Makala

KIKOLEZO: Kimeeleweka!

August 30th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

HUWEZI kumchukia rapa wa kike kutoka Amerika, Missy Elliott hasa kama wewe ni kijana wa jana.

Ni miongoni mwa watumbuizaji waliochangia pakubwa kubadilisha upepo wa muziki wa Hip hop Marekani na duniani kwa ujumla.

Heshima ya Missy Elliott inatokana na vitu vingi sana tu. Akiwa na umri wa miaka 48, huyu sio rapa wa leo. Ni mmoja wa marapa wa kike waliofanikiwa sana kwenye taaluma hiyo kutokana na kazi alizoweza kuachia katika kipindi ambacho alifanya muziki kwa fujo.

Lakini kikubwa zaidi kinachomfanya kupendwa na vijana wengi wa jana na pengine idadi ndogo ya kizazi cha sasa, ni bidii aliyoiweka kutoka kwenye muziki kwa kupambana na marapa wanaume enzi ambazo marapa wa kike wangetosha ganja la mkono. Kwa kifupi, walikuwa wachache mno ukilinganisha na enzi hizi za kina Nicki Minaj.

Hivi majuzi, Missy Elliott alitambuliwa kwa mchango wake kwenye Hip hop.

TUZO YA VIDEO VANGUARD AWARD

Jumatatu ya wiki hii, alipewa heshima yake kwa kutuzwa tuzo ya Michael Jackson Video Vanguard Award kwenye hafla ya utoaji tuzo za MTV Video Music Awards.

Hii ni tuzo ya hadhi kubwa na heshima kumuenzi mtu kama yeye, aliyeibuka na ubunifu mkubwa katika video zake licha ya kuwa enzi hizo teknolojia haikuwa imepiga hatua kama sasa.

Marehemu Michael Jackson ndiye aliyekuwa msanii wa kwanza kupokea tuzo hiyo 1991. Toka kipindi hicho waliopokea ni Janet Jackson(dadake MJ), Britney Spears, Justin Timberlake, Beyonce, Jennifer Lopez kwa kuwataja wachache tu.

Akipokea tuzo hiyo Missy Elliot alikuwa na machache.

“Nimejituma sana kwa zaidi ya miongo miwili kwenye fani hii na wala sikutegemea kwamba leo ningelikuwa hapa nikipokea tuzo hii. Tukio hili hakika lina uzito mkubwa kwangu,” akasema.

Kabla kupokea, Missy Elliott alitumbuiza kwa staili ya kipekee, akiwarejesha waliokuwepo ukumbini miaka 20 nyuma kipindi alipoanza taaluma yake. Moja kati ya kazi zake zilizomtoa na ambayo alitumbuiza ni Supa Dupa Fly. Kizazi cha Wamlambez na Pekejeng kipindi inatoka ‘hit’ hii, hakikuwa bado kimewasili duniani. Kizazi alichofurahisha sana ni kile cha kati ya miaka ya 80 kuelekea 90.

Utumbuizaji wake kwenye hafla hiyo ulikuwa wa kipekee. Katika kila wimbo wa zama hizo aliotumbuiza stejini, rapa huyo alihakikisha anatokea vitofauti.

Kuna kipindi alitokea kavalia kama kinyago, mara kama jini na pia kuna kipindi aliibuka na madansa wake wa enzi hizo ambao kwa sasa umri wao ni mkubwa.

MASTAA WAMMIMINIA SIFA

Mastaa wengi waliokuwemo kwenye tuzo hizo na ambao walitizama kupitia Youtube, TV au vyombo vingine mbalimbali, walimsifia.

“Kila mmoja wetu kamwiga Missy Elliott kwa namna moja ama nyingine, mimi nikiwemo,” alisema Cardi B aliyepata heshima ya kumpokeza tuzo hiyo.

Kwa mkongwe Timberlake, alimsifia kwa kuwa mbunifu kwa staili nyingi alizozichanganya na kuzilazimishia kwenye Hip hop.

“Ana staili yake ya kipekee, ni RnB, ni Hip hop ni muziki wa ki-Missy,” akasema.

Kwa produsa na mwanamuziki wa siku nyingi Pharrell Williams, kilichomkosha kutoka kwa lejendari huyo ni, “uwezo wake wa kuweka lafudhi yake katika video zake, sisi wenyewe hatujawahi kufanya kitu kama hicho,” akamwaga.

Na kulingana na produsa wake wa enzi hizo ambaye ni mshikaji wake wa karibu sana Timbaland, Missy Ellliot alikuwa king’ang’anizi katika kufanya vitu alivyopania hata alipoonekana anakosea.

“Missy Elliott angekuambia wakati mwingine kukosea ndiko kupata. Alipenda kubahatisha mambo mengi na katika hilo kuibuka na ubunifu wa kila aina,” akatiririka.

KIZAZI CHAMSHANGAA

Baada ya ukimya wa miaka kadhaa, ghafla kukaanza kuwa na hamu kutoka kwa wengi kutaka kumwona akichangamka kwenye gemu kama zamani.

Harakati hizi zilianza 2015 baada yake kupiga shoo kwenye tamasha ya Super Bowl Halftime.

Baada ya utumbuizaji wake kuwashangaza wengi hasa wa kizazi cha sasa, walikesha kwenye mitandao ya kijamii wakitaka kumfahamu huyu ‘msanii mpya’ aliyekuja kwa ubaya.

Ni jambo lililomfurahisha na kumchekesha Missy Elliott na kumsukuma kwenye Twitter kumimina mawazo yake.

“Inafurahisha kusikia na kuona mitazamo ya chipukizi wengi wanaofikiria mimi ni msanii mpya. Hii inakuonyesha kwamba bado natisha na kuwa nitaendelea kuvuruga kwa zaidi ya miaka mingine 20 ijayo,” akafunguka.

Kutokana na kampeni hiyo, alikatiza ukimya na akaingia studio tena ambako aliandaa EP yake Iconology ambayo inazidi kufanya vizuri.

Missy Elliott ni mfano mzuri tu kwamba, hata simba awe mzee vipi, bado atakula nyama tu.