KIKOLEZO: Nabii aliyekataliwa kwao!

KIKOLEZO: Nabii aliyekataliwa kwao!

NA SINDA MATIKO

MWEZI Agosti nilikuwa jijini Kisumu kwa shughuli ya uzinduzi wa jukwaa la utumbuizaji la Dunga Hill Camp lililofadhiliwa na serikali ya Ufaransa.

Shughuli zilikuwa nyingi, wasanii wa Kisumu walioalikwa kutumbuiza walikuwa kibao.

Nilikutana na mmoja wa wanamuziki wa nyimbo za kitamaduni mwenye tajriba kubwa Isaac Gem. Shughuli yake kwenye hafla ile haikuwa kutumbuiza, ila kutoa mwelekeo kwa wale wasanii chipukizi walioalikwa kutumbuiza.

Nilimvuta pembeni na kwa dakika 18, tulipiga stori kibao. Akiwa na miaka 48 sasa, Gem amestaafu na sasa anajishughulisha zaidi na ukuzaji wa vipaji ibukia eneo la Dunga, kando ya ziwa Victoria.

Kwa zaidi ya miaka 15, aliishi kutalii Ulaya wakipiga shoo toka nchi moja hadi nyingine akiwa na bendi ya marehemu mkongwe wa nyimbo za kiasili Job Seda al-maarufu Ayub Ogada. Wawili hao waliishia kuwa marafiki wakubwa hadi Ogada alipofariki dunia.

AFIA KWENYE KOCHI

Imepita sasa miaka mitatu na miezi sita toka alipofariki Ogada.

Alikuwa msanii wa kipekee, ala yake pendwa ya muziki ilikuwa Nyatiti ambayo ni ya kitamaduni kutoka kwa jamii ya Waluo.

Marehemu alipatikana kwenye kiti akiwa amefariki dunia wakati akicheki televisheni nyumbani kwake Nyahera, Kisumu, Februari 1, 2019.

Gem anaamini kifo chake kilisababishwa na mambo kadhaa, lakini kubwa ikiwa ni sonona aliyougua baada ya kurejea Kenya. Nyumbani, hakujulikana kama ilivyokuwa Ulaya ambapo aliheshimika na muziki wake kukubalika mno.

Runinga na stesheni za radio hazikupiga nyimbo zake kama ilivyokuwa majuu. Nyumbani hakuwa staa kama alivyokuwa katika mataifa ya Ulaya ambayo yanasifika kwa kuhusudu sana nyimbo za tamaduni za nje hasa Afrika na walifurahia kuona ala kama Nyatiti.

Ingawaje katika maisha yake ya miaka 63 duniani alifanikiwa kuachia albamu mbili tu; En Mano Kuoyo (1993) na Kodhi (2015) zilizotajwa kuwa ‘World Music’ (muziki maarufu wa kitamaduni Ulaya kutoka mataifa yanaoendelea), Kenya hakutambulika kabisa. Nyumbani, alikuwa hana tofauti na msemo wa ‘nabii hukataliwa kwao’.

Alikuwa ni jiwe la pembeni.Lakini hadi anatangulia mbele za haki, muziki wake ulikubali na bado unazidi kuenziwa hasa katika mataifa ya Marekani, Ujerumani, Uholanzi na Uingereza. Takwimu za Spotify kufikia mwisho wa mwaka 2021 zilionyesha kuwa muziki wake ulikamata nafasi ya nne miongoni mwa nyimbo bora za Kenya, zilizopakuliwa kwenye mtandao huo kutoka mataifa ya nje.

Machoni mwake Gem, hakuna mwanamuziki mwingine Kenya atakayewahi kutokea na kuwa na upekee kwenye sanaa yake kama ilivyokuwa kwa swahiba Ogada. ‘Ndiye msanii mkubwa zaidi kuwahi kutokea na kufanikiwa kuuza muziki wetu wa kitamaduni duniani. Nilitalii naye Ulaya, tukipiga shoo na tuliishi pamoja, alikuwa ni mtu wa kipekee,’ anasema Gem, aliyecheza gitaa kwenye bendi ya mwendazake.

JOB SEDA AWA AYUB OGADA

Baada ya kuzaliwa 1956 Mombasa, wazazi wake walihamia Marekani akiwa na miaka sita. Wazazi wake walikuwa ni watambuizaji vile vile wa muziki wa kitamaduni. Katika miaka ya 1970, burudani Kenya ilikuwa imetawaliwa na muziki wa nje hasa Rhumba kutoka Congo, Latin Pop, Soul, RnB na Jazz.

Muziki wa Kenya uliokuwa unajitahidi kupata sauti ulikuwa Benga lakini ulimezwa na staili hizo za nje. Ogada alitaka kubadilisha hilo. 1986, alihamia Uingereza na kubadilisha jina lake kutoka Job Seda na kuwa Ayub Ogada. Kule akajipatia mafunzo ya muziki na kuamua staili yake itakuwa ni muziki wa kitamaduni, na ala itakuwa nyatiti. Alisainiwa na lebo ya Real World Records kule London na 1993 akadondosha albamu yake ya kwanza iliyozibeba hiti kama vile Kothbiro, Dala na Thum Nyatiti. Albamu hiyo ilimzungusha mataifa mengi ya Ulaya akitumbuiza. Aidha ilimwezesha kupata mchongo wa kutumika kwenye filamu kama Out of Africa (1985) na The Kitchen Toto (1987).

Ifahamike tu, hata Kanye West alimkubali sana Ogada na ndio sababu alimjumulisha kwenye hiti yake ya Yikes iliyotoka 2018. Kwenye wimbo huo, Kanye alitumia kipande cha wimbo wa Kothbiro. Alimlipa hela za kutosha Ogada na pia kuongeza jina lake miongoni mwa watunzi wa Yikes.

OGADA, GEM WARUDI OCHA

Katika miaka ya mapema ya 2000, Gem na Ogada walifanya maamuzi ya kurudi ocha. Kila kitu kina mwisho. Walikuwa wameishi sana Ulaya, upweke wa nyumbani ukawa umewaingia na wakataka sana kurudi nyumbani kuendelea na sanaa yao huku baada ya kuwafurahisha wazungu kwa zaidi ya miaka 15.

“Tulifanya maamuzi hayo. Tulikuwa tumetumbuiza sana kule na ikawa imetuchosha hasa ukizingatia tulikuwa tunatumbuiza nyimbo zile zile kwa sababu ya ukosefu wa muda wa kurekodi kazi mpya kutokana na kuwa tulikuwa tuna shoo za mwaka mzima,” Gem anasema.

Gem anakiri maisha yale yalikuwa matamu sana sababu walikusanya hela mno. Lakini pia anasema, yalikuwa ya kuchosha sana.

“Ukizoea kucheza muziki ule ule kila siku, morali inashuka na pia unachoka kiakili. Ndio pesa tulikuwa tunapata lakini haikuwa kila kitu. Ilifika wakati tulihitaji utulivu wa kiakili,” akafunguka.

Kurudi kwao nyumbani kulimshutua Ogada baada ya kukosa yale mapokezi aliyokuwa akipokea majuu.

“Alikuwa ni kama mfalme vile. Tungeshuka uwanja wa ndege Ulaya, ungewaona kabisa watu wakimwinamia kumpa heshima zake. Tuliporudi, watu hawakuwa wakimtambua na hili nafikiri lilimwingia akilini na kumwathiri sana kisaikolojia,” anafafanua.

WATOTOZ NA POMBE

Kilichofuata ni kwa Ogada kuzama kwenye ulevi na watotoz, ukipenda wanawake. Huu ukawa ndio mwenendo wa maisha yake ikiwa ni jitihada za kujaribu kuyatuliza mawazo yake.

“Nakumbuka wakati fulani 2012 tukiwa tunarekodi albamu yake ya pili baada ya kupata ufadhili wa produsa Trevor Warren kutoka Uingereza, tuliweka kambi Naivasha. Siku moja kabla tuanze kurekodi, Ogada alituambia anakwenda madukani kununua sigara. Hatukumwona kwa siku mbili,” Gem anasimulia.

Walimtafuta kila kona ya jiji la Naivasha ikiwemo mochari na vituo vya polisi.

“Siku ya tatu tuliamua kwenda kuripoti kuwa kapotea. Siku hiyo ndio alitokea saa tano asubuhi akiwa mlevi chakari na machunguduo 12. Waliletwa na teksi tatu. Warren akajawa na hasira sana na akawa ananiuliza kama kweli tutafanikiwa kurekodi,” afichua.

Kutokana na hali ile, walimwacha aendelee na starehe zake za ulevi na machangudoa wake.

“Tukiwa tumelala tukiwazia nini cha kufanya, Ogada alituamsha saa tisa alfajiri na kutuambia tunaweza kurekodi sasa. Aliingia studio na kufikia saa kumi na moja asubuhi tulikuwa tumerekodi nyimbo tano mpya. Ndivyo ilivyorekodiwa albamu ya Kodhi,” asema.

Albamu ya mwisho na ya tatu yake Ogada, Omera ilitoka 2019 akiwa tayari ameshafariki dunia. Omera ni mkusanyiko wa vipande vya nyimbo alizorekodi wakati wa uandalizi wa Kodhi, ila akaziacha nje kwa kuhisi hazikuwa bora.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Mhesh asalimu amri ya KOT!

Wakenya waambiwa wawe tayari kuumia

T L