Makala

KIKOLEZO: Kweli kwa 'ground vitu ni different'

March 6th, 2020 3 min read

Na THOMAS MATIKO

WASWAHILI husema, usidanganywe na rangi ya chai, utamu wa chai huwa ni sukari.

Kimsingi maana ya kauli hii ni kuwa sio vyote vinavyong’ara ni dhahabu.

Mfano mzuri ni Instagram ambapo watu wana mazoea ya kujifanya wanaishi maisha ya kifahari wakati kwa ground, vitu ni different.

Hali hii pia ipo kwenye tasnia ya usanii. Wapo wasanii wengi ambao ni maarufu sana kiasi cha kuwafanya maelfu ya mashabiki wao kuamini kuwa wanaishi vizuri au wana pesa za kutosha wakati sio kweli.

Hii ndio sababu, kwa mfano, kwenye tasnia yetu ya muziki, wanamuziki wengi wameishia kupotea. Ni wakubwa kwenye mitandao ya kijamii ila katika maisha ya uhalisia hawana kitu.

Sasa basi ikiwa unafikiria kuwa ni wasanii wa hapa nyumbani pekee wanaopitia hali kama hiyo, utakuwa umekosea.

Kule majuu wapo mastaa wengi waigizaji na wanamuziki wenye majina makubwa na ufuasi mkubwa, ila ni miongoni mwa wenye utajiri mdogo sana ukilinganishwa na umaarufu wao. Hawa ni baadhi tu:

LINDSAY LOHAN

Utajiri (Dola 500,000)

Lohan ni mmoja kati ya waigizaji maarufu sana kule Hollywood. Ana miaka zaidi ya 15 kwenye gemu. Ana ufuasi mkubwa kote duniani. Kwa mfano kwenye Instagram, ana zaidi ya wafuasi milioni nane.

Cha kushangaza ni kuwa pamoja na umaarufu wake na muda ambao amedumu kwenye gemu, utajiri wake ni mdogo sana ukilinganishwa na mastaa wengine waliodumu katika tasnia hiyo kwa muda sawia.

Itakumbukwa kuwa 2011 alitangazwa kuwa kafilisika baada ya kulemewa na madeni makubwa aliyokuwa nayo. Akapata mchongo wa kupozi uchi kwenye jarida la Playboy na kulipwa dola milioni moja. Hata hivyo kiasi kikubwa cha fedha hizo kikatumika kulipia madeni yake hayo. Halmashauri ya ukusanyaji kodi ya Marekani mpaka leo inamdai akiwa anaendelea kulipa pole pole.

50 CENT

Utajiri (Dola 15 milioni)

Utajiri wake wa sasa ni kiasi kikubwa kwa watu wengi, ila kiuhalisia, 50 Cent anapaswa kuwa na thamani kubwa zaidi ya hii ya sasa.

Ikumbukwe kuwa wakati akianza muziki na kundi la G Unit, 50 Cent alipiga mamilioni ya dola. Kwa mfano, 2004 aliingiza zaidi ya dola 70 milioni kutokana na matangazo ya kibiashara pekee pasi na kuweka mapato ya nyimbo na shoo. Utajiri huo ulianza kufifia baada ya kundi kusambaratika. Mnamo 2008 alianzisha kampuni ya filamu Cheetah Vision iliyopokea mkopo wa dola 200 milioni kuistawisha.

Miaka miwili baadaye akapiga dola 10 milioni kutokana na shoo. Licha ya kukafunga hivyo, 2015 alitangaza kuwa kafilisika alipoamrishwa na mahakama alipe fidia ya dola 5 milioni baada ya kuvujisha video ya ngono ya mrembo Lastonia Leviston.

Kipindi hicho madeni aliyokuwa nayo yalikuwa yamefikia dola 50 milioni na alikuwa akihangaika kuyalipa. Ndio sababu ya thamani yake kushuka sana.

NICOLAS CAGE

Utajiri (Dola 25 Milioni)

Mwigizaji huyu mkongwe ana bahati sana kwamba kipaji chake kimeendelea kumpa michongo ya maana kwenye filamu lau sivyo angelikuwa ameisha zamani.

Kuwa wakati alikuwa na utajiri wa zaidi ya dola 150 milioni lakini uraibu wake wa kukesha akibeti kwenye macasino ulimkausha vibaya. Kando na uraibu huo, alikuwa na tabia ya matumizi mabaya ya kifedha kwa kununua vitu kwa thamani iliyopitiliza. Aliwahi kumiliki majumba 15 aliyonunua kwa bei mbaya, ndege yake binafsi na hata nyoka wa kufuga aina ya Cobra.

Aliamini pesa haziwezi kumwishia lakini zilimpungukia kweli kweli baada ya kujikuta akiwa na madeni chungu nzima. Alianza kuuza mali hizo moja baada ya nyingine ili kulipia madeni.

MEL B

Utajiri (Dola 10 milioni)

Mel B alianza kuimba miaka ya tisini akiwa na kundi la Spice Girls. Huko ndiko alikoanza kupata utajiri wake. Baada ya miaka kadhaa ya usanii, Mel B alifanikiwa kujikusanyia utajiri mkubwa wa zaidi ya dola 38 milioni.

Hata hivyo kilichomponza na kuishia kumfilisisha ni matumizi mabovu ya pesa hizo. Kwa mfano aliwahi kuwa na mkusanyiko wa begi za mkononi zenye thamani ya dola 500,000 kwa pamoja.

Pia kuna wakati alitumia dola 200,000 kununua gari lisilopenyeza risasi au bomu. Herini zake pia ni za bei mbaya akiwa na rundo kubwa linalofikia dola 500,000.

Pete na viatu pia kwa ujumla ni zaidi ya dola 600,000.

Matumizi haya mabaya yaliishia kumwacha akijipata akiwa na madeni makubwa sana. Ingawaje ameendelea kushiriki kama jaji wa America’s Got Talent, sehemu kubwa ya kipato chake hicho kizuri amekuwa akikitumia kulipia madeni.

2017 alipotemana na mumewe, aliuza mjengo wake wa kifahari uliopo na kutumia fedha hizo kulipia madeni.

PAMELA ANDERSON

Utajiri (Dola 5 milioni)

Huyu ni staa mwingine mkubwa pale Hollywood ambaye amekuwepo kwa miaka mingi. Hata hivyo, hana mkwanja wa maana ijapokuwa ni maarufu kupindukia.

Aliwahi kuwa na utajiri mkubwa wa zaidi ya dola 12 milioni lakini kwa sasa yupo yupo na vijimilioni vya wasiwasi. Inasemekana alianza kusota 2009 baada ya kutumia sehemu kubwa ya fedha alizokuwa nazo kufanyia jumba lake ukarabati.

Hali hiyo iliishia kumwacha kwenye deni nzito kiasi cha kuishia kushtakiwa na kampuni iliyokuwa ikimfanyia ukarabati huo kwa kushindwa kuilipa.