni)

Katika kibao chake Picasso Baby, anasifia mchoro wa msanii Jean-Michel Basquiat alioangika jikoni. Imebainika kuwa kwa zaidi ya mwongo mmoja amekuwa akinunua michoro ya wasanii maarufu kama huyo Basquiat huku 2013 akidaiwa kutumia dola 4.5 milioni kununua ‘Mecca’ mojawapo ya kazi za msanii huyo.