Makala

KIKOLEZO: Mastaa waliolala nyuma ya nondo

June 28th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

WANGWANA walisema dawa ya moto ni moto.

Ukiua kwa upanga nawe utauliwa kwa upanga.

Juma hili mawazo hayo yalipata picha nzuri sana baada ya mwigizaji maarufu wa Kibongo Wema Sepetu kuachiliwa huru kutoka jela kwa dhamana.

Pamoja na kuwa ni staa, ukorofi wake wa kutaka kushindana na sheria uliishia kumweka pabaya. Lakini Wema sio mwanaburudani wa pekee kuwahi kutupwa nyuma ya nondo.

WEMA SEPETU

Kosa: Kuidharau mahakama

Kwa miezi kadhaa sasa, mwigizaji huyu amekuwa na kesi inayoendelea anakoshtakiwa kwa kuchapisha video ya ngono kwenye Instagramu.

Wiki mbili zilizopita alitakiwa kufika mahakamani kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo. Hata hivyo Wema alifika lakini hakusubiri kusikiza kesi hiyo akiamua kuondoka kwa kile alichokisema ni kuumwa na tumbo.

Hakimu aliyekuwa akiisikiza kesi hiyo aliitaja hatua ya Wema kuwa ya kuidhalilisha korti, aliamrisha akamatwe na siku chache baadaye akaamua atupwe gerezani kwa siku saba. Kwa wiki nzima Wema alisotea kwenye jela ya Segerea hadi alipoachiliwa kwa dhamana mpya Jumatatu ya wiki hii huku akionywa atafungwa kwa muda zaidi hadi kesi itakapoamuliwa endapo ataishia kuidharau mahakama na kukosa kufika tena wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo.

MARIJANI

Kosa: Ugomvi

Mwanamuziki huyu mzalendo aliyepata umaarufu wake kipindi akiwa Grand Pa, aliwahi kusota jela kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kupigana akiwa seli.

Kwa maneno yake, 2011 akiwa anatoka kwenye shoo, alikamatwa na polisi akiwa njiani kuelekea nyumbani baada ya kuzenguana nao. Alifungiwa kwenye seli mjini Narok na akiwa humo alizua vurugu na mmoja wa mahabusu. Waliishia kupigana na kilichofuatia ni yeye kufungwa kwa mwaka mzima kwa kosa hilo.

RAPCHA THE SAYANTIST

Kosa: Uharibifu wa mali

Mcheshi huyu aliyepata umaarufu wake kupitia komedi ya Churchill Show aliwahi kutupwa jela kwa miezi kadhaa kutokana na vurugu ya ulevi ulioishia kusababisha uharibifu wa mali.

TID

Kosa: Kumjeruhi mtu

Siku za hivi karibuni TID amekuwa akitrendi baada ya kuposti picha akiwa amepigwa kisawasawa. Alidai kuvamiwa na majambazi. Hata hivyo waliomshambulia walitokea na kusema TID ni rafiki yao wa siku nyingi na tatizo lilianza baada yake kuwazushia vurugu pale walipoganda kumpa hela za kwenda kununua dawa za kulevya.

TID alifungwa jela mwaka mmoja 2008 baada ya kumvamia na kumjeruhi vibaya binti mmoja aliyekuwa rafikiye. Baada ya kuachiliwa huru, TID alirudi kwenye maisha yake ya maunga.

BLAQY

Kosa: Kusababisha Ajali

Ni mmoja wa wasanii waliopata umaarufu nchini kwa kuachia video ya kitata na yenye mshairi chafu chafu.

Aliwahi kukamatwa 2014 kwa kosa la kumgonga mtu na gari na kisha kutoroka. Aliishia kutupwa jela kwa siku 37 baada ya kushindwa kulipia dhamana hadi pale Gavana Mike Sonko akiwa seneta kipindi hicho alipomwokoa.

ELIZABETH ‘LULU’ MICHAEL

Elizabeth Lulu. Picha/ Maktaba

Kosa: Mauaji

Toka aachiliwe huru Mei 2018, mwigizaji huyu wa Bongo Movie amekuwa akijitahidi sana kuishi maisha ya usiri sana akikwepa vyombo vya habari.

Lulu alisukumwa nyuma ya nondo kwa kosa la kumuua bila kukusudia mpenzi wake Steven Kanumba baada yao kugombana.

Kifungo chake kilikuwa cha miaka miwili lakini aliachiliwa huru baadaye kutokana na msamaha wa Rais John Magufuli.

BOBI WINE

Kosa: Uchochezi

Mara kwa mara, mwanamuziki huyu wa Uganda ameishia kujipata seli kwa siku kadhaa kutokana na kuendelea na kampeni yake ya kupingana na utawala wa Rais Yoweri Museveni.

Aliwahi kulala jela kwa zaidi ya wiki nzima kwa kile kilichotajwa kuwa uchochezi wa umma dhidi ya serikali.

VYBZ KARTEL

Kosa: Mauaji

Katika visiwa vya Jamaica, bado mkali wa Dancehall mwenye umaarufu mkubwa duniani Vybz Kartel anaeendelea kusotea jela kwa kosa la mauaji.

Kartel alihukumiwa kifungo cha maisha 2014 kwa kosa la kumuua aliyekuwa produsa wake Clive Lizard Williams 201.

Hata hivyo kwenye kifungo hicho, atahitajika kuhudumu jela kwa miaka 35, ndipo aweze kupewa fursa ya kuomba kuendeleza kifungo chake nje ya jela na hii itatolewa kwa misingi ya tabia atakayokuwa ameonyesha kwa kipindi hicho.

LAURYN HILL

Kosa: Ukwepaji ushuru

Mwanamuziki huyu aliponea kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kukwepa kulipa kodi. Lauryn alitupwa jela mwaka 2013 lakini akaachiliwa baada ya miezi mitatu kutokana na tabia njema.