KIKOLEZO: Mwaka umeanza na ‘vipindiree’

KIKOLEZO: Mwaka umeanza na ‘vipindiree’

NA SINDA MATIKO

MWAKA umeanza na tayari tumeanza kuwaona maceleb waliolewa kiki wakianza tena kukimbizana na vipindi au ukipenda vipindiree.

2022 tulishushudia maceleb wengi wakishachisha tasnia ya showbiz nchini kwa kuzua vipindi ilimuradi watrendi au wazungumziwe. Baadhi ya hao kwenye listi wameonyesha dalili za kuanzia pale walipoachia.

ERIC OMONDI

Licha ya kuwa ana umri wa miaka 40, mchekeshaji huyo ameamua lazima awe mtu wa kuzungumziwa.
Omondi alijipatia heshima zake miaka ya nyuma kupitia Churchill Show.

Baada ya kuondoka na kuanza kufanya mambo yake taratibu alianza kupoteza dili na siku hizi ni kiki baada ya kiki. Kila kukicha Eric huamka kuzenguana na msanii.

Wiki iliyopita alizenguana na Stivo Simple Boy baada ya msanii huyo kukosa kupiga shoo Mombasa. Eric alidai kuwa Simple Boy alitua Mombasa akiwa na mameneja wanne na wakala msosi wa Sh84,000.

Ilipofika muda wa kupanda steji hakutokea kisa hakuwa amelipwa. Mjadala ukawa ni vipi basi alisafiri hadi Mombasa bila kulipwa hata advansi.

STEVE SIMPLE BOY

Kama hatumiwa na waliomzunguka kwa manufaa yao basi atakuwa naye anafanya kiki azungumziwe.

Mwaka 2022 Simple Boy alitrendi sana kisa mahusiano yake. Baada ya kuachana na mpenzi wake Pritty Vishy, alifeki mahusiano na hata kuishia kuchumbiana na mrembo Jenny Wangui.

Wiki chache akatangaza wameachana. Kumbe ilikuwa ni kipindi tu.

Kwa muda wote walioigiza kuwa wapenzi Steve Simple Boy alikuwa akizungumiziwa kila siku.

Wiki iliyopita baada ya kuchambwa na Eric, aliingia studio na kumwandikia distrac ‘Haya Basi’.

Kwenye wimbo Simple alimkejeli Omondi kwa kumwonea wivu huku akihoji ni kwa nini anaumwa sana na mameneja wake wanne.

Ila kikweli, Steve Simple Boy anahitaji mameneja wanne wa nini?

PRITTY VISHY

Baada ya kuachana na Simple Boy, Vishy amekuwa akizua vipindi vyote vikionekana kumlenga ex wake.

Na kweli vipindiree alivyozua amehakikisha anazungumziwa. Juzi kati aliamua kuachia wimbo ambao ni disstrack aliomwelekezea Simple Boy. Faida ya kiki hizi ni umaarufu mtandaoni.

AMBER RAY

NI mmoja wa masoshiolaiti ambao hawezi kukaa kimya bila ya kuzungumziwa. Hapendi kuona umaa umetuliwa bila ya kumchamba ama kumsifia.

Mwaka 2022 aligonga vichwa vya blogu mara mia fil mia kutokana na mahusiano yake ya kimapenzi akiruka kutoka kwa mwanamume mmoja hadi mwingine ilimuradi ana pesa.

Mwaka huu ameanzia pale pale. Ameuanza kwa kutangaza kuwa ana ujauzito wa mchumba wake wa sasa Kennedy Rapudo ambaye waliachana mwaka jana kabla ya kurudiana.

Wapo wanaodai kikiuma, Amber ataioa mimba kuruka kwa mwanamume mwingine mwenye pesa bila ya kushtuka.

KRG THE DON

Yake huwa ni yale yale tu, kujipiga kifua jinsi alivyo na pesa. Jinsi gani hawezi kujichanganya na watu maskini.

Mwaka 2022 alikwenda hatua na kudai anamiliki klabu ya Casavera ila baadaye ikafichuka kuwa yeye sio hata mumiliki.

Hata hivyo mumiliki wa klabu hiyo hana tatizo na jamaa kujigambia klabu kuwa yake ilimuradi inailetea biashara yake umaarufu.

  • Tags

You can share this post!

Catherine Kasavuli kuzikwa Jumamosi nyumbani Vihiga

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Malezi bora ya watoto yahitajika...

T L