Makala

KIKOLEZO: Mapenzi yazima taa yao

February 14th, 2020 2 min read

Na THOMAS MATIKO

LEO ndiyo siku ya wapendanao al-maarufu Valentine’s Day.

Ndiyo siku ambayo wapenzi hujitokeza kudhihirishiana mapenzi yao.

Huwa sio siku ya ugomvi, ni siku ya mapenzi tu.

Ukiwa katika huo muktadha wa mapenzi, tumeshuhudia baadhi ya wasanii wakizama kwenye mapenzi na mahusiano yao kuishia kwenye ndoa.

Lakini kitu kingine ambacho tumeshuhudia ni kwa baadhi ya wasanii kupotea kwenye gemu baada ya kuchumbiana na wapenzi wao au mara tu wafungapo ndoa. Hii hapa listi niliyoibuka nayo ya baadhi yao tu.

BEN POL

Ben Pol alikuwa mmoja kati ya wasanii wakali kutoka Bongo walioshia kupata umaarufu hapa nchini kutokana na bidii yao ya kimuziki.

Msanii huyu alikuwa akijituma sana studio na mara kwa mara aliishia kuachia nyimbo zilizoishia kuwa ‘hit’. Lakini ghafla upepo huo ulibadilika alipokutana na binti tajiri Anerlisa Muigai mwaka mmoja uliopita. Mapenzi yalimnogea na kumpoteza kabisa Ben Pol kwenye chati za muziki. Hata hivyo wengi wanamini kuwa kando na kulewa mapenzi ya Anerlisa, fedha za kutosha za binti huyo pia zimemvuruga akili akashindwa kumakinikia muziki. Kwa sasa Ben Pol haonekani akijituma kwenye muziki wake, anaufanya ilimuradi tu. Kashindwa kuachia kete kali. Asilimia kubwa ya mashabiki ni wenye mtazamo kuwa, jamaa kapoteza ladha ya muziki baada ya kumpata msupa wa kumfuga.

WENDY KIMANI

Miaka michache iliyopita, Wendy Kimani alikuwa mmoja wa wanamuziki wa kike mashoka hapa nchini. Alijitahidi sana kufanya muziki na mara kwa mara angeachia kazi mpya mpya. Miongoni mwa ‘hits’ zake ni kama vile Unajua aliyoshirikishwa na Gilad Millo, Haiwi Haiwi aliyokaa kwenye biti moja na Bien Baraza wa Sauti Sol. Bidii hii ilikuwa ni kabla ampate mume wake mzungu wa Kidachi Marvin Onderwater. Toka waoane 2014, muziki kwa Wendy umebaki stori.

EMMY KOSGEI

Hakuna ambaye hakuwa akimfahamu Emmy licha ya kwamba nyimbo zake nyingi aliziimba kwa lugha ya nyumbani kwao Kalenjin.

Shoo alipiga nyingi sana huyu Emmy miaka hiyo. Kisha akatokea mzee mmoja Mnaigeria askofu Anselm Madubuko ambaye kwa sasa atakuwa anakaribia kugoma miaka sabini kama sikosei.

Toka alipoolewa na mzee huyo mwenye pesa zake, Emmy ni kama vile alishasahau kabisa kwamba aliwahi kuwa na sauti nzuri ya kuimba. Mara ya mwisho kumsikia nashindwa kupata picha kamili.

NYOTA NDOGO

Kama yupo msanii mmoja aliyeiwakilisha Mombasa vizuri kwenye chati za muziki, basi ni Nyota Ndogo ambaye sasa kapotea kabisa.

Duru zinaniarifu kwamba kwa sasa Nyota kajikita zaidi kwenye masuala ya ujasiriamali. Lakini michakato yote hii ilianza mara tu baada yake kukutana na mume wake mzungu Henning Nielsen. Ndoa yao ilifanyika miaka mitatu iliyopita baada ya kuwa kwenye uhusiano wa miaka kadhaa. Tayari Nyota alikuwa ashapotea.

CECE SAGINI

Namkumbuka akiwa msanii ibukia ambaye kama angeendelea kwa kasi aliyoanza nayo, basi angelikuwa mwanamuziki mkubwa kwa sasa hapa nchini.

Lakini kabla ya hilo, mapenzi yalimkuta. Alimpenda mpiga picha Victor Peace ambaye alimchumbia 2016. Kipindi hiki bado Sagini alikuwa akiufanya muziki wake wa Afro Beats kwa bidii na vishindo. Ndoa yao ilipofuata miaka miwili baadaye, Cece ndio kama hivyo kazima. Mara ya mwisho yeye kujitokeza alisema kahamia kwenye muziki wa injili ila mpaka leo bado kazi yake ya kwanza ya injili inasubiriwa.