Makala

KIKOLEZO: Ndege wa mbawa tofauti

November 15th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

UNAAMBIWA ndege wenye mbawa sawa huruka pamoja.

Ni kawaida kuwaona masupastaa wakioana na mastaa wenzao walioko kwenye tasnia moja kwa mfano pale mwigizaji anapoishia kuwa na mwigizaji mwenzake au mwanamuziki akamwoa msanii mwenzake.

Hata hivyo, inakuwa ni kitu spesho zaidi pale supastaa kwenye ulimwengu wa burudani anaishia mikononi mwa supastaa aliye kwenye ulimwengu wa kimichezo. Mifano ya masupastaa wa burudani wanaochora picha hii vyema ni kama:

VICTORIA (Mwimbaji) na DAVID BECKHAM (Soka)

Victoria alipata umaarufu wake miaka ya 90 alipokuwa mmoja wa wanamuziki waliounda bendi maarufu ya Spice Girls. Baada ya kundi hilo kusambaratika 2000, Victoria aliendelea na taaluma yake ya muziki kwa miaka kadhaa kabla ya kuacha kuimba na kugeukia ujasiriamali na uwanamitindo. Kipindi akiwa anatesa kwenye ulimwengu wa sanaa na burudani, mume wake David naye alikuwa akitesa uwanjani akiwa miongoni mwa mastaa tegemeo kwenye kikosi cha Manchester United. Wote wawili walikuwa ni majina makubwa. Kipindi hiki Victoria alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na marehemu mwigizaji Corey Haim lakini mambo hayakuwaendea sawa wakaja kuachana. Hapo ndipo baadaye akaja kukutana na David 1997, kwenye mechi moja ya soka ya mtaani na sogora huyo akamtongoza na hapo ndipo uhusiano wao ulianzia hadi wakaja kuoana miaka miwili baadaye.

GABRIEL UNION (Mwigizaji) na DWAYNE WADE (basiketiboli)

Gabriel ni mmoja wa waigizaji wakali wa Hollywood. Union mwenye miaka 47, amekuwa kwenye ndoa na mchezaji vikapu Wade kwa muda wa miaka mitano sasa. Uhusiano wao ulianza Julai 2010 na baada ya miaka mitatu, staa huyo akiwa anaichezea timu ya Chicago Bulls katika ligi maarufu ya NBA alimchumbia. Agosti 2014, Wade alimwoa Union anayemzidi umri kwa miaka tisa. Mpaka sasa wapo pamoja kila mmoja akiendelea na mishe mishe yake ya kikazi.

SHAKIRA (Mwanamuziki) na GERARD PIQUE (soka)

Beki huyu wa Barcelona alikutana na kichuna mwimbaji Shakira Afrika Kusini, miaka tisa iliyopita kwenye Kombe la Dunia. Shakira alikuwa miongoni mwa wanamuziki walioteuliwa kutumbuiza kwenye sherehe ya ufunguzi wa dimba hilo na utamkumbuka na ile ngoma yake ya Waka Waka. Pique naye alikuwa huko na kikosi cha taifa kushiriki dimba hilo. Wakaanza urafiki wa kawaida hadi Machi 2011 Shakira mwimbaji kutoka Colombia alipothibitisha kuwa wapo kwenye uhusiano na staa huyo. Januari 2013 walijaliwa kumpata mtoto wao wa kwanza wa kiume Milan Pique na Januari, 2015 wakajaliwa wa pili Sasha Pique. Wamedumu pamoja kwa kipindi hicho wakiwa ni wachumba tu.

ENRIQUE IGLESIAS (Mwanamuziki na ANNA KOURNIKOVA (Tenisi)

Wamekuwa wachumba kwa miaka 18 sasa , ila hawajawahi kufunga ndoa wala kupata mtoto. Iglesias mwenye miaka 44, ni supastaa mkubwa aliyeachia hiti nyingi kama vile Hero, Bailando kati ya nyinginezo kibao zilizomwezesha kupata kipato kikubwa. Demu wake Anna 38, ni mwanatenisi mstaafu aliyekutana naye enzi za uchezaji wake. Wamekuwa wapenzi tangu 2001 walipokutana na kupendana.

HAYDEN PANETTIERE (Mwigizaji) na WLADIMIR KLITSCHKO (Boksa)

Hayden ni mwigizaji wa Marekani aliyetokea kwenye filamu kadhaa ikiwemo Heroes, na sasa yupo kwenye Series ya Nashville. Hayden alianza mahusiano na boksa mstaafu ambaye ni bingwa wa zamani wa uzani wa juu Klitschko 2009 lakini wakatengana 2011 kutokana na shuhguli za kikazi. Walirudiana Aprili 2013 na miezi michache baadaye Juni, Hayden akatangaza kuwa kachumbiwa na bondia huyo. Mwaka mmoja baadaye alijifungua mtoto wao wa kwanza. Uhusiano wao ulivunjika Agosti mwaka jana.

CIARA (mwanamuziki) na RUSSELL WILSON (soka)

Nyota wa RnB Ciara alianza kutoka kimapenzi na Wilson mchezaji wa soka ya Marekani 2015 baada ya kutemana na rapa Future. Walifunga ndoa 2016 mjini Liverpool na mpaka sasa ndoa yao ipo juu ya kistari.

JENNIFER LOPEZ (mwanamuziki, mwigizaji) na ALEX RODRIGUEZ (baseball)

J-Lo ni mwanamuziki wa siku nyingi tu na vilevile mwigizaji stadi. Bado kaendelea kuwa na mvuto licha ya umri wake mkubwa kwa sasa akiwa kagonga 49. J-Lo kajaribu ndoa mara nne hivi zikigonga mwamba. Hata hivyo, penzi lake na Alex mchezaji mstaafu wa baseball limezidi kunawiri. Alex mwenye miaka 44 alimchumbia miezi kadhaa mwaka huu. Acha tusubiri ndoa ya tano yake J-Lo.